Image
Image

Mart Nooij amesikitika kuondoka Tanzania akiwa hajafanikiwa kuipa timu hiyo ya taifa mafanikio.

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij amesikitika kuondoka Tanzania akiwa hajafanikiwa kuipa timu hiyo ya taifa mafanikio tofauti na alikowahi kufanya kazi ambako alifanya vizuri.Nooij alikuwa akizungumza jana kwenye mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam ambako aliwashukuru wachezaji, wadhamini wa Stars na Watanzania kwa ushirikiano walioonesha tangu alipoteuliwa mwaka jana.
Mwishoni mwa wiki, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kufuta kibarua cha Mholanzi huyo kwa kushindwa kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ikiwemo ule wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) dhidi ya Uganda baada ya kufungwa mabao 3-0.
Nooij alisema kufanya vibaya katika michuano hiyo, hawezi kumlaumu mtu yeyote kwani wachezaji wake walikuwa wakijituma vizuri isipokuwa bahati haikuwa ya kwao.
“Nasikitika kwa kushindwa kufanya vizuri, najua kila familia ya Tanzania inahuzunika kuona timu inafanya vibaya, sikuwa na bahati kwa hapa, ila nilikopita nilifanya vizuri, tatizo lilikuwa ni hapa,” alisema Nooij.
Alisema anakubali kuwajibika kwa yote yaliyotokea kwani hawezi kumlaumu yeyote wala kumkosoa yeyote. Kocha huyo anaondoka huku akiacha mwito kwa TFF kuweka nguvu katika soka la vijana ili kujenga timu bora itakayofanya vizuri wakati ujao.
Nooij aliyejiunga na Stars Aprili 25, mwaka jana akichukua mikoba ya Kim Poulsen wa Denmark, ameiongoza Stars katika mechi 18 huku kati ya hizo akishinda tatu pekee, sare sita na kufungwa tisa.
Mholanzi huyo anajiona kama mwenye bahati mbaya, kwani katika maeneo aliyofanya kazi haikuwa hivi.
Aliwahi kuwa Kocha wa timu ya vijana ya Burkina Faso ya miaka 20 katika Kombe la Dunia mwaka 2003 kabla ya mwaka 2004 kuwa msaidizi wa muda wa FC Volendum ya Uholanzi.
Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Msumbiji na akiwa na timu hiyo, ilifuzu kwa fainali za Afcon mwaka 2010 baada ya kuzikosa kwa miaka 12.
Baada ya kushindwa kufuzu kwa fainali za Afcon za mwaka 2012, alijiuzulu kazi hiyo Septemba mwaka huo. Aprili 12, 2012 aliteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa Klabu ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Santos lakini alifukuzwa Desemba 18, mwaka huo.
Na mwaka 2013, Nooij aliteuliwa kuwa Kocha wa Saint George ya Ethiopia na miezi mitano baadaye alikubali kuifundisha Tanzania.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema jana kuwa watamlipa kocha huyo fedha zake za kuvunja mkataba ambazo zinakadiriwa kuwa Sh milioni 75 kwani alikuwa akilipwa Dola za Marekani 12,500 na anatakiwa kulipwa mishahara ya miezi mitatu kwa mujibu wa mkataba aliosaini na TFF.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment