Majigambo hayo yametolewa kwa nyakati tofauti
na mamlaka mbalimbali za Serikali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete aliyesema kuwa
Serikali yake inajivunia maendeleo katika sekta ya elimu.
Hata jana, Bunge la bajeti linaloendelea
mjini Dodoma lilielezwa kuwa sekta hiyo imefanikiwa kwa asilimia 81 na hivyo
kushika nafasi ya kwanza ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN).
Awali, Rais Kikwete katika hotuba yake
aliyoitoa katika Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), uliofanyika
jijini Arusha Mei 28, alisema Serikali yake inajivunia mafanikio makubwa katika
sekta ya elimu, licha ya kwamba bado zipo changamoto zinazopaswa kufanyiwa
kazi.
Alielezea mafanikio hayo kuwa ni pamoja na
uanzishwaji wa programu za walimu wa kozi za muda mfupi au walimu wa leseni,
ongezeko la kiwango cha uandikishaji wanafunzi, ujenzi wa maabara na kuondoa
utitiri wa vyombo vya kuhudumia madai ya walimu.
Pamoja na mafanikio haya, ni ukweli usio na
shaka kuwa uanzishwaji wa programu za kozi za muda mfupi za ualimu, ni sababu
mojawapo ya kushuka kwa kiwango cha elimu nchini. Hili limekuwa likilalamikiwa
mara kwa mara na wadau wa elimu.
Kimsingi, Watanzania hawajasahau makovu
waliyoyapata kutokana na walimu wa UPE na wale wa ‘vodafasta’.
Katika risala yao, walimu hao walipendekeza
mambo tisa ambayo walitaka Serikali iyafanyie kazi ili kuboresha sekta ya
elimu.
Baadhi ya mambo hayo waliyoyatoa kama wito
kwa Rais Kikwete ni kufanyia mabadiliko ya mafao ya pensheni, uboreshwaji wa
idara za ukaguzi wa shule na urejeshwaji wa posho za kufundishia.
Hata hivyo, wakati Rais Kikwete na mamlaka
nyingine za Serikali zikieleza mafanikio hayo, Kamati ya Bunge ya Huduma za
Jamii imesema hadi kufikia Machi, baadhi ya taasisi zilizopo chini ya Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi zilikuwa hazijapata hata fedha za maendeleo.
Kamati hiyo imeeleza pamoja na kuwapo kwa
takwimu za mafanikio, wanafunzi bado wanakaa chini kwa kukosa madawati, bado
kuna uhaba wa walimu, madarasa na vifaa vya kufundishia, huku karo katika shule
binafsi zikiendelea kuwa juu.
Matatizo hayo ndiyo yaliyoifanya kambi
rasmi ya upinzani bungeni kuhoji aina ya uwekezaji uliofanyika katika
sekta ya elimu hadi ikafikia mafanikio makubwa ya kujivunia kama inavyoelezwa
na mamlaka hizo za Serikali.
0 comments:
Post a Comment