Image
Image

Utoro bungeni haufai ukemewe na usifumbiwe macho.

HIVI karibuni tumeshuhudia hekaheka za mchakato wa uchukuaji wa fomu za kuwania kugombea urais zikishika kasi pamoja na jitihada za kusaka wadhamini mikoani zikiendelea.Ni dhahiri kuwa mchakato huu umeamsha hamasa sana sio tu kwa wanasiasa bali hata kwa jamii nzima ya watanzania na hata ya kimataifa. Kutokana na unyeti wake, tumeshuhudia mwaka huu kuwepo wa ushabiki mkubwa wa kisiasa kiasi kwamba umeweza kuathiri hata shughuli mbalimbali za kiserikali na hata za kijamii.
Mojawapo wa sehemu iliyoathirika zaidi na mchakato huu wa hekeheka na homa ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kumekuwepo na mahudhurio duni ya wabunge wakiwemo mawaziri ambao ndio wadau wakubwa katika kusimamia na kujibu hoja za Serikali katika kuboresha utendaji kazi wa idara na taasisi wanazozisimamia. Jambo hili la wabunge kukimbia ukumbi wa bunge na kwenda kujiunga na wasaka urais sio la kizalendo kwani wananchi waliwatuma waende wakawatetea na kuwasilisha hoja zao ili zishughulikiwe.
Lakini jambo hilo la kuwatetea wananchi kwa kipindi hiki limekuwa gumu kwao kwa kutelekeza ukumbi wa bunge huku wakimuacha spika na baadhi tu ya wabunge wachache kuendeleza mijadala. Hali iliyopo bungeni kwa wakati huu inatia aibu kubwa kwa taasisi hii nyeti na muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu.
Mahudhurio haya duni hivi karibuni yalimlazimu spika wa bunge Anne Mkinda kuviagiza vyama vya siasa nchini vyenye wawakilishi bungeni hapo kuhakikisha kuwa vinawarejesha wabunge wao ndani ya ukumbi wa bunge ili kuendelea na mijadala iliyosalia kabla ya mwisho wa kusitisha bunge hilo haujawadia.
Licha ya harakati hizi za kusaka kuingia Ikulu kuathiri shughuli za bunge, pia zimesambaratisha na kuzifunga baadhi ya ofisi za serikali na taasisi kutokana na wahusika kukimbilia kwenye kampeni za wafuasi wao wanaowaunga mkono.
Kitendo hiki cha watumishi wa umama kuzikimbia ofisi zao na kuziacha bila ya huduma kama vile wenyeviti wa halmashauri ni kinyume cha sheria kwani wanawakoseha wananchi huduma wanaokuja kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao.
Maendeleo ya taifa hili yanahitaji utendaji kazi wa pamoja usiokuwa na mashaka lakini kwa kitendo cha wabunge na baadhi ya watumishi kuzikimbia ofisi zao na kutelekeza majukumu yao na kukimbilia kampeni kwa kuunga mkono wasaka urais sio cha kizalendo.
Kila mtu nanapaswa kukemea tabia hii kwa kuhakikisha anamuuliza mbunge wake, ni kipi kilichokuleta huku jimboni kwa muda huu wakati bunge linaendelea na sisi tulikutuma uende ukakae bungeni utuwakilishe?
Kwa kufanya hivyo huenda wabunge wetu wataona aibu na kurejea bungeni kuendelea na shughuli za kujadili na kupitisha miswada mbalimbali yenye tija katika maendeleo ya taifa letu.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment