Image
Image

Nani adui wa umoja wetu wa kitaifa?.

Hakuna taifa linaloweza kusimama bila ya kuwa na umoja wa kitaifa.Tanzania imesimama imara hadi leo hii kwasababu ya umoja wa kitaifa uliojengwa na waasisi wa taifa letu.
Tunasifiwa kwa utulivu na amani. Sifa hizi ni za kweli na kilichotukifisha hapa tulipo ni umoja.Na hili halikunyesha tu kama mvua ni jambo lilofanyiwa kazi usiku na mchana. Waasisi wa Taifa letu walijitahidi kuujenga umoja.
Kuna mambo mengi yaliyowasaidia kuujenga umoja huu: tulikuwa na chama kimoja cha siasa.Chama kilitunga sera na kutoa dira. Hivyo chama kilikuwa ni chombo kimojawapo cha kuujenga umoja wa taifa letu.Ingawa kulikuwa na watu wachache walioupinga mfumo wa chama kimoja, hawakuwa tishio la kuuvunja umoja wetu. Walikuwa wapinzani wenye kulenga kujenga umoja wa kitaifa.
Ukabila ulipigwa vita na utawala wa machifu ulifutiliwa mbali.Lugha ya Kiswahili ilipewa kipaumbele na kuwa chombo cha kuwaunganisha Watanzania wote. Nchi ambazo zinatumia lugha za kigeni kama lugha zao za kitaifa, hadi leo zinapata shida ya kujenga umoja wa kitaifa.
Jeshi la kujenga taifa lilianzishwa kwa lengo la kuwakutanisha vijana waliomaliza kidato cha sita na vyuo wa Tanzania nzima.Kipindi chote cha mafunzo ya vijana hawa uzalendo na umoja wa kitaifa ni mambo yaliyosisitizwa.
Mfumo wa elimu wa kuwasambaza vijana kwenye shule mbali mbali za mikoa ya Tanzania, ulisaidia kuwakutanisha vijana na kujenga umoja wa kitaifa. Vijana kutoka Kagera, walipelekwa kusoma Mtwara,Moshi au Dar-es-salaam. Wa Kigoma, walipelekwa Arusha, Kagera, Musoma au Dodoma.
Mwaka 1995, Tanzania, ilijiingiza katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.Tunayoyashuhudia sasa hivi hakuna chama kinachoonyesha sera ya kujenga umoja wa kitaifa. Wapinzani wa leo ni tofauti kabisa na wapinzani wa zamani wakati wa utawala wa chama kimoja.
Wapinzani wa leo pamoja na chama tawala cha CCM, wanaangalia zaidi umoja wa vyama vyao kuliko umoja wa kitaifa, wanatanguliza kuingia Ikulu, ruzuku, mbwembwe za madaraka na ushindani wa chuki na utengano.
Baadhi ya vigogo wa CCM, wanasema ni lazima kitangulizwe chama. Wakati tunalilia umoja wa kitaifa, wao wanalilia umoja wa chama chao. Hivyo kwao jambo la muhimu na kutanguliza ni chama chao!
Mfumo wa elimu umevurugika, shule nyingi za binafsi na sekondari za kata zimeanzishwa na kuchochea watoto wengi wasiweze kuivuka mikoa yao. Watoto wa matajiri hawasomi tena na watoto wa masikini.Kiwango cha elimu kimeanza kutofautiana na kuleta hatari ya kuaanza kuunda tabaka katika taifa letu.
Mfumo uliokuwa umejengwa na waasisi wetu wa kuunda umoja wa kitaifa umeaanza kupotea! Ni wajibu wa kila Mtanzania kujiiuliza: Ni nani adui wa umoja wetu? Kama nilivyosema hapo juu, ni vigumu taifa lolote kusimama bila ya umoja. Kama tunataka Taifa letu liendelee kusimama ni lazima tukazane kujenga umoja.
Hivi sasa kila tunapoingia kwenye mchakato wa uchaguzi Mkuu, Waislamu wanamtaka rais Mwislamu na Wakristu wanamtaka rais Mkristu. Maoni haya yanafunika hekima na busara yote. Si uwezo wa mtu na wala si mapenzi ya mtu katika Taifa lake. Jambo muhimu ni dini!.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment