Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa la Chama cha Wananchi (CUF), limeutaka uongozi wa chama hicho kusitisha uamuzi wa kumpata mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia vyama vinavyounda Ukawa hadi suala hilo litakapojadiliwa kikatiba ndani ya chama hicho Julai 25.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye
Ofisi Kuu ya chama hicho Buguruni, Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu
Bara, Magdalena Sakaya alisema wajumbe wa baraza hilo ndiyo wenye uamuzi
wa kutoa tamko la kuendelea kuwamo ndani ya Ukawa au kujitoa.
Taarifa hizo za CUF zinakwenda tofauti na taarifa
iliyotolewa juzi na Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia kwamba
wamekamilisha mazungumzo ya kumpata mgombea wa urais ambaye atatangazwa
kwenye mkutano wa hadhara muda wowote ndani ya siku saba.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi
akizungumza akiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti
wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi na viongozi wengine wa vyama hivyo, alisema
hakuna mpasuko kama inavyodaiwa na kusisitiza kwamba bado wapo na CUF
katika umoja huo.
Hata hivyo, jana Sakaya alisema: ”Hili la kujiunga
na Ukawa linatakiwa kujadiliwa kwa kina na Baraza Kuu na hata
ikiwezekana kuwashirikisha na wanachama ndipo mwafaka wa kujiunga au la
utolewe.”
Alisema hata baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba kutangaza mbele ya viongozi wa Ukawa kwamba juzi
wangemtangaza mgombea wa urais lilikuwa ni kosa kwani liliwashtua
wajumbe wa Baraza Kuu kwa kuwa hawakushirikishwa.
Alisema kutokana na katiba ya chama hicho, hakuna
kiongozi yeyote mwenye mamlaka ya kutangaza jambo kama hilo hadharani
bila ya kushirikisha Baraza Kuu ili litoe baraka zake. Alisema jambo
jingine ambalo liliwashtua wajumbe wa baraza hilo na wanachama wao ni
baada ya kusikia taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya habari na mitandao
ya kijamii kwamba tayari mgombea urais kupitia vyama vinavyounda Ukawa
ameshapatikana.
“Ni jambo la kushangaza kwani mpaka idadi ya kura
ambazo mgombea huyo kupitia chama fulani alizozipata zimewekwa hadharani
kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, suala hili
lilitushtua sisi viongozi na hata wajumbe wa baraza Kuu hivyo tumeona
tulijadili kwanza,” alisema.
Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na Bunge wa
CUF, Shaweji Mketo alisema ni muhimu Watanzania wakatambua kwamba CUF
haijajitoa Ukawa, bali ni mchakato tu unaoendelea kwa mujibu wa sheria
ya chama hicho.
Alisema nchi inapitia kipindi kigumu na pia
ongezeko la majimbo 26 ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) katika kipindi kifupi kabla ya kuanza kwa kampeni, ni
changamoto kubwa kwa Ukawa.
Alisema CUF ina imani kwamba kwa maridhiano ya
pamoja, Ukawa itajengwa imara na hatimaye kuwa na mgombea mmoja wa
urais, wabunge na madiwani.
0 comments:
Post a Comment