Baada ya kitendawili cha muda mrefu kilichokuwa
hakina majibu ya kina juu ya kujiunga UKAWA-Waziri mkuu Mstaafu nchini Tanzania
Edward Lowassa kukitegua jana kwamba sasa ni Mwanachama halali wa Chama cha
Demokrasia na maendeleo CHADEMA ,kwa niaba ya vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi-UKAWA Baadhi ya wananchi jijini Dar es Salaam
wametoa maoni yao juu ya waziri mkuu huyo kujiunga na chama cha Demokrasia na
maendeleo chadema na kuachana na chama cha mapinduzi CCM ambapo wamesema hatua
hiyo ni ya kishujaa na ya kizalendo hivyo wanachukulia kama maamuzi Magumu.
Je, hadhi ya kisiasa ya Lowassa itapanda na kuzidi kufikia ndoto za
utumishi wake, ama atakuwa anaanguka kiasi cha kufikia hatua ya
kusahaulika kwa jamii?
Kwa namna yoyote, hatua ya Lowassa kujiunga Chadema itachagiza kazi
ya mageuzi ya kisiasa hasa katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25,
mwaka huu na `kukitikisa’ Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho nguvu zake
za kisiasa zinaendelea kupungua kutokana na sababu kadhaa ikiwamo
kushamiri kwa vyama vingi vya siasa.
Yanayotokea baada ya Lowassa kujiunga upinzani ni mwendelezo wa
mageuzi yaliyowahi kutokea mwaka 1995 hasa baada ya kufikiwa hatua kama
hiyo kwa aliyekuwa Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, Augustine
Mrema.
Ingawa kuondoka kwa Mrema kutoka CCM `kuliitikisa’ nchi na
kuiathiri CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo, lakini historia
inaonyesha kuwapo pia aliyekuwa Waziri wa Fedha, Profesa Kighoma Ali
Malima (marehemu) aliyefikia hatua kama hiyo kwa kujiondoa CCM na
kujiunga na NRA, baada ya kutoteuliwa kuwa mgombea mwaka 1995, ingawa
hakushiriki zaidi siasa za upinzani kutokana na kifo kilichomkuta akiwa
jijini London, Uingereza.
Mbali na Mrema, ikumbukwe pia kwamba kugombea urais kwa Katibu Mkuu
wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, katika kuwania urais katika Uchaguzi
Mkuu wa 2010, kulileta mageuzi mengine yaliyosababisha waliokuwa
wagombea kupitia CCM, wakiwamo mawaziri waandamizi kushindwa.
Ingawa ni hivyo, ukweli ni kwamba zipo tofauti nyingi za kijamii
kati ya wakati Mrema alipojiondoa CCM kujiunga National Convention for
Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-Mageuzi) na wakati huu
anapoondoka Lowassa.
Miongoni mwa tofauti hizo ni kwamba Mrema `alikorofishana’ na
mawaziri wenzake katika Baraza la Mawaziri kiasi cha kufukuzwa kazi na
aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, wakati Lowassa
‘ametoswa’ katika mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia Chama Cha
Mapinduzi.
Inaweza kuainishwa kwamba Mrema (kwa wakati huo) hakupata fursa
pana ya kuwaunganisha wafuasi wake katika mpango wa kuondoka katika CCM,
hata kama wapo waliotoka kwenye chama hicho wakamfuata NCCR-Mageuzi na
baadaye Tanzania Labour Party (TLP).
Kwa upande wake, Lowassa anaondoka baada ya kuaminika kuwa na kundi
kubwa la wafuasi wanaomuunga mkono ndani na nje ya CCM. Mchakato wa
kumpata mgombea urais kupitia CCM uliompa ushindi Mbunge wa Chato, John
Magufuli, ulikuwa kielelezo cha kuwapo idadi hiyo ya watu wanaomuunga
mkono Lowassa.
Kwa hali hiyo, kama Lowassa atafanikiwa kuondoka na wafuasi wake
walio ndani ya CCM, wakamfuata na kujiunga Chadema ni dhahiri kwamba
uhai wa CCM unaweza kuwa katika hatua za mwisho katika siasa za nchi
hii.
KUKUA KWA UPINZANI
Lowassa anaondoka katika CCM akiwa na nguvu kubwa kisiasa. Lakini
pia anajiunga katika upinzani ambao unazidi kupata nguvu za kisiasa hasa
kupitia Ukawa.
Hatua hiyo inaweza kuibua tofauti kubwa kwa hali ya kisiasa kati
ya ilivyokuwa wakati wa Mrema na sasa. Hivyo matokeo yake itakuwa ni
kuzidi kuiathiri CCM.
Nguvu za upinzani katika siasa na chaguzi zimekuwa zikiongezeka
kupitia viashiria kama ongezeko la kura za urais na idadi ya wabunge na
madiwani wanaotokana na vyama hivyo.
Kwa mfano, Mrema alipojiunga NCCR-Mageuzi na kukiongoza chama hicho
katika Uchaguzi Mkuu wa 1995, kumbukumbu zinaonyesha kuwa kilifanikiwa
kuwapa wabunge 28 wa majimbo, ukiacha wale wa viti maalum.
Yalikuwa ni mafanikio makubwa kwa chama cha upinzani upande wa
Tanzania Bara, ingawa baadaye chama hicho kilikumbwa na mgogoro
uliokisababisha kupoteza umaarufu wake.
Lakini kwa ujumla, upinzani ulizidi kuimarika huku Chama Cha
Wananchi (CuF) kikiimarisha ngome yake visiwani Zanzibar hususani Pemba
na Chadema ikiongeza uwakilishi mpana upande wa Tanzania Bara.
Kwa mfano, baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Chadema ilipata ushindi
mkubwa kwenye majimbo ya miji mikubwa kama Moshi, Iringa, Arusha, Mbeya,
Mwanza na jijini Dar es Salaam, japo kutaja kwa uchache.
Lakini yapo maeneo ya vijijini kama jimbo la Mbulu lililokuwa
linawakilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philipo
Marmo, akashindwa na aliyekuwa mgombea kupitia Chadema, Mustapha
Akoonay.
Hivyo mazingira hayo yanayoashiria kushamiri kwa upinzani na nguvu
za kisiasa za Lowassa, linaweza kuufanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu
kuzidi kuwa mgumu katika ngazi zote na si urais pekee kama
inavyotarajiwa na wengi.
VYOMBO VYA HABARI
Uhuru wa vyombo vya habari katika kutoa taarifa kila zinapotokea ni
sehemu ya nyenzo ya hamasa inayochochea kukuza shughuli za kisiasa
zikiwamo zinazofanywa na wapinzani.
Mathalan, tukio la kujiondoa katika CCM kwa Lowassa na kujiunga
Chadema lilitanguliwa na tangazo la mara kwa mara kupitia vituo vya
runinga, hivyo kuufanya umma wa Watanzania kujiandaa kwa kushuhudia
tukio hilo.
Hata hivyo, inawezekana Chadema na Ukawa wasiishie katika kutangaza
ujio wa Lowassa pekee, bali kumtembeza kwenye maeneo tofauti ya nchi
kwa ajili ya ‘kumtambulisha’ kwa wananchi kama inavyofanyika kwa mgombea
urais kupitia CCM, John Magufuli.
Ikiwa Chadema na Ukawa vitafanikiwa kumfikisha Lowassa kwa
wananchi, wakitumia mkakati kama ilivyokuwa wakati alipokuwa akitafuta
wadhamini katika kuteuliwa na CCM ili awanie Urais, hali hiyo itaibua
hamasa kubwa na kuvipa nguvu za kukubalika zaidi vyama vinavyofungamana
katika Ukawa.
NGUVU ZA UKAWA
Jambo jingine linalochagiza mageuzi makubwa ya siasa kutokana na Lowassa kujiunga Chadema ni kuimarika kwa Ukawa.
Awali Ukawa ilifananisha na mipango iliyoshindwa mwaka 1995 na
2000 kwa upinzani kukusudia kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi za
miaka hiyo.
Hata hivyo, ingawa hali hiyo ilitokea na kila chama kugombea
kivyake, lakini mwaka huu vyama vinne, Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF
vilikuwa na chanzo cha kuunda umoja wao. Chanzo hicho ni msingi
walioubaini katika kuunganisha nguvu za pamoja kwenye Bunge Maalum la
Katiba.
Umuhimu wa umoja ulipojidhihirisha ndani na nje ya Bunge hilo, vikawa mwendelezo unaochagizwa na Lowassa kujiunga Chadema.
KUHAMA NA WAFUASI WAKE?
Hofu iliyopo Lowassa atafanikiwa kuwashawishi wafuasi wake
wakiwamo waliokuwa wabunge kupitia CCM, wakitose chama hicho na
kuelekeza maisha mapya ya kisiasa kwa Chadema na Ukawa?
Ikumbukwe kwamba wakati akirejesha fomu za kuomba kuteuliwa na CCM
kuwa mgombea urais wake, Lowassa alisindikizwa na wenyeviti 15 wa chama
hicho wakati wabunge waliokadiriwa kufikia 150 waliwahi kuripotiwa
kukutana mjini Dodoma wakionyesha kumuunga mkono (Lowassa).
Wapo watumishi wengine katika halmashauri za wilaya, wakuu wa
wilaya na taasisi nyingine za utumishi wa umma, waliaminika kumuunga
mkono Lowassa, wakiwa pamoja na muasisi wa CCM, Mzee Kingunge-Ngombare
Mwiru.
Je, makundi hayo na wengine waliokuwa pamoja na Lowassa ndani ya
CCM watabaki ndani ya chama hicho ama watakuwa tayari kujitangaza katika
maeneo yao siku baada ya siku, kama ilivyokuwa kwa madiwani 20 wa kata
za jimbo la Monduli ambalo dalili zimeshaonyesha wazi kuwa ngome ya
Chadema!
Lowassa akifanikiwa kuyashawishi makundi hayo yamfuate Chadema,
bila shaka atazidi kuwa na nguvu kubwa na kukiathiri chama chake cha
zamani-CCM.
Lakini kama wafuasi hao watamuacha kama ilivyokuwa kwa Mrema mwaka
1995, Lowassa atabaki na mtaji mkubwa atakaoukuta Chadema na Ukawa, na
hilo halitakuwa na maana sana kwake kisiasa.
Ingawa ni hivyo, dalili zinaonyesha wazi uwezekano kwa umma
kushuhudia makundi ya wafuasi wake kumfuata kutokana na hofu ya
kutengwa, `kuzibwa’ midomo, kunyanyaswa ama kudhibitiwa watakapoendelea
kubaki ndani ya CCM.
CCM INAVYOWEZA KUMDHIBITI LOWASSA
Mrema alipoihama CCM palikuwa na matumizi makubwa ya vyombo vya
dola hasa polisi kumdhibiti, ikiwamo kuisambaratisha mikutano yake kwa
mabomu ya machozi.
Kutokana na mabadiliko kadhaa yaliyotokea tangu 1995 hadi sasa,
njia hiyo haitakuwa muafaka kwa CCM na serikali kumdhibiti Lowassa,
badala yake chama hicho kinaweza kuhakikisha wanachama waliokuwa watiifu
(kwa Lowassa)na ambao wameonyesha nia ya kuwania ubunge, ujumbe wa
Baraza la Wawakilishi Zanzibar na udiwani, wanapata fursa hizo.
Kama hali hiyo itatokea, CCM inaweza kudhibiti wimbi la wanachama
wake wanaomtii Lowassa kumfuata katika Chadema, ingawa swali litabaki
kuwa ni kwa namna gani hata wakibaki ndani ya CCM watajiweka kando na
‘siasa za Lowassa’?
Kwa vile hali ya kisiasa imeanza kubadilika sasa, ni wajibu wa umma
kufuatilia ili utakapofika Uchaguzi Mkuu, kila mpiga kura afanye uamuzi
ulio sahihi.
Majibu ya wananchi na fikra zao kuhama kwa Lowassa kwenda Chadema wanaongea hapa#Bofya Kusikia,na kwa Taarifa Endelea kufuatilia Taarifa zetu kumbuka pia ku Like Page yetu hapo juu>>
0 comments:
Post a Comment