Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (53), amehukumiwa kwenda jela
mwaka mmoja au kulipa faini ya Shilingi milioni moja baada ya kupatikana na hatia
ya kumshambulia Mwangalizi wa Ndani wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Nassir
Uronu.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya
Hakimu Mkazi Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro jana.
Hata hivyo, Mbowe alifanikiwa kulipa
kiasi hicho cha faini na hivyo kuepuka kwenda kutumikia kifungo cha mwaka mmoja
jela.
Mbowe alikuwa akikabiliwa na kesi
namba 73 ya mwaka 2011 iliyofunguliwa na Nassir; aliyedai kushambuliwa kwa
kipigo akiwa katika Zahanati ya kijiji cha Nshara kata ya Machame Kaskazini
Wilaya ya Hai, mwaka 2010.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Wilaya za Hai na Siha, Denis Mpelembwa, alisema mahakama hiyo
imemtia hatiani Mbowe kwa kosa la kumshambulia Nassir kinyume cha kifungu cha
24 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 cha Sheria iliyofanyiwa Mrekebisho mwaka
2002.
“Mahakama imekuona una hatia katika kosa linalokukabili na inakuhukumu kulipa faini ya Shilingi milioni moja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela,” alisema Hakimu Mpelembwa.
Awali, upande wa utetezi ukiongozwa
na Wakili Issa Rajabu, aliyekuwa akisaidiana na Wakili Albert Msando; aliiomba
mahakama hiyo kumpunguzia adhabu mteja wake (Mbowe), kwa madai kwamba ni kosa
lake la kwanza.
Kesi hiyo ya uchaguzi mkuu uliopita,
imekuwa ikivuta hisia za wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Kilimanjaro,
Arusha, Manyara na Tanga hasa kutokana na nguvu ya kisiasa aliyonayo Mwenyekiti
huyo wa Chadema na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Katika uchaguzi huo, Nassir alikuwa
Mwangalizi wa Ndani wa Uchaguzi Mkuu akiliwakilisha Baraza la Waislamu Tanzania
(Bakwata).
Hata hivyo, Mbowe aliyekuwa mgombea
ubunge wa Jimbo la Hai kwa tiketi ya Chadema, aliibuka mshindi kwa kupata kura
28,585, akifuatiwa na Fuya Kimbita (CCM), kura 23,349, Hawa Kihogo (UDP) 258 na
Petro Kisimbo (TLP) kura 135.
Wakili wa Jamhuri katika kesi hiyo,
Simon Feo, ambaye ni Mwendesha Mashitaka wa Polisi, aliieleza mahakama
hiyo kwamba kutokana na ukubwa wa kosa, anaiomba mahakama impatie adhabu
stahiki kwa vile makosa kama hayo yanaharibu taswira ya jamii na hasa
ikizingatiwa kuwa Mbowe ni kiongozi wa kitaifa.
Baada ya Hakimu Mpelembwa kumaliza
kusoma hukumu hiyo, Mbowe alitolewa nje ya mahakama chini ya ulinzi mkali wa
Polisi waliokuwa wameimarisha ulinzi katika viunga vya mahakama hiyo na
kumshikilia kwa zaidi ya saa mbili; hadi alipofanikiwa kulipa faini ya Shilingi
millioni moja na kuachiwa huru.
Akiwa chini ya ulinzi wa Polisi,
wanachama na wafuasi wa Chadema waliofurika mahakamani hapo, walilazimika
kujichangisha na kisha kulipia faini hiyo kupitia Benki ya NMB na baadaye
kuwasilisha mahakamani stakabadhi yenye namba 0317489.
0 comments:
Post a Comment