MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi) ameitaka
Serikali kuwasilisha bungeni taarifa ya kashfa ya ununuzi wa mabehewa
feki katika Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kusababisha hasara ya Sh
bilioni 230.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni jana, mbunge huyo
alisimama kuomba muongoza wa Spika kwamba kutokana na unyeti wa jambo
hilo, ikiwa ni pamoja na madai kwamba Kampuni iliyopewa zabuni ya
kuagiza mabehewa hayo haikuwa na uwezo huo, kwa nini suala hilo
lisipelekwe bungeni kujadiliwa.
Mbunge huyo alihoji kwamba si vyema suala hilo likazungumzwa na
kuishia nje ya Bunge badala ya kujadiliwa na kupata ufumbuzi, lakini
akijibu muongozo huo Spika wa Bunge, Anna Makinda alisema jambo hilo ni
la kisekta na kwamba lilitakiwa lianzie kwenye kamati inayohusika.
Hata hivyo, akichangia muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 wenye
lengo la kuzifanyia marekebisho sheria 16 zinazohusu masuala ya fedha,
kodi, ushuru na tozo mbalimbali nchini uliowasilishwa jana na Waziri wa
Fedha, Saada Mkuya Salum, mbunge huyo alirudia suala hilo la TRL akisema
kuna haja ya jambo hilo kufanyiwa kazi kwani matumizi mabovu ya sh
bilioni 230 hayawezi kufumbiwa macho.
Alisisitiza taarifa ya jambo hilo ipelekwe bungeni na kuhoji kampuni
hiyo iliyohusika na kuagiza zabuni hiyo imelipwaje fedha zote hizo kabla
ya kutimiza masharti na kumuomba Spika Makinda aagize taarifa
iwasilishwe bungeni na sio kuwalinda.
Kauli hiyo ya kuwalinda ilimfanya Spika Makinda kusimama na kusema
halindi mtu na kumtaka mchangiaji ajielekeze katika hoja husika.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta wakati akifanya majumuisho ya bajeti
yake Mei mwaka huu, alisema maofisa watano wa serikali wanatarajiwa
kupandishwa kizimbani hivi karibuni, kutokana na kashfa ya uagizaji wa
mabehewa 274 kutoka India, huku wengine wakitarajiwa kuchukuliwa hatua
za kiutawala.
Aprili mwaka huu, Sitta alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Kipallo Kisamfu na wengine wanne, ili
kupisha uchunguzi wa kashfa ya uingizaji wa mabehewa feki ya mizigo.
Wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Mitandao, Ngosomwile
Ngosomiles, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper
Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment