WACHEZAJI wa kigeni wa klabu ya Yanga ya Jijini Dar es Salaam, Andrey Coutinho pamoja na Kpah Sherman wameanza mazoezi rasmi jana.
Wachezaji hao walikuwa katika mapumziko baada ya kumalizika kwa ligi kuu, ambapo Yanga walinyakua ubingwa huku wakiwa na mechi mbili mkononi.
Akizungumza baada ya mazoezi hayo jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo Hans Van de Pluijm alisema kuwa amefurahishwa na ujio wa wachezaji hao.
Alisema, anaamini kuwa wachezaji hao wataongeza nguvu katika mazoezi ya timu hiyo yaliyoanza wiki iliyopita.
Alisema kuwa timu yake ilianza mazoezi mapema na wachezaji walikuwa wachache kutokana na baadhi yao kuwa likizo na wengine kujiunga na timu za Taifa.
"Nimefurahi wachezaji wangu kurudi kwani naamini wataongeza nguvu katika kikosi changu kilichoanza mazoezi mapema kwa ajili ya maandalizi ya michuano mbalimbali," alisema Pluijm.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa timu ya Yanga Dkt. Jonas Tiboroha alisema wameanza mazoezi mapema kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kirafiki na timu ya Sports Villa ya Uganda kabla ya kuanza michuano ya Kombe la Kagame.
Yanga na Villa wanatarajiwa kucheza mchezo huo Juni 27, mwaka huu uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya kuchangia fedha zitakazotumika kujenga kituo cha kulelea watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
0 comments:
Post a Comment