Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum ndiye aliyetangaza uamuzi huo
wakati akihitimisha hotuba ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha
2015/2015. Aidha, alitangaza pia kuanza kwa mchakato wa kuhakikisha kuwa
wazee wote nchini wanaanza kulipwa katika mwaka huo wa fedha unaoanza
Julai Mosi.
Hakika, hizi ni habari njema kwa umma mpana wa Watanzania..
Tunapongeza uamuzi huu ambao tunaamini kuwa kwa kiasi kikubwa utapunguza
machungu waliyokuwa wakikumbana nayo wastaafu kwa kipindi kirefu sasa.
Kuanza kwa mchakato wa kuwaandalia malipo ya kila mwezi wazee wote
nchini ni taarifa nyingine tunayoamini kuwa itawafariji wengi, tena bila
kujali rika.
Tambarare Halisi tunalazimika kuipongeza serikali kwa uamuzi wake huu
kutokana na sababu nyingi, kubwa zaidi ikiwa ni changamoto wanazokumbana
nazo wazee nchini. Na kwa kuzingatia kwamba awali serikali ilitoa
pendekezo la kutaka wazee wa kima cha chini waongezewe malipo yao hadi
kufikia Sh. 85,000 kwa mwezi, ni wazi kwamba tangazo la juzi la Waziri
wa Fedha limezingatia rai ya wabunge waliopaza sauti zao kutaka kiwango
hicho kiwe walau Sh. 100,000 au zaidi.
Kama tulivyogusia, msingi wa pongezi hizi uko wazi. Kwamba, hivi
sasa wastaafu na wazee wengine nchini wamekuwa wakikabiliwa na
changamoto nyingi za kimaisha. Wengi wao wamekuwa wakiishi maisha
magumu, hasa kutokana na ukali wa maisha unaoongezewa pia na kasi ya
mfumuko wa bei, kuporomoka kwa thamani ya shilingi na pia maradhi ya
mara kwa mara yanayowaandama watu wa umri wao na hivyo wengi wao
kujikuta wakilazimika kutumia rasilimali chache walizo nazo kwa ajili ya
matibabu.
Sisi tunajua kuwa kiwango hiki ni kidogo kulingana na changamoto
hizi tele walizo nazo wastaafu na wazee. Hata hivyo, tunalazimika
kupongeza hatua hii kwa kuamini kuwa huu ni mwanzo tu wa kuendelea
kuboresha zaidi malipo ya kundi hili la Watanzania.
Jambo pekee tunalodhani kwamba linapaswa kukumbukwa wakati wote ni
kuhakikisha kwamba dhamira hii nzuri ya serikali inatekelezwa mara moja
kuanzia Julai Mosi. Kwamba, kama ilivyoahidiwa na Waziri wa Fedha, kamwe
kusiwe na kigugumizi cha kutekeleza jambo hili muhimu, na ambalo kwa
kiasi kikubwa litasaidia kuonyesha kuwa kweli tunawaenzi wastaafu na
wazee wetu hawa, ambao tunaamini kuwa wakati wote wa ujana wao
walijitolea kila hali katika kulijenga taifa hili.
Kwa kuanzia, ni vyema serikali ikahakikisha kuwa inafanyia kazi
taarifa zilizotolewa na waziri bungeni kuhusiana na takwimu za wazee
wote nchini. Kwa mujibu wa ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka
2012, taifa lina wazee milioni 1.2. Ni kweli kwamba katika kipindi hiki
cha miaka mitatu, idadi hiyo itakuwa imebadilika kwa kiasi kikubwa kwani
wapo Watanzania wengine wengi waliofikisha umri wa wazee na pia wapo
waliofariki dunia. Tunadhani kwamba ni vizuri mchakato huo wa kujua
idadi halisi ya wazee waliopo sasa ikafanyika haraka kwa kuzishirikisha
mamlaka za serikali za mitaa ili mwishowe ulipwaji wa pensheni kwao
uanze mapema, kama itakavyokuwa kwa wastaafu.
Tunasisitiza hili kutokana na imani yetu kuwa kitendo chochote cha
kuchelewa kuwalipa wazee hawa, maana yake ni kwamba matumaini makubwa
waliyoyapata kupitia tangazo la waziri yatayeyuka na mwishowe
kuwasononesha kwa kiasi kikubwa. Haitakuwa jambo zuri hata kidogo kuona
kuwa wazee waliotumikia taifa kupitia sekta mbalimbali zisizokuwa za
serikali na za umma wakikosa pensheni hii iliyoahidiwa na waziri jana.
Kadhalika, tunakumbushia hili kutokana na ukweli kuwa yapo maamuzi
kadhaa mazuri yanayofanywa na serikali lakini utekelezaji wake unakuwa
wa shida, mojawapo ikiwa ni uamuzi wa serikali wa kutoa huduma za
matibabu bure kwa wazee. Utekelezaji wa jambo hili unaelekea kukabiliwa
na changamoto nyingi zikiwamo za kukosekana kwa dawa na vifaa tiba kwa
ajili ya wazee, hivyo kukwamisha dhamira nzuri ya serikali.
Ni kupitia uzoefu huo wa utoaji wa huduma za bure za matibabu kwa
wazee, ndipo nasi tunapolazimika kupongeza uamuzi huu mzuri wa kuwalipa
pensheni wazee, lakini tukisisitiza kuwa ni lazima kuwe na utekelezaji
wa kweli utakaoleta nafuu kwa wazee.
0 comments:
Post a Comment