Image
Image

Kilio cha wadau kwa Taifa Stars.


TIMU ya taifa ya mpira wa miguu ‘Taifa Stars’ imeshiriki na kutolewa katika hatua za awali katika michuano ya Kombe la Cosafa , nchini Afrika Kusini ikiwa kama mgeni mwalikwa.
Ni mashindano ya kila mwaka yanayoshirikisha timu kutoka nchi za Kusini mwa Afrika , mashindano hayo huandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Mguu Kusini mwa Afrika la Soka (Cosafa).
Ushiriki wa Taifa Star kwenye mashindano hayo ulileta faraja kwa wapenzi wa kabumbu kwani wengi waliona mashindano hayo ya kimataifa kuwa ni kipimo cha kizuri timu hiyo kimataifa ikizingatiwa inakabiliwa na mashindano hivi karibuni.
Mpira wa miguu ni mchezo wenye mashabiki wengi duniani kuliko mwinginem hivyo timu inapofanya vibaya husababisha watu wengi kuumia.
Mpira wa miguu (soka au kandanda) ni mchezo unaochezwa na jumla ya wachezaji ishirini na wawili katika timu mbili husika, kila timu ikiwa na wachezaji kumi na mmoja.
Lengo hasa la mchezo huu ni wachezaji kuumiliki mpira kwa kutumia miguu na kuuingiza katika wavu wa wapinzani mara nyingi zaidi.
Matumizi ya mikono ni marufuku isipokuwa kwa mlinda mlango katika eneo maalumu na wakati wa kurudisha mpira baada ya ya kutoka nje ya uwanja.
Haina ubishi kuwa soka ni mchezo maarufu na wa kwanza, unaopendwa na watu wengi zaidi nchini Tanzania.
Kama ilivyo baadhi ya michezo mingine, soka ilianzishwa na wakoloni walipokuja nchini Tanzania, walikuta michezo ya jadi kama vile riadha na wakaingiza michezo mipya na soka kuwa miongoni mwao.
Kwa bahati, mchezo huo umejipatia umaarufu kushinda michezo mingine.
Tanzania ina timu ya soka ya Taifa ya wanaume inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kukuza na kuhimiza na kuendeleza soka, shirikisho hilo lilianzisha Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu tangu mwaka 1965, wakati huo yalijulikana kama Ligi ya mpira wa miguu ya Daraja ya Kwanza.
Katika michuano iliyofanyika hivi karibuni inayoandaliwa nchi za Kusini mwa Afrika ‘Cosafa’, Taifa Stars ilionesha kiwango cha chini kabisa , jambo lililosababisha kupoteza kupoteza na kuondolewa mapema.
Timu hiyo ilifungwa na timu ya Swaziland bao 1-0, Madagascar mabao 2-0 na Lesotho bao 1-0.
Kwa kipigo hicho, timu ya Taifa ilitolewa kwa hatua za awali. Stars ilichezailitolewa bila ya kupata pointi na mabao.
Kutolewa katika hatua za mwanzo kwa timu hiyo ya taifa ya mpira wa miguu licha ya kuwaumiza mashabiki, umekuwa ni mwendelezo wa siku zote wa timu za taifa za michezo mbalimbali kufanya vibaya Kimataifa.
Maoni, lawama zimekuwa zikitolewa na wadau wa soka kwa klabu za michezo, serikali na wizara ya husika ya michezo.
Mwandishi wa Makala haya alipata nafasi kukutana wadau wa mpira wa miguu ili kutoa maoni yao ambayo baadhi yake yanaweza kurejesha heshima ya mchezo huo ndani na nje ya nchi.
Juma Mtembo anaelekeza lawama kwa Shirikisho la Mpira wa Muguu Tanzania, anasema: Wanaorudisha nyuma maendeleo ya timu ya Taifa ni TFF.
Uongozi wa Jamal Malinzi unaingiza Uyanga na Simba ndani ya TFF. Anaelekeza pia lawama kwenye kamati za kuteua wachezaji wanaochezea timu hiyo, anafika mbali zaidi kuwa kamati hizo zinaangalia zaidi kitu kidogo yaani rushwa wakati wa uteuzi.
Anabainisha zaidi kwa kusema kuwa hata akiletwa José Mourinho timu yetu ya Taifa bado haitafanya vizuri. Mourinho ni mmoja wa makocha bora barani Ulaya katika msimu ulioisha ameisaidia Chelsea kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.
Katembo anatoa rai kwa Rais wa TFF, Jamali Malinzi kuwa aache kuingiza Uyanga katika timu ya Taifa, pia anasema kuwa, kwa utashi wa sasa wa shirikisho hilo, hautaweza kuleta mageuzi ya kweli ndani ya mchezo huo.
Kosa kubwa walilofanya TFF ni kutoandaa timu ya Taifa kwa msingi wa kuwaendeleza vijanam mfano ni watoto waliochukua kombe la dunia Brazil.
Watoto wa mitaani wakishikilia Kombe la Dunia walilonyakua Brazil mwaka jana.
Timu ya taifa ya Tanzania ya watoto wa mitaani ilinyakua Kombe la Dunia kwa 2014, katika mashindano yaliyozishirikisha timu za mataifa mbalimbali duniani huko Rio de Janeiro, nchini Brazil.
Ikiwa imetinga fainali za Kombe la Dunia kwa watoto wa mitaani kwa mara ya pili mfululizo, timu hiyo ya Tanzania ilitwaa Kombe la Dunia katika mashindano yajulikayo kama “Street Child World Cup” Rio de Janeiro nchini Brazil.
Katika mechi ya fainali hizo, Tanzania iliibanjua Burundi iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kulinyakua kombe hilo kwa mabao 3-1 huku mchezaji kiungo mshambuliaji wa Tanzania Frank William akipiga funga mabao matatu na kuwa nyota wa mchezo.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Tanzania ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-0. Kipindi cha pili iliongeza bao la tatu. Burundi ilipata bao la kufutia machozi zikiwa zimebakia dakika nne mpira kumalizika.
Tanzania ilitwaa ubingwa huo baada ya kuonesha kiwango cha juu hata kuzishinda timu ngumu kama Burundi, Marekani, Indonesia, Nicarague, Ufilipino na Argentina.
Mlinda mlango wa Tanzania Emmanuel alichaguliwa kuwa kipa bora wa michuano hiyo ya kombe la dunia.
Hii ilikuwa mara ya pili kwa timu ya Tanzania kutinga fainali za michuano hiyo ya dunia kwa watoto wa mitaani inayofanyika siku chache kabla ya fainali za Kombe la Dunia kuanza Juni 2014.
Fainali za michuano hiyo iliyofanyika Durban Afrika Kusini mwaka 2010, Tanzania ilifungwa na India katika fainali.
Mashindano haya hutambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu, yaani Fifa, Katembo anasema kosa lingine linalofanywa na shirikisho hilo ni kutoingilia mpangilio wa Kocha wa timu ya taifa kwani yeye anapawapanga wachezaji wa timu hiyo kwa nafasi zisizo zao.
Anasema kuwa hata kocha huyo kuonesha udhaifu wa ufundishaji, lakini bado amepewa mechi nyingine mbili za michuano Kombe la Mataifa ya Afrika.
Katembo anatoa rai kuwa benchi la ufundi la timu ya Taifa livunjwe.
Mwandishi wa Makala hii alipotaka maoni kuhusu kuimarishwa kwa timu za mpira wa miguu kwenye vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kuwa na uwezekano wa kupata wachezaji wenye uwezo na nguvu, kwani vyombo hivyo, wachezaji wake wamekuwa wakifanya vizuri nje ya nchi, Juma Katembo alisema kuwa hilo pia linaweza kusaidia kuwa na wachezaji wenye nidhamu na nguvu.
Katembo anasema kuwa mpira wa miguu ukitumiwa vizuri nchi itafaidika zaidi , chanzo cha michezo kimefukiwa, kwani michezo ina faida nyingi kwa Taifa, anamalizia Juma Katembo.
Katembo pia anaelekeza lawama kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kuwa anaegemea zaidi upande wa Yanga kuliko timu ya Taifa.
Juma anasema kuwa TFF hawaangalii wala kuzingatia sheria za Uchaguzi, viongozi hao pamoja na Waandishi wa Habari wanachoangalia ni Uyanga na Usimba tu!
“Malinzi na Waandishi wa Habari wameharibu soka la Tanzania! TFF na Waandishi wa Habari wasiangalie na kuegemea Simba na Yanga tu, wanakalia kuichambua timu ya Simba, wafuate demokrasia!
Anaitaka TFF iangalie Katiba ya Yanga kuhusu uongozi.
Mdau mwingine Said Rashidi anaunga mkono kauli na mawazo ya Juma Katembo. Yeye anasema kuwa soka la Tanzania limeharibiwa na Waandishi wa habari, kwani uandishi wao ni wa kubomoa wala si wakujenga, wengi wao wanajiingiza kwenye Usimba na Uyanga.
Anasema kuwa wachezaji wa timu ya Taifa hawana stamina pia hawajengwi kisaikolojia.
Anataja kuwa kosa lililolifanyika ni kuiachia timu ya vijana wa mitaani iliyochukua kombe la dunia nchini Brazil, hao ndio wangeaandaliwa zaidi na kupandishwa hadi ngazi ya timu ya Taifa, anasema kuwa mfano mzuri ni Thomas Ulimwengu wangemchanganya na Cannavaro, tujenge msingi wa timu ya vijana!
Jabiri Makunga, mdau wa mpira wa miguu anasema kuwa , kwa sababu ya kutokuwa makini kwa viongozi wa mpira wa miguu na klabu imechangia kufika tulipofikia.
Anatoa maoni yake kuhusu timu ya Taifa kuwa: Siyo kuwa timu hiyo imeingiliwa na watu wasiojua Mpira wa Miguu bali ni ‘ubinafsi tu’ umeharibu timu ya taifa, wachezaji wanaochukuliwa kutoka katika klabu, tunawaona bora kwa sababu wanapangiwa matokeo, hawana ubora, anasema Makunga.
Antoa ushauri kuwa ligi zote ziwe ni za kihalali na waamuzi wachezeshe mechi kihalali.
Ameitaka serikali kuisimamia timu ya Taifa kama ilivyokuwa kwa Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda.
Salum Masenga shabiki wa Stars, yeye anaitaka TFF ichague timu ya Taifa ya kudumu, anasema kuwa kwa sasa timu iliyopo ni ya ‘Majaribio’ tu siyo Timu ya Taifa.
” Isichaguliwe timu kila mwaka, tunachagua na kubomoa timu kila mwaka! Tunabomoa na kuchagua!”
Masenga anasema kuwa timu ya Taifa iliyotolewa hivi majuzi kwenye michuano ya Cosafa, si mbaya, unatakiwa kuendelea kujengwa na kuimarishwa zaidi, kinachotakiwa ni kuongeza wachezaji wenye uwezo na uzoefu, anatoa wito kuwa timu hiyo ijengwe kwanza, halafu iigizwe kwenye mashindano.
Anasema wachezaji wanapokaa kambini muda mrefu wanajengwa kwa stamina na saikolojia, wasikae uraiani.
Anatoa rai kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwa Jakaya Kikwete avae jezi ya Taifa kila mwanzo wa mwezi na mwisho wa mwezi asimamie mazoezi ya timu hiyo kama ilivyokuwa kwa Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda na ‘KK Eleven’ timu ya taifa ya Zambia.
Kocha anavuja timu mara nne, anatoa mfano kuwa shamba linatakiwa kulimwa kwa kuliboresha kwa nguvu zako zote, hata kulimwagilia maji!
Kauza Jumbe, mdau mwingine wa mpira wa miguu anasema kuwa yeye binafsi aliacha kwenda uwanjani kuangalia mpira kwa kuwa haridhishwi unavyochezeshwa.
Jumbe anasema,” Tunataka ushindi bila kujipanga, hata tukimleta kocha Jose Mourinho aje kufundisha Timu ya Taifa ni kazi bure!
Jumbe anasema kuwa iundwe timu ya vijana wenye umri wa miaka 17, vijana hao waandaliwe kwa muda wa miaka minne, ukijengwa msingi huo hata kombe la dunia linawekwa kushukuliwa na timu hiyo, anasema Jumbe.
Pia ameitaka TFF kutowadharau makocha wazawa kwa ushauri wao, kuwe na malengo ya wachezaji, ujengwe timu ya Vijana endelevu itakayowarithi wakongwe.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment