Akizindua Tamasha la Ulamaa la Qaswida katika
shule ya Benjamen Mkapa jana, Membe alisema uongozi wa heshima ni ule wenye
kuzingatia maadili na unaochukizwa na vitendo vya rushwa.
Alisema rushwa ni kero kubwa kwa wananchi,
hivyo viongozi waadilifu pekee ndiyo wanaoweza kumaliza tatizo hilo.
“Wachujeni viongozi wanaotangaza nia ya
kuwaongoza, muwapime kama wana maadili ya kutosha, wapimeni kama siyo wala
rushwa,” alisema na kuongeza:
“Rushwa ni tatizo kubwa, viongozi wasio na
maadili hawawezi kumaliza tatizo la rushwa. Angalieni ni viongozi gani wenye
sifa na maadili.”
Membe alisema watangaza nia hao wanapaswa
kupimwa na wananchi hadi kwenye dini zao kama ni watu safi ambao wanafaa
kuwaongoza.
Alisema ni vyema wananchi wakatumia muda wa kuwapima
viongozi hao katika mambo mbalimbali na kuepuka kuwa wepesi wa kusikiliza kauli
na kuzikubali.
“Uongozi wa heshima ni ule wenye maadili.
Viongozi bora ni wale watakaochukia vitendo vya rushwa kwa nguvu zote,
jamii imechoka kushuhudia vitendo hivi vinavyonyima haki,” alisema waziri huyo
wa Mambo ya Nje.
Katika tamasha hilo, Membe aliahidi kuchangia
kiasi cha fedha ambacho alikataa kukitaja akisema yeye si mtu wa kutafuta
umaarufu katika masuala kama hayo.
“ Nitachangia katika tamasha hili, lakini sitasema
hadharani ni kiasi gani kwa sababu sitafuti umaarufu mwepesi kupitia hela,”
alisema.
Kuhusu ndoto yake ya urais, Membe alisema
Juni 7, mwaka huu wananchi wakae kwenye runinga zao kwani atatangaza nia ya
kugombea urais na kuomba ridhaa kwa CCM. Tayari makada wengine wa CCM
wameshaweka hadharani dhamira yao ya kuwania kiti cha urais katika Uchaguzi
Mkuu baadaye mwaka huu.
Tayari Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa amezindua mbio hizo mwishoni mwa wiki mjini Arusha na Naibu Waziri wa
Fedha Mwigulu Nchemba alizindua jana mjini Dodoma.
0 comments:
Post a Comment