Q-Chillah anatamani kufuata nyayo za mchezaji Mbwana Samatta.
ABUBAKARI Katwila ‘Q- Chillah’, ni miongoni mwa wasanii wanaofanya vizuri katika muziki kwa takribani miaka 10 na kuuweka sehemu nzuri.
Q-Chillah ni mkongwe ambaye alikuwa ni mfano wa kuigwa katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini kutokana na juhudi zake katika tasnia hiyo ikiwa ni pamoja na kujua nini anakifanya katika tasnia hiyo.
Mkongwe huyo ambaye alishawahi kutamba na nyimbo mbalimbali zilizomtambulisha vizuri katika tasnia hiyo ikiwa ni pamoja na Ulinizaa wewe ukanikataa, ‘Uhali gani’, ‘Kama yule’, anabainisha kuwa muziki wa sasa ni tofauti na muziki wa miaka 10 iliyopita.
Anasema muziki uliopo sasa ni mzuri na ni bora kutokana na kuonesha ushindani katika nchi nyingine na kwamba anawapongeza wasanii Naseeb Abdul ‘Diamond’ na Ambwene Yesaya ‘AY’.
“Napongeza juhudi za baadhi ya wasanii ambao wameutoa muziki tulipouacha na kuufikisha kimataifa, sasa nimeamua kurudi tena katika tasnia hii nikiamini siwezi kuwaangusha wasanii walipofikia, nitaendelea kuupeleka mbele zaidi,” anasema.
Anasema uwezekano wa kuufikisha muziki mbali zaidi ya hapa ulipo upo kinachotakiwa ni wasanii kujipanga na kuhakikisha wanapata wasimamizi wazuri wa kazi zao ambao wanaweza kuwasaidia katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwatangaza kimataifa.
Q-Chillah anasema msanii yoyote ili aweze kufanikiwa na kutimiza ndoto zake ni lazima awe na usimamizi mzuri ndio aweze kufanikiwa.
“Wasanii wengi hapa kwetu wanashindwa kufika mbali kutokana na kushindwa kuamini uongozi walionao na kuamua kujisimamia wao wenyewe kitu ambacho hakiwezekani,” anasema Q Chillah.
Anasema alipotea katika tasnia hiyo kutokana na kutokuwa na msimamizi kitu ambacho ni changamoto kubwa kwake iliyokuwa ikimuandama.
Ananshkuru Mungu kwani ameingia mkataba na Kampuni ya QS na kuweka wazi malengo yake ya sasa.
“Mwaka huu nataka uwe mwaka wa kazi, hivyo sihitaji tena malumbano na watu zaidi ya kupiga kazi za juu,” anasema Chillah huku akitabasamu.
“Mwaka huu nitahakikisha napambana na changamoyo zote zilizokwamisha maendeleo yangu, lengo ni kurudisha hadi yangu kwa nchi za Nigeria, Kenya, Rwanda na nchi nyingine nyingi zilizoendelea kimuziki,” anasema.
Q-Chillah anafafanua hilo kwa kutolea mfano wa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa TP Mazembe, kwa kusema ni miongoni mwa Watanzania ambao wanajua nini wanafanya kimataifa kutokana na kipaji alichonazo.
Anasema kama Samatta asingekuwa anafikiria mbali asingeweza kuondoka Simba na kuweza kujiunga na timu hiyo tajiri lakini amefanya hivyo ili aweze kuonesha kipaji chake katika mataifa mbalimbali.
Q-Chillah anasema anatamani kufuata nyayo za mchezaji huyo ili naye aweze kufikisha kipaji chake katika nchi mbalimbali nje ya Tanzania.
“Kupitia mkataba nilioupata sipo tayari kupoteza muda namuomba mwenyezi mungu aweze kunijaza ujasiri niweze kukitumia vizuri kipaji nilichonacho kuutoa muziki ulipo na kuufikisha sehemu nyingine.
Kwa sasa msanii huyo ameachia ngoma yake mpya iitwayo ‘For You’, anasema ana uhakika wa kufanikiwa zaidi kwa ngoma yake hiyo, kwani imetumia gharama kubwa.
“Kwa sasa ana mtazamo wa kuja kivingine kabisa, nashukuru kwa kupata kampuni inayosimamia kazi zangu,” anasema.
Nyota huyo ameaachia ngoma hiyo akiwa amemshirikisha msanii MB Dogy ambaye pia ni msanii wa muda mrefu katika muziki wa kizazi kipya.
Mbali ya wimbo huo, pia kwa sasa Chillah anatamba kwa video yake mpya iitwayo Mdogo mdogo iliyoongozwa na Adam Juma.
Anasema ataendelea kuthamini mchango wa mkongwe mwezake, Profesa Jay kutokana na kuwa katika fani hiyo kwa muda mrefu na anaendelea kufanya vizuri.
“Profesa Jay ni zaidi ya Legend (gwiji) hapa Tanzania maana anafanya vitu vizuri katika muziki kiasi kwamba hata wasanii ambao walianza muziki kabla yake wanatamani kuvifanya siku zote.”
Mbali na gwiji huyo, Chillah pia anavutiwa na kipaji alichonacho Ali Kiba kwani ni miongoni mwa wasanii wenye sauti nzuri.
Chillah pia muda mwingi akiwa hana kazi za kufanya anautumia katika kufanya sala na kusoma kurani.
0 comments:
Post a Comment