Dr. Clifford B. Majani
Mkomamanga (Punica granatum)ni
mmea ambao asili yake ni katika nchi za Mashariki ya Kati (Middle East)
na umetajwa sana katika vitabu vya kale vya historia ya eneo hilo. Kwa
mujibu wa kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyoandikwa na Taasisi ya Utafiti
wa Kiswahili (Institute of Kiswahili Research) ya Chuo Kikuu cha
Dar-es-Salaam-Tanzania, mkomamanga ni mti unaozaa matunda ambayo maganda
yake huchemshwa na kufanywa dawa ya kufunga kuhara (TUKI, 1981). Hii
inaonyesha kuwa wenyeji wa Upwa wa Afrika Mashariki wamekuwa na uzoefu
wa kutosha kuhusiana na uwezo wa tiba wa mmea wa mkomamanga kwa muda
mrefu hasa ikizingatiwa kuwa wamekuwa na mfungamano wa kihistoria na
wageni toka Mashariki ya Kati kwa kipindi kirefu.
Mkomamanga
una dawa mbalimbali kama vile Tannis (punicalin na punicalagin),
Flavonoids, Alkaloids, Steroids, Triterpenes na Polyphenols. Dawa hizi
hupatikana katika magome, majani, mbegu, maganda ya matunda, juisi ya
matunda na katika maua ya mkomamanga. Tunda la komamanga pia lina
vitamini C na E kwa wingi pamoaja na madini ya potassium na copper.
Faida za kitabibu za mmea-dawa huu.
Katika
majaribio ya kisayansi imethibitika kuwa juisi ya komamanga na fukuto
ya mmea huu husaidia kudhibiti kasi ya kuzaliana kwa virusi vya UKIMWI
namba 1 [HIV-1]. Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Neurath A. R
pamoja na wenzake na kupewa kichwa kisemacho “Punica granatum juice
provides an HIV-1 inhibitor and candidate tropical microbicide”. Utafiti
huu ulichapishwa katika jarida la kisayansi la BMC infectious diseases
(4) 41-45(2004). Matokeo yanayofanana na hayo pia yalithibitika katika
utafiti mwingine uliofanywa na Kun Silprasit na wenzake mnamo mwaka wa
2011 na kupewa jina la “Anti-HIV-1 Reverse transcriptase activities of
hexane extracts from Asian Medicinal Plants”. Utafiti huo ulichapishwa
katika jarida la kisayansi la “Journal of Medical Plant Research Vol. 5
(17), pp. 4194-4201, 9 Sept 2011”.
Dawa
zinazopatikana katika maganda na majani ya mkomamanga husaidia katika
matibabu ya hali ya tumbo kujaa gesi na kudhibiti tindikali (acid)
tumboni. Mkomamanga pia husaidia katika matibabu ya kuhara damu na
kutibu uambukizo katika kibofu cha mkojo (Cycititis).
Lojo
ya mbegu za matunda ya komamanga ikichanganywa na maziwa, husaidia
katika tiba ya kuondosha mawe katika figo. Fukuto ya Mkomamaga husaidia
katika tiba ya minyoo aina ya tegu (Tapeworms) lakini pia husaidia
katika matibabu ya uvimbe wa wengu (Spleen). Dawa-lishe hii pia husaidia
kwa kiwango kikubwa katika uponaji wa vidonda vya tumbo.
Katika
jaribio moja lililofanywa kwa wanyama, dawa hii ilionyesha uwezo mkubwa
sana (97.4%) wa kuponya vidonda vya tumbo. Kazi hii hutokana na uwezo
wa dawa hii wa kudhibiti bakteria aina ya Helicobacter pylori ambao kwa
kiasi kikubwa huchangia kutokea kwa vidonda vya tumbo (70 -80% ya
vidonda vya mfuko wa chakula na 90% ya vidonda katika utumbo). Hii ni
kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Hu W. na wenzake mnamo mwaka 2006 na
kupewa kichwa kisemacho “Study of in-vitro inhibition effect of
Pomegranate rind on H.pylori”. Utafiti huu ulichapishwa katika jarida la
Academic Journal of Kunming Medical College 27, 25-27.
Utafiti
mwingine uliofanywa na H.R. Rahimi na wenzake mnamo mwaka 2011
ujulikanao kwa jina la “Punica granatum is more effective to prevent
Gastric Disorders Induced by Helicobacter pylori or any other stimulator
in humans” uliochapishwa katika jarida la kitabibu la Asian J. of Plant
Sciences 10 (7): 380-382, 2011; pia ulithibitisha uwezo wa mkomamanga
katika tiba ya vidonda vya tumbo. Lakini pia uwezo wa dawa hii wa
kupunguza uzalishaji wa tindikali tumboni, huchangia katika uponaji wa
haraka wa vidonda vya tumbo.
Katika mfumo
wa damu, komamanda hutoa msaada mkubwa wa kuzuia na kutibu magonjwa
yanayoshambulia mfumo huo nyeti. Komamanga ni dawa nzuri ya kuzuia na
kutibu shinikizo la damu, magonjwa ya nyama za moyo, kiharusi
(Cerebrovascular Accident) na magonjwa ya mishipa ya damu. Komamanga
lina madini aina ya potassium na copper kwa wingi, pamoja na faida
zingine mwilini, madini haya husaidia kusharabiwa (kufyonzwa) kwa madini
ya chuma kutoka katika utumbo kwenda mwilini kwa urahisi na hii
husaidia katika matibabu na kinga ya tatizo la upungufu wa damu mwilini.
Komamanga
pia ni mahili katika tiba na kuzuia magonjwa ya kusendeka (magonjwa ya
muda mrefu) kama vile saratani ya tezi ya prosteti ya wanaume, saratani
mbalimbali, kisukari, baridi yabisi na uvimbe wa maungio ya vidole
(gout). Komamanga husaidia mwili kuondosha sumu na uchafu utokanao na
kemikali na mabaki ya vyakula mwilini kama vile asidi ya uriki (uric
acid). Sumu hizi ni chanzo kikuu cha magonjwa mengi ya kusendeka.
Komamanga
pia husaidia katika jitihada za kukabiliana na tatizo la unene wa
kupindukia (Obesity). Husaidia katika matibabu ya tatizo la ini pale
linapolemewa (Liver congestion). Dawa ndani ya komamanga licha ya kuwa
na uwezo wa kudhibiti aina kadha wa kadha za bakteria wanaosababisha
magonjwa mwilini, pia zina uwezo wa kukabiliana na virusi wa aina
mbalimbali wanaosababisha magonjwa kwa binadamu.
Kwa
mujibu wa wasomi na wanazuoni wenye shahada za uzamivu, Dk. Navindra
Seeram na Dk. Risa Schulman, komamanga kwa hakika ni dawa asilia
inayotamba katika tiba za kisasa (Modern Medicine) kwenye karne ya 21.
Kipimo
Dawa-lishe
hii hutumiwa kwa kunywa fukuto inayotokana na sehemu za mmea kiasi cha
gram 3 hadi 9 kwa siku inatosha kwa ajili ya tiba ya magonjwa
mbalimbali. Kwa ajili ya minyoo ya tegu magome au mizizi ya mkomamanga
kiasi cha gram 50 huchemshwa katika lita 1 ya maji ili kupata fukuto.
Juisi
ya matunda yake pia inaweza kutumiwa kiasi cha bilauli moja kila siku
ili kukinga magonjwa mbalimbali. Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali dawa
hii ni salama kama itatumiwa kulingana na kipimo sahihi. Tahadhari
ichukuliwe kuhusu matumizi ya dawa hii kwa wanawake wajawazito na kwa
watoto chini ya umri wa miaka 12 kwani hakuna taarifa za kutosha
kuhusiana na usalama katika makundi haya.
Madhara yanayoweza kutokea kwa kutumia dawa-lishe hii (Adverse reactions)
Matumizi
ya kipimo kikubwa cha dawa hii ikiwa katika hali yake ya asili (zaidi
ya gram 80) kinaweza kusababisha kizunguzungu, maumivu makali ya kichwa,
kushindwa kufumbua macho, kutapika, kuzimia na wakati mwingine inaweza
kusababisha kifo. Dawa hii pia inaweza kusababisha mwili kunyong’onyea,
kutokuona vizuri, kushitukashituka kwa misuli na kutetemeka kwa mikono
kama mlevi (tremors).
Onyo:
Ni vizuri
kuepuka matumizi holera ya dawa hata kama ni dawa za asili. Si kila dawa
ya asili ni salama kama itatumiwa bila kufuata ushauri wa mtaalamu
aliyesoma na kuelewa vizuri sayansi ya tiba asilia na lishe. Mimea ina
kemikali za asili hivyo inapotumiwa ni lazima tahadhari zichukuliwe
kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.Kumbuka mimea ni dawa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment