Siku moja baada ya Waziri wa Fedha, Saada
Mkuya kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka
2015/16, Waziri wa Fedha Kivuli, James Mbatia amesema watawasilisha bajeti yao
ambayo kama Serikali itaipuuza, itawagharimu. Mkuya aliwasilisha Bajeti ya
Serikali ambayo makadirio yake ni Sh22.4 trilioni.
Akizungumza kwa kifupi jana kwenye Viwanja
vya Bunge mjini Dodoma, Mbatia ambaye hakutaka kuingia kwa undani akiahidi
mambo yote Jumatatu, alisema kuwa watawasilisha bajeti ikiwa na vielelezo
vyote, takwimu zilizofanyiwa kazi, bajeti ndogo lakini inayokidhi na kugusa
maisha ya Mtanzania.
Alisema kuwa bajeti ya Serikali imejaa
mbwembwe, lakini bajeti ya upinzani inalenga kwenye maeneo ya msingi, yanayomgusa
Mtanzania na yenye kueleza maisha nafuu ya Mtanzania. “Tumeangalia tozo katika
maeneo mbalimbali, tumeifanyia uchambuzi, inatekelezeka ni bajeti rahisi,”
alisema Mbatia ambaye ataiwasilisha kuanzia saa 10:00 jioni.
Baada ya bajeti kusomwa juzi, wabunge
walipewa siku tatu ili kupitia maeneo mbalimbali ya bajeti hiyo na kuwasilisha
hoja zao kwa ajili ya kuipitisha.
Akizungumza baada ya Mkuya kumaliza
kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16, Spika Anne Makinda ambaye hii
ni bajeti yake ya mwisho kuisimamia akiwa Spika, alisema: “Wale mtakaoendelea
na Bunge, muifanyie kazi bajeti hii, mhakikishe yote yaliyopendekezwa
mnayafanyia kazi.”
“Halafu mje tuijadili hapa. Tutaanza
kuijadili Jumatatu kwa siku saba mfululizo. Mje, hata kama mna homa ya uchaguzi,
siku saba haziwezi kuwavurugia mipango yenu. Tunataka mje tuijadili, lakini
bila matusi. Muungwana siku zote anashindana kwa hoja, mje na hoja zenu, lakini
si matusi,” alisema Spika Makinda ambaye tayari ametangaza kutowania tena
ubunge katika Jimbo la Njombe Kusini.
Kati ya waliotoa maoni yao ni Kiongozi wa
Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye alisema bajeti hiyo haina
nafuu kwa Mtanzania masikini. “Haya ni maneno matamu ya kuwahadaa Watanzania
kwa kuweka vifungu vya kuwapa matumaini kwao,” alisema akisisitiza ni bajeti ya
kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Alisema kwamba kambi ya upinzani ilitoa maoni
ya kutaka kuanzishwa kwa mafao kwa wazee wote tangu bajeti ya mwaka 2012/2013.
Hata hivyo, licha ya kutajwa tena wanafanya maandalizi ya kuweza kutoa pensheni
hiyo kwa wazee haitaweza kutekelezeka katika mwaka wa fedha 2015/16.
Alisema haitaweza kutekelezeka kwa sababu
hakuna mpango wa kuileta sheria ya pensheni kwa wazee katika Bunge hili. “Hili
ni changa la macho kwa wazee hakuna atakayelipwa pensheni katika mwaka ujao wa
fedha,” alisema Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema).
Alisema, katika bajeti hii kuwapo ongezeko la
kodi na ushuru wa mafuta nchini wakati bei katika soko la dunia inapungua kila
siku kutaongeza gharama za maisha. “Watu wanaweza kufurahi sasa miradi ya umeme
vijijini itatekelezeka kwa kuwa fedha hiyo itaenda moja kwa moja Rea (Wakala wa
Umeme Vijijini) lakini katika mwaka uliopita, ingawa fedha hizo ziliwekewa
uzio, zilichotwa na kupelekwa katika matumizi mengine,” alisema.
Alisema tatizo kubwa la nchi liko katika
utekelezaji wa mipango ya serikali. “Nusu ya mawaziri hawapo wakati bajeti yao
inasomwa bungeni. Kwa nini wabunge wao hawapo bungeni, sisi wabunge wa kambi ya
upinzani wote tulikuwa bungeni,” alisema.
TGNP waichana bajeti
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment