"Nilirudia uanachama wangu wa CCM mwaka 2011, baada ya kustaafu wadhifa niliokuwa nao kama Jaji Mkuu... Sina doa katika serikali au utumishi wangu; kwa kweli hakuna Mtanzania anayeweza kuninyooshea kidole kwa kupokea au kuhusika na vitendo vya rushwa. Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza..."
Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino
Ramadhan, ametangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akieleza kuwa licha ya kuwapo kwa
utitiri wa wagombea urais, hakuna Mtanzania yeyote anayeweza kumnyooshea kidole
akimtuhumu kupokea au kuhusika na vitendo vya rushwa.
Jaji Ramadhan ambaye ni kada wa 36
kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama chake kuwania kiti hicho, alisema
hakuna mgombea anayemtisha kati ya wote waliomtangulia, kwa kuwa hakuna
mwanajeshi anayeogopa.
Jaji Ramadhani alikuwa akizungumza
na waandishi wa habari jana katika Makao Makuu ya CCM Mjini Dodoma, muda mfupi
baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
“Sina doa katika serikali au
utumishi wangu; kwa kweli hakuna Mtanzania anayeweza kuninyooshea kidole kwa
kupokea au kuhusika na vitendo vya rushwa. Kizuri chajiuza, kibaya
chajitembeza. Mimi ni mwanajeshi, nimestaafu nikiwa Brigedia Jenerali Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Sijui kama kuna mwanajeshi anayeogopa na hakuna
mgombea ninayemuogopa; nikiogopa ina maana mimi si mwanajeshi,” alisema na kuongeza:
“Nina uzoefu wa kutosha, nina uwezo
wa kuwatumikia Watanzania twende huko tunakotaka na kuinua uchumi wetu.
Nimejipima na nimeona nina uwezo wa
kugombea urais kwa sababu nakidhi vigezo vyote vinavyotakiwa kisiasa na
kiuongozi; kilichonisukuma kutangaza nia ya kugombea ni uwezo wangu,
sijashinikizwa na mtu yeyote,” alisema Jaji Ramadhani.
KUJIUNGA NA CCM
Kuhusu utata alijiunga lini na CCCM,
wakati amekuwa mtumishi wa umma kwa zaidi ya miaka 33, Jaji Ramadhani alisema:
“Nilijiunga na CCM mwaka 1969 nikiwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na niliendelea na uanachama wangu hadi 1992 kipindi mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa na kusababisha mabadiliko ya Katiba ambayo yaliweka masharti kwa mtumishi wa umma kutokuwa mwanachama.”
Jaji Ramadhani alisema baada ya
mabadiliko hayo, uanachama wake ndani ya CCM ulisimama hadi mwaka 2010
alipostaafu nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania na kulazimika kurejesha uanachama
wake mwaka 2011 kwa ajili ya kuendelea na masuala ya siasa.
“Nilirudia uanachama wangu wa CCM mwaka 2011, baada ya kustaafu wadhifa niliokuwa nao kama Jaji Mkuu”.
RUSHWA
Kuhusu rushwa, alisema ni tatizo
kubwa nchini. “Tatizo la rushwa katika serikali na nchi yetu ni kubwa, nataka
nilimalize kama chama changu kitaniteua na kushinda nafasi hiyo…wakati
nilipokuwa Jaji Mkuu, nilipambana nalo katika mahakama zetu,” alisema na
kuongeza:
"Nawahakikishia Watanzania nikiwa Rais, ukila rushwa Kilimanjaro, hutahamishiwa Mtwara maana hata waliopo Mtwara ni Watanzania, hawataki mla rushwa.”
KATIBA MPYA
Alipoulizwa msimamo wake kuhusu
mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya, Jaji Ramadhani alisema: “Kwa nafasi
yangu niliyokuwa nayo kama Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
kazi yetu ilikwishamalizika, baada ya kumkabidhi Rais Jakaya Kikwete, Rasimu ya
Pili ya Katiba pale kwenye ukumbi wa Karimjee na Bunge Maalum la Katiba
limemaliza kazi yake, hatua iliyobaki ni wananchi kuamua katika Kura ya Maoni.
Na ndiyo itakayoamua hatma ya Katiba Mpya na si Rais.”
ASUBIRI ILANI
Alisema kwa sasa hawezi kuainisha
vipaumbele vyake lakini iwapo atateuliwa kugombea urais, kazi yake kubwa
itakuwa ni kutekeleza sera na siasa za CCM ambayo itakuwa imeainishwa ndani ya
Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015.
ALIKOTOKEA
Jaji Augustino Ramadhani, alizaliwa
Desemba 28, 1945 mjini Unguja, Zanzibar akiwa mtoto wa pili kati ya wanane
waliozaliwa kwa wazazi wake. Baba yake ni Mathew Douglas Ramadhan, mkazi wa
Zanzibar aliyefariki dunia mwaka 1962.
Alipata elimu ya msingi wilayani Mpwapwa,
Dodoma katika Shule ya Msingi Mpwapwa, kati ya mwaka 1952 -1953 na baadaye
alihamia mkoani Tabora na kusoma darasa la tatu na la nne katika Shule ya
Msingi Town School mwaka 1954 – 1956. Mwaka 1957 – 1958, alisoma darasa la sita
na la saba katika Shule ya Msingi Kazel Hill (sasa Shule ya Msingi
Itetemia), kabla ya kurudi Mpwapwa ambako alihitimu darasa la nane mwaka
1959.
Elimu yake ya sekondari aliipata
katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, kati ya mwaka 1960 hadi 1965.
Baada ya kumaliza elimu ya sekondari alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam Kitivo cha Sheria kati ya mwaka 1966 hadi mwaka 1970.
Baada ya kuhitimu masomo ya Chuo
Kikuu alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria na
aliajiriwa na JWTZ kufanya kazi za uanasheria.
Mwaka 1971, alitunikiwa cheo cha
Luteni akiwa kambi ya Mgulani jijini Dar es Salaam na miaka sita baadaye
akahamishiwa Brigedi ya Faru mkoani Tabora wakati huo akiwa na cheo cha Meja.
Baadaye, Rais wa Zanzibar wakati
huo, Aboud Jumbe Mwinyi, alimwomba na kumwondoa jeshini Jaji Ramadhani na
kumteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)
mwaka 1978.
Oktoba 1978, aliteuliwa kuwa Jaji
Mkuu wa Zanzibar. Mabadiliko mengine yalitokea Machi, 1979 na kurudishwa
jeshini, ambako hakukaa muda mrefu; akahamishiwa vitani Uganda kuendesha
Mahakama za Kijeshi (akiwa na cheo cha Luteni Kanali).
Baada ya vita, alirejea Zanzibar na
kurudishwa kwenye utumishi wa kiraia ambako Januari 1980, aliapishwa kuwa Jaji
Mkuu wa Zanzibar.
Miaka tisa baadaye, aliteuliwa kuwa
Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.
Alidumu katika Ujaji wa Mahakama ya
Rufaa kwa miaka minne hadi alipoteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (Nec) mwaka 1993.
Alikaa Nec hadi Oktoba 2002
alipohamishiwa Zanzibar kufanya kazi kama Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (Zec) hadi Oktoba 2007. Mwaka 2007 aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete,
kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania hadi alipostaafu mwaka 2010.
Jaji Ramadhani kwa sasa ni Rais wa
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu yenye makao yake jijini Arusha.
SHEIN KUCHUKUA FOMU LEO
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed
Shein, leo anatarajia kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania tena nafasi ya
urais wa Zanzibar.
Dk. Shein atachukua fomu hizo katika
ofisi kuu ya CCM Kisiwandui.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, Itikadi na
Uenezi Zanzibar, Waride Bakari Jabu, Dk. Shein atakabidhiwa fomu hiyo na Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
Waride alisema baada ya kukabidhiwa
fomu hiyo, Dk. Shein atazungumza na viongozi wa CCM wakiwamo wa wilaya na mikoa
ya Unguja.
Wengine ni wazee wa CCM na waasisi
wa mikoa mitatu ya Unguja na Pemba.
Dk. Shein anakuwa mgombea wa kwanza
wa CCM kuchukua fomu kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar. Kwa mujibu wa taarifa
hiyo, hadi sasa hakuna jina la mwanachama wa CCM aliyetangaza nia ya kutaka
kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi Zanzibar.
Mwishoni mwa wiki, wenyeviti wa CCM
wa mikoa sita kichama, walitoa tamko la kumuomba Dk. Shein kuchukua fomu
kuwania nafasi hiyo kutokana na uwezo wake wa kuisimamia na kutekeleza ilani ya
chama hicho kwa mafanikio makubwa.
Dk. Shein ataungana na mgombea wa
nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (Cuf), Maalim Seif
Sharif Hamad, ambaye ameshachukua fomu ya kuwania nafasi hiyo baada ya
kuidhinishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama chake.
0 comments:
Post a Comment