Hali hiyo inazilazimisha mamlaka za kiusalama
katika mataifa nazo kuumiza vichwa ili kutafuta mbinu za kung’amua, kukamata na
kudhibiti usafirishwaji wa dawa za kulevya ambao hunufaisha matajiri wachache,
huku kundi kubwa la wananchi hasa vijana likiteketea.
Tanzania ni moja ya mataifa ambayo
yanapambana na uingizaji, usafirishwaji na utumuaji dawa za kulevya kupitia
Kikosi Maalumu cha Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya, chini ya Jeshi la
Polisi katika Wizara ya Mambo ya Ndani.
Katika mahojiano na gazeti hili, mkuu wa kikosi
hicho, Godfrey Nzowa anaeleza kuwa ingawa waingizaji na wasafirishaji wa dawa
za kulevya wamekuwa mstari wa mbele katika kubuni mbinu mpya ili kuhakikisha
wanafanikisha uingizaji dawa za kulevya nchini kikosi chake hakitarudi nyuma
kupambana na uhalifu huo akiongeza kwamba wamebaini mbinu zote za wahalifu hao.
Anasema, awali, ilizoeleka watu hao kutumia
njia kadhaa ikiwamo kumeza kete au kuhifadhi kwenye mabegi ya nguo, lakini sasa
njia hizo hutumika mara chache, badala yake wamebuni mbinu nyingine.
Anataja baadhi ya mbinu hizo ‘mpya’ kuwa ni
pamoja na kutumia simu za mkononi na ‘chaja’ zake kuhifadhia dawa, hivyo kuwa
vigumu kuwabaini.
“Wanazifungua simu na kutoa mashine za ndani
kisha kupakia dawa za kulevya, mtu wa kawaida akaziona ni simu na ni vigumu
kujua ndani kumewekwa nini,” anasema Kamanda Nzowa na kuongeza:
“Pia huchukua betri za simu na kuziharibu
kisha kujaza dawa hizo kwenye ujazo sawa na betri kisha kuzifunga upya kama
betri halisi, mbinu hizo tumezibaini.”
Nzowa anataja mbinu nyingine walizobaini:
“Wengine wanachukua viazi mbatata bandia na kuweka dawa za kulevya, kisha
huzichanganya na viazi halisi.”
Mbinu nyingine ni dawa hizo kuchanganywa na
gundi ya maji. Gundi hiyo ikisafirishwa salama hadi eneo husika basi
hufunguliwa na kutenganishwa na dawa hizo.
“Siyo hizo tu, wanatumia hata marumaru za
kusakafia kusafirisha dawa za kulevya. Dawa hizo zinawekwa katikati ya vigae
vilivyopangwa kitaalamu. Mara nyingi mizigo yao huisafirisha kupitia njia ya
maji (bahari) kwa sababu huko ndiko mizigo hubebwa kwa wingi tofauti na njia ya
anga. Hawa jamaa hawana tofauti na wale wanaosafirisha bangi kutoka Arusha kuja
Dar es Salaam, juu yake wanaweka kabeji huku chini wakiweka dawa hizo.Mtu
mwingine anaagiza magari kadhaa, lakini kati ya magari hayo, moja anahifadhi
dawa hizo katika sehemu ya ‘waterpump’ (pampu ya maji ya gari husika) au ‘power
window’ za bandia ambazo zikifika hung’olewa na kubakia zile halisi.”
Anafafanua kuwa licha ya wasafirishaji
kutumia mbinu hizo, kikosi chake kipo imara kupambana na suala hilo, ndiyo
maana katika kipindi cha kuanzia Mei mwaka jana, hadi Mei mwaka huu,
wamefanikiwa kuwakamatawa watuhumiwa 44.
0 comments:
Post a Comment