Image
Image

Michezo, sanaa si ajenda za wanaotaka urais.


Taifa liko kwenye kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ambao utalipatia Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, wabunge na madiwani watakaoongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Tayari mchakato wa kuelekea uchaguzi huo umeshaanza kwa vyama vya CCM, CUF, na NCCR-Mageuzi, ambapo vyama vya CCM na CUF vikiwa hatua ya juu ya kupata wagombea urais.
Kwa takriban wiki mbili, tumekuwa tukisikia jinsi watiania wa CCM walivyokuwa wakitangaza vipaumbele vyao iwapo watapitishwa na chama hicho kuwania urais. Makada hao wameeleza mambo mengi makubwa, ambayo kwa namna fulani, ni yale yale yanayoimbwa na wanasiasa bila ya kufanyiwa kazi, ingawa baadhi wamekosolewa kuwa hawawezi kutangaza mikakati kabla ya chama chao kutoa ilani.
Pamoja na kwamba mikakati hiyo huwa vigumu kutekelezeka, lakini kilicho kizuri ni kwamba angalau wametaja kwamba watashughulikia kuboresha kilimo, kukusanya mapato, kudhibiti matumizi, kupambana na rushwa na ufisadi, kuchochea ubunifu, kulinda viwanda vya ndani na kuboresha miundombinu ya usafiri, maji, nishati na huduma nyingine.
Lakini kilicho dhahiri ni kwamba makada wote hawajaonyesha ni jinsi gani watashughulikia kukuza michezo na kuweka mazingira mazuri ya sanaa kukua na hivyo kuongeza wigo wa ajira kwa vijana.
Wale waliotaja michezo na sanaa wamezungumzia kwa ujumla tu kuwa watahakikisha michezo na burudani inaendelezwa na kuwa ajira kwa vijana, lakini hakuna aliyechukulia suala la michezo kama moja ya ajenda zake kuu, akichanganua matatizo yaliyopo sasa na jinsi atakavyoyatatua na mikakati mipya ya kuhakikisha michezo na burudani inaendelea na kuwa sehemu ya vyanzo vikuu vya ajira.
Hadi sasa nchi imesimamia kwenye Sera ya Michezo ya mwaka 1995 ambayo kwa hali ilivyo sasa imepitwa sana na wakati, hasa kutokana na vyama vya kimataifa vya michezo kutoa miongozo mipya kwa wanachama wake ambayo inaenda tofauti na miongozo na sheria za nchi.
Sera ya kwanza ya utamaduni ilitoka mwaka 1997, yaani miaka miwili baada ya Sera ya Michezo. Sera hizo zote hazichukulii michezo na utamaduni kama ajira, bali kama mambo ya starehe, kuburudisha, kujenga afya na kuunganisha watu.
Kwa maana hiyo, kuendeleza mambo ambayo ni ya kuburudisha, kujenga afya na kuunganisha watu, inaonekana kuwa ni kitu kinachoweza kujiendesha na kinachofanywa na viongozi wa Serikali ni kuhakikisha kunakuwapo na fedha za kutosha kwa ajili ya michezo ya taasisi za Serikali, mashirika ya umma na shule za msingi na sekondari kwa kuwa mashindano hayo hayahusishi vijana ambao wanaona michezo na burudani ni sehemu ya vyanzo vya ajira.
Tulitarajia kusikia makada hawa wakizungumzia ni jinsi gani watahakikisha vifaa vya michezo kwa ajili ya watoto vinapatikana kwa bei ambayo mwananchi wa kawaida anaweza kuimudu, vifaa vya kufundishia walimu wa michezo kwa watoto vinapatikana kwa bei nzuri, jinsi gani viwanja kwa ajili ya watoto kucheza vinalindwa na ni kwa jinsi gani inatoa unafuu katika ujenzi wa viwanja vya mashindano kwa taasisi zilizo tayari kufanya hivyo.
Tulitarajia kusikia wanazungumzia ni kwa jinsi gani watabadilisha sera za utamaduni na michezo, ili ziendane na hali halisi ya mabadiliko ya uendeshaji michezo na burudani.
Michezo na sanaa ni mambo ambayo hayaepukiki katika dunia ya leo, kwa hivyo ni vizuri ikawa sehemu za ajenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment