Mzimu wa Nyerere wawatesa wagombea urais.
Jina la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere limeibuka ghafla na kwa nguvu baada ya makada wanaowania kupitishwa na CCM kuanza kutangaza nia, huku wengi wao wakionyesha kuaminiwa na muasisi huyo wa Taifa na wengine kuahidi kufuata miiko aliyoiweka wakati alipoongoza Serikali ya Awamu ya Kwanza. Makada hao pia wamezuru kaburi la Baba wa Taifa na wengine kutumia kuaminiwa kwake na wananchi wakati akiwa na umri mdogo ili kujenga hoja kuwa uzoefu na umri si suala la kuzingatiwa katika kupata kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwalimu Nyerere, aliyeongoza Tanganyika tangu mwaka 1961 na baadaye Tanzania kuanzia mwaka 1964 hadi 1985 alipong’atuka, anajulikana sana kutokana na kuanzisha Azimio la Arusha mwaka 1967 lililoweka miiko ya uongozi bora na kuweka misingi ya siasa za ujamaa, mambo ambayo yalitenguliwa na Azimio la Zanzibar miaka michache baada ya kuachia urais.
Mbali na kutangaza miiko hiyo iliyojenga maadili ya uongozi wakati nchi ikielekea kujenga Taifa la kijamaa, Mwalimu Nyerere alikuwa na nguvu ya ushawishi na mkali dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi, jambo lililomfanya aheshimike ndani na nje ya nchi.
Wakati Taifa likisikiliza hoja za wanaotia nia ya kuwania urais ikiwa ni miezi michache baada ya Bunge la Katiba kuondoa mambo ya maadili kwenye Rasimu ya Katiba, suala hilo linaonekana kurudi kwa nguvu kwenye sera za wagombea uongozi ambao wanataja kila mara jina la Nyerere, miaka 16 baada ya kifo chake.
“Wanamtumia Nyerere kwa sababu wanajua alikuwa muadilifu, alikuwa akisema kitu watu wanatekeleza. Leo kiongozi anatoa maagizo hakuna anayetekeleza,” alisema mchungaji wa Kanisa la Pentekoste, Dk Damas Mukasa alipoulizwa maoni yake kuhusu kuibuka kwa jina hilo la muasisi wa Tanganyika.
Akitangaza rasmi nia ya kuutaka urais kwenye hafla iliyofanyika uwanja wa ofisi ya CCM ya Mkoa wa Lindi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema kuwa anatosha kushika wadhifa huo na kwamba Mwalimu Nyerere atafurahi huko aliko iwapo atachaguliwa kuwa Rais kwa miaka 10 ijayo.
Pia, Membe alisema kuwa Machi mwaka huu alikwenda Butiama na kuzuru kaburi la Mwalimu Nyerere ambako alipiga magoti na kumweleza nia yake ya kuutaka urais.
“Nilipiga goti nikamwambia Mwalimu, navitaka viatu vyako, alivivaa Mzee (Ali Hassan) Mwinyi, Mzee (Benjamin) Mkapa na (Rais, Jakaya) Kikwete. Sasa nataka kuvivaa mimi na nina hakika vinanitosha,” alisema Membe.
“Ninaamini vitanitosha. Nikamwambia chondechonde, kama havitanitosha, niambie… timu yangu ya mikoani ikawahi kuniambia unatosha.”
Mkurugenzi mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Hassy Kitine naye alitumia jina hilo wakati akitangaza nia ya kutaka kurejea Ikulu ambako alifanya kazi chini ya utawala wa muasisi huyo, akiahidi kutumia miaka mitano kuirudisha Tanzania ya Mwalimu Nyerere.
Dk Kitine alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake aliyoitoa mjini Dodoma kutoa mifano ya utendaji wa Mwalimu Nyerere na kuwaponda wengine waliojitokeza kuwa hawana sifa za kumfikia.
0 comments:
Post a Comment