Kurejea kwao kumeongeza matumaini ya
kupatikana amani licha ya kuripotiwa mapigano mapya karibu na visima vya mafuta
vya nchi hiyo.
Wapinzani hao walionekana kuwa washirika wa
kiongozi wa waasi Riek Machar wakati mapigano yalipozuka miongoni mwa majeshi
ya serikali katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba mnamo Desemba 2013. Serikali
ilidai njama ya kumpindua Rais Salva Kiir ilizimwa, na kuwazuilia washirika
kadhaa wa Machar wakati machafuko yakisambaa kote nchini humo.
Chini ya upatanishi wa jumuiya ya ushirikiano
wa nchi za mashariki na pembe ya Afrika IGAD, baadhi ya wapinzani hao
waliachiliwa huru na kuhamishiwa Kenya. Na sasa wale waliorudi nyumbani jana
pamoja ni Deng Alor Kuol, John Luk Jok, Kosti Manibe Ngai, Cirino Hiteng na
Madut Biar. Wote ni mawaziri wa zamani waliohudumu katika serikali ya Kiir.
Naibu rais wa Afrika Kusini Cyrile Ramaphosa,
ni miongoni mwa viongozi wa Afrika walioandamana na wapinzani hao kwenda Juba
na akawaambia waandishi wa habari kuwa kurejea kwao kunaashiria “siku kubwa ya
amani nchini Sudan Kusini“. Kuol amesema wapinzano hao wamerejea nyumbani ili
kushiriki mazungumzo ya kukiunganisha chama tawala na kumaliza vita katika
taifa hilo.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anasema viongozi
wa IGAD wataleta nguvu mpya kuzipa msukumo juhudi zilizokwama za kutaka
kuukomesha mzozo wa Sudan Kusini ambao umedumu kwa miezi kumi na saba.
"Mchakato wa IGAD utaanza tena mnamo Juni saba, ili kujaribu kuleta amani
na utulivu kwa ndugu zetu wa Sudan kusini. Na tunapoanzisha mchakato huu, na
nasema wazi huu sio uhitimisho, bali kuongezwa nguvu, kuwekwa pamoja michakato
miwili ambayo imeendelea sambamba ikiwa na matumaini ya kuhakikisha kuwa
Wasudan Kusini wanaweza kunufaika, wanaweza kufurahia uhuru, na mafanikio
ambayo wangeyapata tokea mwanzo".
Wakati huo huo, Sudan Kusini imeamua kumtimua
mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Toby Lanzer wiki chache tu kabla ya
kuondoka ili kupewa majukumu mengine.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
alilaani hatua hiyo na kutoa wito kwa serikali kuubatilisha maramoja uamuzi huo
dhidi ya Lanzer, raia wa Uingereza ambaye pia alihudumu kama naibu wa balozi wa
Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini. Lanzer alikuwa anakaribia kukamilisha
muhula wake na Eugine Owusu wa Ghana tayari alikuwa ameteuliwa kuchukua nafasi
yake.
Hakuna sababu iliyotolewa kwa kutimuliwa
kwake, lakini maafisa wa Umoja wa Mataifa wamedokeza kuwa ukosoaji unaofanywa
dhidi ya serikali na waasi kuhusiana na kuongezeka kwa mapigano huenda
uliikasirisha serikali ya Kiir.
0 comments:
Post a Comment