Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia (pichani), alisema
kinachofanywa na serikali kuongeza kodi ni kuongeza ugumu wa maisha ya
Watanzania hasa wa kipato cha chini.
"Tulipendekeza maeneo kadhaa ambayo pia yalipendekezwa na kamati
ya Spika ya kuisaidia serikali kuibua vyanzo vipya vya mapato na kutoa
taarifa yake kwako, maarufu kama Chenge 1, lakini kwa kiasi kikubwa
serikali haijafanyia kazi ipasavyo taarifa hii," alisema.
Alisema ni vema taarifa hiyo ikatekelezwa na mapato yatapatikana
katika kuendeleza sekta ya umeme, maji, elimu, afya badala ya kubebesha
mzigo huo kwa Watanzania.
"Tunazidi kuitaka serikali iangalie na kutumia vyanzo vipya vya
mapato hasa sekta ya uvuvi katika Bahari Kuu ukusanyaji wa kodi za
majengo kwa ufanisi, mazao ya misitu na kuweka utaratibu wa kurasimisha
sekta isiyo rasmi katika tasnia mbalimbali za uchumi na kuongeza
asilimia 40 ya Pato la Taifa,"alisema.
Kwa mujibu wa Mbatia, mabadiliko katika sheria ya leseni za
biashara inayoweka sharti kuwa ili mfanyabiashara aweze kupata leseni ya
biashara lazima awe na hati ya ukaguzi wa kodi, iwapo itaanza kutumika
Julai mosi, mwaka huu, italeta usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara
pamoja na kujenga mianya ya rushwa, urasimu na migogoro baina ya
wafanyabiashara na serikali.
Alisema hakukua na ushirikishwaji wa wadau na kwamba
hayajaandaliwa mazingira rafiki na yanayojitosheleza katika utekelezaji
wa sheria na kwamba halmashauri zimejiwekea viwango visivyotabirika na
vinavyobadilika mara kwa mara vya kodi ya leseni.
Waziri huyo alisema miradi ya uwekezaji ya hadhi maalum ambayo
itapewa misamaha mikubwa ya kodi kwa wenye masharti ya uwekezaji wa dola
za Marekani, ni muhimu kwa serikali kutoa taarifa bungeni kuhusu
utaratibu iliyojiwekea wa kutoa vivutio hivyo na ufanisi wa utekelezaji.
0 comments:
Post a Comment