Aidha, inakadiriwa kuwa kisukari pekee kimeathiri maisha ya watu
takribani milioni 371 duniani kote huku asilimia 80 ya idadi hiyo
ikiishi katika nchi zenye uchumi wa kati na maskini.
Nchini Tanzania, takribani watu tisa kati 100 wana ugonjwa wa
kisukari na kwamba mtu mzima mmoja kati ya watatu, ana tatizo la
shinikizo la juu la damu.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi kutoka
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Hauson Rweumbiza, wakati wa semina ya
siku moja iliyowashirikisha waandishi wa habari wa kutoka vyombo
mbalimbali.
Lengo la semina hiyo lilikuwa ni kuzungumzia magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza.
Alisema gharama ya kukabiliana na magonjwa ya siyo ya kuambukiza
duniani kote ni mabilioni ya dola na hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa
rasilimali finyu zilizopo.
"Kwa mwaka 2010, Shirika la Afya Duniani lilikadiria kuwa jumla ya
gharama zinazohusiana na kisukari zilifikia Dola bilioni 378 duniani
kote na kiasi hicho cha fedha kinaweza kufikia Dola bilioni 490 ifikapo
mwaka 2030,'' alisema.
Aliongeza kuwa nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania na
zilizoendelea, pia hazina rasilimali za kutosha kutibu watu wote
wanaobainika kuwa na kisukari.
Aliongeza kuwa jitihada za kukabiliana na tatizo hilo ni budi
zikajikita zaidi katika mitazamo jumuishi inayolenga kukinga ili
kupunguza kiwango cha magonjwa yasiyoambukiza kwenye jamii.
Alisema kwa kufahamu hilo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa
kushirikiana na Taasisi ya Kisukari Tanzania pamoja na wadau wengine,
imeandaa kitabu kwa lengo la kupunguza athari na matokeo mapya ya
magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwenye jamii ya Watanzania.
Alifafanua kuwa kitabu hicho kilichoandikwa kwa lugha nyepesi,
kinajumuisha taarifa muhimu na kumpa nafasi kila mtu kuchagua mtindo wa
maisha utakaomwezesha kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa
usioambukiza.
Aidha, aliwataka wananchi kuachana na uzushi ambao umekuwa
ukitolewa na baadhi ya wafanyabiashara kuwa mayai ya kware hutibu
ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na kuongeza kinga kwa watu wenye
Ukimwi.
"Watu wapo kibiashara zaidi, mayai ya kware ni kama mayai ya kuku
na bata na hayatibu kisukari, shinikizo la damu wala kuongeza kinga kwa
watu wenye Ukimwi," alisisitiza.
Hali kadhalika, aliwataka wagonjwa wa kisukari kuacha kutumia asali
kwani wamekuwa wakilaghaiwa na wafanyabiashara kwamba ni mbadala wa
sukari.
Naye Mratibu kutoka Taasisi ya Kisukari hapa nchini, John Gadina,
alisema utafiti uliofanyika mwaka 2012, ulionyesha kuwa asilimia tisa ya
Watanzania waligundulika kuwa na kisukari huku Wilaya ya Temeke
ikiongoza.
Alisema ugonjwa huo umewakumba vijana na watu wenye umri mkubwa na
kwamba serikali mpaka sasa imefikia kutoa huduma hiyo kwa asilimia 75
ambapo kila palipo na hospitali panakuwa na kitengo cha kutoa huduma za
ugonjwa huo.
Alisema sababu ya Wilaya ya Temeke kuwa na wagonjwa wengi imetokana
na ulaji kwa wingi wa vyakula vya nazi, chapati, wali pasipo kufanya
mazoezi.
0 comments:
Post a Comment