Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia
Hanspoppe,aliiambia NIPASHE jana kwamba atakwea 'pipa' kesho kuelekea
Brazil kwa ajili ya kusaka nyota wapya.
Simba hadi sasa ina wachezaji wawili tu wa kigeni, Mganda Emmanuel
Okwi na beki Juuko Murshid na imedhamiria kujaza nafasi zote saba, kama
zinavyoruhusu kanuni mpya za ligi hiyo kuhusu wachezaji wa kigeni.
Wakati dili la kumsajili mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo, likionekana
kuota mbawa, Simba tayari imeshaachana na nyota wake wa kimataifa,
Danny Sserunkuma, Simon Sserunkuma na Joseph Owino huku Paul Kiongera
akirejea Kenya kutokana na kutopona goti lake.
Hanspope alisema mbali na yeye kwenda Brazil, lakini pia wanapanga
kutuma 'majeshi' Zimbabwe, Burundi na Uganda kwa ajili ya kusaka nyota
zaidi wa kujaza idadi ya wachezaji saba wa kigeni.
Aidha, Hanspoppe alisema kwa sasa hawezi kuthibitisha taarifa
kwamba wanakaribia kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Hamis
Kiiza 'Diego'.
Akizungumzia suala la kiungo, Ramadhan Singano 'Messi', alisema
bado wanamtambua ni mchezaji wao halali hadi mwakani na kwamba tayari
wameshamlipia pango la nyumba ambalo mkataba uliisha na taarifa
kuchelewa kuwafika, lakini sasa kila kitu kiko sawa.
Kuhusu uvumi kwamba Singano anakwenda Azam, alisema analisikia tu, lakini halijafika mezani kwake.
MZUNGU MWINGINE
Wakati kocha mkuu wa Simba Muingereza, Dylan Kerr, anatarajiwa
kutangaza mikakati yake ya kiufundi ndani ya klabu hiyo kesho, uongozi
wa klabu hiyo umesema kuwa leo utampokea kocha mpya wa viungo wa timu
hiyo ambaye ni raia wa Serbia, Dusan Momcilovic.
Akizungumza na gazeti hili jana, Rais wa Simba, Evans Aveva,
alisema kuwa kocha huyo wa viungo tayari ameshaingia mkataba mfupi wa
mwaka mmoja na klabu hiyo na ajira yake itaanza sambamba kocha mkuu.
Aveva alisema kwamba ujio wa kocha huyo wa viungo utasaidia
kuimarisha kikosi cha timu yao ambacho kinajiandaa na msimu mpya wa Ligi
Kuu ya Soka Tanzania Bara.
"Kocha wa viungo ataingia nchini kesho (leo) na mkataba wake
unatarajia kuwa mfupi, awali tulitarajia kumpa mkataba wa mwaka mmoja,
lakini inaweza kufikia mitatu kutokana na mahitaji yatakavyokuwa,"
alisema kiongozi mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Aliongeza kwamba Mserbia ana uzoefu mkubwa katika fani ya mpira wa miguu hususan mazoezi ya viungo.
Alitaja sehemu nyingine ambazo kocha huyo wa viungo amefanya kazi
ni pamoja na Malaysia, Indonesia, Bosnia & Herzegovina, Oman na
Georgia, ambako alikuwa kocha wa mazoezi ya viungo wa klabu ya FC
Dinamo, iliyocheza mechi za awali za Ligi ya mabingwa Ulaya.
Kocha huyo pia amewahi kufanya kazi Afrika katika klabu ya FC SOGOR–Tobruk ya Libya na ana Digrii ya Mazoezi ya Viungo.
"Klabu ya Simba ina furaha kubwa kuingia mkataba na kocha Dusan
Momcilovic mwenye uzoefu na weledi wa kutosha, tunaamini atakuwa chachu
ya mafanikio pia katika kunoa vipaji vya wachezaji wa Simba," alimaliza
Aveva.
Ujio wa kocha huyo unafanya idadi ya makocha wa kigeni ndani ya
Simba kufikia watatu baada ya kocha wa makipa Mkenya, Abdul Iddi Salim
na Kerr.
Simba ambayo ilishaanza mazoezi ya viungo chini ya kocha msaidizi,
Selemani Matola, inatarajia kuingia kambini siku yoyote huku pia
viongozi wakikamilisha mipango ya kwenda kuweka kambi Shelisheli.
0 comments:
Post a Comment