Image
Image

JK Aongoza mamia ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine katika mazishi ya Mufti wa Tanzania,Shekh Mkuu, Issa Bin Shaaban Simba.


Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza mamia ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine katika mazishi ya Mufti wa Tanzania, Shekh Mkuu, Issa Bin Shaaban Simba yaliyofanyika kwenye makaburi ya Nguzonane mkoani hapa. Mufti Simba alifariki dunia juzi katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam baada ya kuugua kisukari na shinikizo la damu.
Mwili wa Sheikh Simba uliwasili jana kwenye Uwanja wa Ndege Shinyanga na kupokewa na mamia ya wananchi na uliongozwa na msafara wa magari ya polisi hadi nyumbani kwake, Majengo.

Baada ya mwili huo kuwasili nyumbani kwake saa 8.30 mchana, vilio vilisikika kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki huku viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), wakifanya kazi kubwa kuwatuliza.
Wagombea urais  wagongana
Baada mwili wa Shekh Simba kufikishwa nyumbani kwake wagombea urais kupitia CCM ambao waliwahi kuwa Mawaziri wakuu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa walikutana na kusalimiana kwenye msiba huo na kisha wote kuketi pamoja. Lowassa ndiye aliyetangulia kufika msibani saa tisa alasiri na Sumaye aliwasili nusu saa baadaye.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye pia ni mmoja wa wagombea wa CCM, aliwasili kwenye mazishi hayo wakati waombolezaji wakiwa makaburini. Mazishi ya Shekh Simba yalifanyika saa 11 jioni.
Bilal aongoza  waombolezaji  Dar
Wakati shughuli za mazishi zikiendelea Shinyanga, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal aliwaongoza viongozi mbalimbali wa Serikali, wanasiasa, mabalozi na viongozi wa dini katika ibada mahsusi kwa ajili ya msiba huo iliyofanyika kwenye Makao Makuu ya Bakwata, Kinondoni, Dar es Salaam na kuwataka Watanzania kudumisha amani, upendo na mshikamano akisema hiyo ndiyo njia sahihi ya kuendeleza mazuri yaliyofanywa na Mufti
Baadhi ya viongozi waliohudhuria ibada hiyo ni Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa, Waziri Mkuu mstaafu, Salim Ahmed Salim, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed.
Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile, Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu, mabalozi wa Sudan, Comoro, Iran na Sudan nchini na Mwenyekiti wa Kampuni ya IPP, Reginald Mengi.
Akizungumza katika ibada hiyo, Dk Bilal alisema; “Tumempoteza kiongozi muhimu ambaye alikuwa dira na alijenga maelewano mazuri sana kati ya viongozi wa dini na viongozi wa Serikali.”
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment