Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA), Dkt. Agnes Kijazi (mwenye suti nyeusi) akiongoza ujumbe wa Tanzania
kwenye Mkutano Mkuu wa 17 wa Shririka la Hali ya Hewa Duniani unaofanyika Mjini
Geneva, Uswisi. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa
katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Celestine Mushy (Kulia)
Tanzania yachaguliwa kuwa mjumbe katika baraza la utendaji (executive
council) la shirika la hali ya hewa duniani–world meteorological organization
(wmo).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes
Kijazi, amechaguliwa kuwa Mjumbe katika Baraza la Utendaji (Executive Council)
la Shirika la Hali ya Hewa Duniani–World Meteorological Organization (WMO) kwa
kipindi cha miaka minne kuanzia 2015 hadi 2019. Dr. Kijazi amechaguliwa tarehe
4 June 2015 wakati wa Mkutano Mkuu wa Kumi na Saba wa Shirika la Hali ya Hewa
Duniani (WMO-Congress wa 17) ulioanza tarehe 25 Mei 2015 na unatarajiwa
kumalizika tarehe 12 Juni, 2015 Jijini Geneva, Uswisi.
Kuchaguliwa kwa Dr. Agnes Kijazi kumetokana na jitihada zilizofanywa na
Ubalozi wetu wa Kudumu Umoja wa Mataifa wa Geneva na Idara ya Ushirikiano wa
Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambazo kwa
pamoja zilisimamia zoezi la kuomba kura kutoka kwa wanachama na kampeni wakati
wa uchaguzi.
Dr. Kijazi ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania katika ushiriki Mkutano
huo ambao una washiriki kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Maji na Ubalozi wa Tanzania
Nchini Uswisi.
WMO ni Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya hali ya
hewa duniani na mabadiliko ya tabianchi. WMO inatekeleza majukumu na maamuzi
kuhusu maendeleo ya sayansi ya hali ya hewa na uboreshaji wake ikiwa ni pamoja
na kusimamia viwango katika upimaji na utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa
nchi wanachama.
Hadi wakati wa Mkutano huu huko nchini Uswisi, WMO ilikuwa na nchi
wanachama 191. Katika Mkutano huu nchi za Sudan Kusini na Tuvalu zilikaribishwa
rasmi kama wanachama wapya wa WMO. Kati ya nchi hizi 191 ni nchi 37 tu ambazo
zina wajumbe katika Baraza hilo kuu. Hivyo hii ni nafasi adhimu na heshima kwa
Tanzania, TMA na Dr Kijazi ambaye ni msomi mwenye utaalamu wa kutosha akiwa na
Shahada ya Uzamivu (Ph.D) katika Sayansi ya Hali ya hewa.
Kazi kuu ya Baraza la Utendaji la WMO, ambalo Tanzania imefanikiwa kuwa
mjumbe ni kuchukua hatua zinazostahili, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa
Shirika hilo kutekeleza maamuzi yanayotolewa na Mkutano Mkuu (WMO-Congress)
ambao hukutana mara moja kila baada ya miaka minne.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo Balozi Celestine Mushy, Mkurugenzi wa
Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alielezea sababu ya Tanzania kugombea nafasi
hiyo muhimu kuwa ni pamoja na kuwa ndani ya chombo cha maamuzi na hivyo
kushawishi maamuzi yatakayoinufaisha jamii nzima ya kimataifa ikiwemo Tanzania
katika masuala ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kutoa mwelekeo wa kisayansi
katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea katika
maeneo mengi Duniani.
Kwa upande wake, Dkt. Kijazi alieleza kuridhishwa kwake na jinsi
ambavyo nchi wanachama 190 walivyoridhishwa na utendaji wa Tanzania katika
kipindi cha miaka mitatu (2012-2015) ambacho alikuwa mjumbe wa Baraza hili na
hivyo kumchagua tena katika kipindi kingine cha miaka minne. “Hii ni heshima
kubwa kwa nchi yangu ya Tanzania na ninaahidi kutumia uwezo wangu wote
kutekeleza majukumu ya nafasi hii” alisema Dkt. Kijazi.
0 comments:
Post a Comment