Image
Image

Pazia urais CCM kufungwa leo.

WAKATI leo ni siku ya mwisho kwa watia nia wa urais kupitia CCM, makada 33 kati ya 42 wamerejesha fomu huku kila mgombea akizungumzia tatizo la rushwa namna atakavyopambana nalo. Makada waliorejesha fomu jana ni pamoja na Edward Lowassa, Mwigulu Nchemba, Lazaro Nyalandu na Dk Hassy Kitine. Hadi sasa wanachama tisa ambao wanatakiwa kurejesha fomu hizo hawajarudisha na mwisho wake ni saa 10 kamili jioni.
Wagombea hao ni Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Godwin Mwapongo, Balozi Patrick Chokala na Peter Nyalile.
Wengine ni Ritha Ngowi, Helena Elinewinga, Anthony Chalamila na Sonoko Banda. Hata hivyo, Katibu wa Sekretarieti Oganaizesheni ya CCM, Mohamed Seif Khatib alisema hakuna adhabu kwa mtu ambaye atashindwa kurudisha fomu hizo.
Lowassa
Miongoni mwa wanachama waliorudisha fomu jana ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa. Aliporudisha fomu hizo jana alisema amedhaminiwa na wanachama wapatao 879,000 na kutaka wote wanaomtuhumu kwa ufisadi kuacha mara moja.
Alisema ikiwa atateuliwa kuwa mgombea urais na kuwa rais atahakikisha anatumia rasilimali zote kwa faida za Watanzania. Alisema kwa bahati mbaya watu ambao wanakosa hoja, wamekuwa wakiwatuhumu wenzao kwa vitu ambavyo havina ukweli wowote.
“Nataka nitumie nafasi hii kwa wale wote ambao wamekuwa wakinituhumu kwa miaka kadhaa sasa na kunihusisha na suala zima la rushwa, kuwaambia waache mara moja kwani hakuna hata chembe ya ukweli wa maneno hayo,” alisema.
Alisema kwa yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma hizo autoe. “Aseme nimechukua rushwa lini, kwa nani, kwa lipi na kwa kiasi gani,” alisisitiza huku akisema ni majungu na sasa yametosha na ikiwa atateuliwa, ataongoza nchi kwa haki.
Alisema ana shauku kuunganisha uwezo wa kila Mtanzania katika kupambana na umaskini wa nchi, umaskini wa watu siyo amri ya Mwenyezi Mungu kwani kwa pamoja raslimali, maarifa na ufanisi zaidi vitatokomeza umaskini.
Hata hivyo, waandishi wa habari hawakupewa nafasi ya kumuuliza maswali kutokana na muda aliokuwa ametengewa kuisha.
Dk Asha-Rose Migiro
Mwanachama mwingine aliyerudisha fomu jana ni Dk Asha-Rose Migiro ambaye alisema hayuko tayari kuzungumza na waandishi wa habari.
Eldefonce Bilohe
Pia mkulima kutoka Kigoma, Elfonce Bilohe naye alirejesha fomu akikishukuru chama kwa demokrasia iliyoionesha. Bilohe alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kurudisha fomu.
Alisema yeye ni mkulima lakini amepata nafasi ya kushiriki katika kinyang’anyiro hicho, kitendo ambacho kweli kimeonesha kuwa ni chama cha wakulima na wafanyakazi.
Aizungumzia zoezi la kutafuta wadhamini, amesema limeenda vizuri na amekabidhi idadi ya wadhamini waliohitajika kutoka katika mikoa 15 kama chama kilivyotaka. Alisema alikutana na changamoto ya kuombwa rushwa.
“Changamoto kubwa ambayo nimekutana nayo katika kuwapata wadhamini ni baadhi ya watu kuniomba kitu kidogo kama maji ya kunywa,” alisema.
Waziri Nyalandu
Mwingine wa CCM aliyerudisha fomu jana ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu. Akizungumza na waandishi wa habari alisema ana imani na Watanzania na yupo tayari kuhakikisha CCM inashika dola mwaka 2015.
Alisema kila alipokuwa akipita ameona watu wakiwa na mapenzi makubwa na chama chao na hiyo ni ishara kuwa bado wana imani na chama chao.
Akizungumzia kuhusu umoja uliopo katika Taifa alisema kuwa ni lazima kuhakikisha tunu hiyo inalindwa na kuenziwa na kusisitiza kuwa ni lazima kupiga vita ubaguzi wa aina yoyote.
Luhaga Mpina
Kwa upande wake mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina alisema ametembelea mikoa 17 na kusema zoezi lililenda vizuri. Alitoa ushauri kwa CCM kuweka mdahalo kwa wagombea wote wa nafasi ya urais ili kujua nini ambacho watakifanya kwa Watanzania.
Alisema kuwa hana presha na wagombea 42 ambao wamekwishachukua fomu na anaamini kuwa atashinda. Alisema anaamini jina lake litakuwepo katika tatu bora kwa wale watakaoteuliwa na chama.
Malick Malupu
Mwanachama mwingine aliyerudisha fomu ni Malick Malupu, mwanafunzi wa shahada ya uzamili ya utumishi wa umma Chuo Kikuu cha Mzumbe alirudisha fomu aliwataka wagombea wenzake kuwa makini na wapambe wao kwani wanaweza kusababisha mtafaruku au mgongano baina yao. Alisema kama kuna mtu anamuabudu mgombea aachane na chama.
“Ukiona mtu anakatwa jina lake akalalamika ujue ameingia kwa hujuma au kwa njia ya ubatili pamoja na kutoa rushwa,” alisema.
Dk Hamisi Kingwangala
Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kingwangala naye alirudisha fomu na kusema amefanikiwa kupata wadhamini kama ilivyo agizo la chama. Alisema atahakikisha anashughulikia suala la rushwa na ufujaji wa fedha za umma.
Dk Kitine na kesi za rushwa Wakati akirudisha fomu hizo za kuwania kuteuliwa kuwa Rais wa Tanzania, Dk Kitine alisema rushwa ni sehemu ndogo ya ufisadi na kupambana na vitu hivyo kunategemea ushirikiano.
“Rushwa imetapakaa sana na sababu kubwa ya kuamua kuchukua fomu ni pamoja na kuhakikisha nikiwa kiongozi napambana na kukomesha rushwa na ufisadi katika nchi,” alisema. Alisema atahakikisha wahusika wa vitendo hivyo wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Alisema atapeleka bungeni sheria hiyo ili ipitishwe kwani itakomesha kabisa vitendo hivyo kwa kuwa vitawabana wahusika na itatosha kuwa na ushahidi wa kimazingira yaliyosibu mpaka mhusika kupelekwa mahakamani na itatosha mtu kupatikana na hatia.
Alisema jaji au hakimu hawatapewa uhuru wa kuamua adhabu ya kesi za rushwa. ‘‘Tutatengeneza sheria na hatutampa uhuru Jaji au Hakimu kuamua kesi hizo. Hakimu atakuwa na maagizo kutokana na sheria husika, yeye hana uhuru wa kutoa adhabu anayoitaka yeye adhabu itakuwa kwenye sheria,” alisema.
Alisema kwenye sheria hiyo mtoa rushwa na mpokea rushwa wote watashtakiwa na watahukumiwa wa makosa waliyofanya. Dk Kitine alisema rushwa imekuwa chanzo cha matatizo yote yaliyo katika nchi hii.Alisema wakati akitafuta wadhamini alipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi.
Mwigulu kuibadilisha Takukuru
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba wakati anarudisha jana fomu na kusema atapambana na rushwa ambayo imekuwa ikipoteza haki za masikini.
Alisema katika awamu zilizopita wamejitahidi kupambana na rushwa kwa kuanzisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), lakini alisema atabadilisha sheria namba 11/2007 kwani inaleta rushwa juu ya rushwa kuna kipindi kirefu ambacho kimekuwa kikitumia kabla ya mtu kushtakiwa.
“Sheria itabadilika na rushwa itakuwa ni janga maalumu na kuondokana na uchunguzi juu ya uchunguzi. Tutaipa mamlaka taasisi inayofanya jukumu la kukamata na kuondokana na uwezekano wa kutoa mwanya wale wanaokamatwa na kuondokana na uwekezano wa mtu kutumia hela za rushwa kumaliza kesi za rushwa,” alisema.
Pamoja na rushwa, mgombea huyo aliahidi kupunguza tatizo la ajira kwa kiasi kikubwa iwapo nia yake ya kuingiza nchi kwenye uchumi wa kati itafanikiwa.
Mwigulu alisema uchumi wa viwanda utachochea kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa viwanda vya usindikaji ikiwemo wa mafuta ya alizeti na viwanda vingine.
“Kukiwa na soko la uhakika mazao na kukiwa na viwanda kwenye maeneo hayo na vijana wengi watakwenda hapo na kutengeneza ajira kwa wakati moja,” alisema.
Pia alisema uwepo wa viwanda kutapelekea kuzalishwa kwa bidhaa nyingi na kutachochea sekta binafsi kutengeneza mazingira mazuri ya biashara kwa kuondokana na mfumo wa kodi unaokatisha tamaa, rushwa na ukiritimba vijana wengi watakuwa na cha kufanya.
Akizungumzia mabadiliko ya katiba, alisema hakuna haja ya kugombana kwani katiba si Biblia au Kurani ambazo hazifanyiwi mabadiliko, lakini katiba inaweza kufanyiwa mabadiliko.
Alisema hata kuna nchi ziliwahi kuharibikiwa zikiwa na katiba, lakini katiba halisi inakaa moyoni. “Twende kwenye taratibu za kisheria tumalizie suala hili na si kwenda kwenye taratibu za kifujo kwenye sheria hapo tutamaliza tofauti na tafsiri nzuri na kupata kile tunachokipata,” alisema
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment