Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza la
Mitihani la Taifa (Necta) jana, wanafunzi 35 walishindwa kufanya
mitihani hiyo baada ya kuugua ghafla.
Akitangaza matokeo hayo mjini Zanzibar jana,
katibu mtendaji wa Necta, Charles Msonde alisema kati ya wahitimu
waliofaulu, wasichana ni 11,734, sawa na asilimia 98.56 na wavulana ni
27,119, sawa na asilimia 97 ya watahiniwa.
Kwa mujibu wa Msonde, Shule ya Sekondari ya Feza
ya jijini Dar es Salaam iliongoza katika orodha ya shule 10 bora
inayojumuisha pia shule za Runzewe (Geita), Feza Girls (Dar), Sumbawanga
(Rukwa), Ivumwe (Geita), St Mary’s Mazinde Juu (Tanga), Vwawa (Mbeya),
Kisimiri (Arusha), Namabengo (Ruvuma) na Scolastica (Kilimanjaro).
Orodha ya shule kumi zilizofanya vibaya inaongozwa
na Shule ya Sekondari ya Meta ya Mbeya, iliyoshika mkia ikifuatiwa na
Kwiro (Morogoro), Mtwara Tech (Mtwara), Iwalanje (Mbeya), Lugoba
(Pwani), Kaliua (Tabora), Kilangalanga (Pwani), Lwangwa (Mbeya),
Ilongero (Singida) na Bariadi ya Simiyu.
Msonde alisema kwamba kiwango cha ufaulu kwa
matokeo ya kidato cha sita kimekuwa kikiongezeka kila mwaka kutokana na
juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuboresha kiwango cha
elimu kwa maendeleo ya Taifa na wananchi wake.
Alisema kwamba matokeo ya mtihani ya mwaka huu
yanaonyesha kiwango cha ufaulu kimepanda kwa asilimia 0.61 kutoka
asilimia 98.26 mwaka 2014 hadi asilimia 98.87 mwaka 2015.
Alisema kwamba katika shule kumi bora kitaifa,
kuna shule tano za Serikali wakati katika orodha ya shule 20 bora, shule
13 za Serikali zimeongoza, zikifuatiwa na shule saba za binafsi.
Hata hivyo, alisema wanafunzi 35 walishindwa
kufanya mitihani yao, wakiwamo 10 ambao walishindwa kumaliza mitihani
baada ya kuugua na 25 waliougua kabla ya mitihani kuanza na kwamba Necta
imeafiki wanafunzi hao warudie mitihani yao Mei mwakani.
“Kati ya wanafunzi hao watano wamefutiwa matokeo
ya mitihani baada ya kuthibitika waliingia kwenye vyumba vya mtihani
wakiwa na karatasi za kuwasaidia kujibu maswali ya mitihani wakati ni
kinyume na sheria,” alisema Msonde.
“Watahiniwa waliofanya vizuri zaidi wamepatikana
kwa kulinganisha wastani wa pointi kwenye masomo ya tahasusi pamoja na
wastani wa alama za jumla walizopata katika masomo yao,” alisema Msonde.
Msonde alisema kwamba wanafunzi hao wameonyesha
uwezo mkubwa katika masomo ya sayansi na kuingia katika kundi la
wanafunzi wenye kipaji maalum wa mchepuo wakitoka katika mikoa
mbalimbali ya Tanzania Bara.
0 comments:
Post a Comment