Sherehe hizo ziliandaliwa katika uwanja wa kitaifa
wa Nyayo,ambapo zaidi ya watu 30,000 walihudhuria.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali
nchini Kenya wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, na Naibu Rais William Ruto.
Aidha Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Naibu Rais
wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa,waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Balozi
Berhane Gebre-Christos ,na Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Abdulrahman Kinana
pamoja na viongozi wengine walihudhuria sherehe hizo.
Vifijo,shangwe na nderemo zilitanda katika
maadhimisho ya 52 ya sikukuu ya Madaraka katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo,huku
nyimbo za kizalendo zikihanikiza.
Wakenya kutoka matabaka mbalimbali pamoja na wageni
walihudhuria sherehe hizi na angalau kupata fursa ya kusikiza hotuba ya rais.
Sikukuu ya madaraka inaadhimishwa kukumbuka siku
ambayo Kenya ilipata idhini ya kujitawala kutoka kwa mkoloni.
Katika hotuba yake kwa taifa,Rais Uhuru Kenyatta
alisema ulaji rushwa ndio tatizo kubwa linaloikabili Kenya kutokana na idadi
kubwa ya maafisa wa umma wanaojikita katika jambo hilo.
Rais Kenyatta aliwahimiza wananchi kusimama kidete
na kupinga ulaji rushwa.
Madaraka day 7 "Leo nawahimiza kila mmoja wenu
kujitolea kupiga vita tamaduni ya ulaji rushwa,hongo na mambo yote maovu ambayo
yanaenda kinyume na maslahi ya umma"
Rais Kenyatta pia aliahidi kwamba serikali yake
itafanya ufuatiliaji na kuwachukulia hatua wote waliotajwa katika uchunguzi wa
hivi karibuni kuhusiana na ulaji rushwa,suala lililowaathiri baadhi ya maafisa
wakuu serikalini ikiwa ni pamoja na mawaziri.
Aidha Rais Kenyatta alisema serikali yake bado
inazidi kupambana na wanamgambo wa Al Shabaab na kuzuia usajili wa vijana
katika kundi hilo.Alisema kundi hilo kinawalaghai vijana katika misingi ya dini
kwa mambo ya uongo.
Kenyatta alitoa wito kwa wananchi kutoa ripoti
kuhusu mtu yeyote aliyejiunga na kikosi cha Al Shabaab,kwa sababu wote
wanaojiunga na kikosi hicho ni maadui.
Madraka day 9 "Huyu ni adui ambaye ameharibiwa
na kutiwa siasa chafu.Sisi sote twaelewa ya kwamba hakuna dini ambayo
inamuamini Mwenyezi mungu inaweza kusema inaruhusiwa kuua au kukata mtu
kichwa,hiyo ni lugha iliyowekwa na watu wachache kuharibu watoto wetu.Mimi
nawaomba wakenya wote lazima tuwe macho"
Aidha Rais Kenyatta aliagiza kwamba asilimia 40 ya
bidhaa na huduma zinazotumiwa na serikali lazima ziwe ni za kutoka nchini.
Alisema agizo hilo litaanza kutekelezwa katika mwaka
ujao wa kifedha kuanzia mwezi Julai.
"Serikali yangu itahakikisha kwamba katika ujao
wa kifedha tutaweka vikwazo vya bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na serikali
lazima ziwe ni kutoka hapa nchini"
Wakati huohuo Naibu Rais wa Afrika Kusini Cyril
Ramaphosa aliomba radhi kwa niaba ya serikali yake kwa wakenya kutokana na
mashambulizi ya kibaguzi kwa waafrika yaliyotekelezwa na wananchi wa Afrika
kusini nchini humo hivi majuzi.
"Kama mnavyojua hivi karibuni tulipitia wakati
mgumu wakati baadhi ya waafrika kusini walipoanza kuwashambulia waafrika wenzao
nchini Afrika Kusini.Nasimama hapa kuwaomba radhi kama alivyoomba Rais Jacob
Zuma kwa viongozi wa Afrika.Nasimama hapa kuomba msamaha kwa yaliyotokea"
Mariphosa alisema tatizo hilo linashughulikiwa na
wakenya pamoja na waafrika wote wanakaribishwa nchini Afrika Kusini wakati
wowote.
Naye Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema kwamba
kundi la Al shabaab limeshindwa na ndio maana linavamia watu wasio na hatia.
Aidha Museveni alitoa rambirambi zake kwa Kenya
kutokana na shambulizi la Garissa lililopelekea vifo vya wanafunzi 145 na
maafisa wawili wa polisi.
Siku ya Madaraka huadhimishwa kila mwaka tarehe 1
Juni nchini Kenya.Hii ni siku ambayo Kenya ilipata idhini ya kujitawala yenyewe
mwka 1963,kabla ya kupata uhuru kamili na kuwa jamhuri mwaka huohuo mnamo
tarehe 12 Desemba.
0 comments:
Post a Comment