Watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi walivamia katika Kituo cha
Polisi Stakishari, jijini Dar es Salaam, kuwaua askari polisi wanne,raia wawili na pia dereva wa bodaboda anayetuhumiwa kuwa ni mwenzao.Wahalifu hao walipora bunduki zinazodaiwa kufikia 20 na pia shehena ya
risasi waliyoihifadhi kwenye gunia.
Tambarare Halisi tunalaani mauaji haya.Tunalitaka Jeshi la Polisi lishirikiane
na raia wema kupitia dhana yao ya ulinzi shirikishi kuwanasa wahusika
popote walipo.
Pamoja na yote, tunadhani kwamba sasa ipo haja kwa polisi kuanza
kujitathmini wenyewe huku pia wakishirikiana na raia katika kuendesha
operesheni za kusaka wahusika. Tunasisitiza hili kutokana na mfululizo
wa matukio ya kuvamiwa kwa polisi na vituo vya polisi kuongezeka.
Ikumbukwe kuwa kuanzia Juni mwaka jana peke yake, wavamizi walishaua
askari polisi 7 na kupora jumla ya bunduki 53, ikiwamo 15 zinazodaiwa
kuporwa Stakishari mwishoni mwa wiki.
Takwimu hizi haziashirii mema.Waliouawa wengi na silaha
zilizoporwa ni nyingi pia kiasi cha wahusika kuwa na fursa ya kuamua
watakacho pindi ikitokea kuwa bunduki zote zinazoporwa zinapelekwa kwa
mtu mmoja, au kikundi kimoja cha watu wenye dhamira ovu. Tuombee hili
lisitokee.
Sisi tungali tukijiuliza kwamba je,ni kipi kimetokea hata ikafikia
wahalifu wanapata ujasiri huu wa kuvamia vituo vya polisi na kisha
kuacha vilio vikubwa kwa umma? Ni kwa nini jeuri hii ya majambazi ingali
ikitokea sasa?.Kunani polisi?.
Je,hawa waporaji wa silaha ni majambazi wa kawaida tuliowazoea au
ni wanakikundi fulani wenye kujikusanyia silaha kidogo kidogo kwa
minajili ya kutekeleza mipango ya hatari zaidi kwa mustakabali wa taifa?
Maswali ni mengi. Yanaibuka sasa kwa sababu haikuwa kawaida kwetu
kusikia kila mara kuwa kuna majambazi wameteka kituo cha polisi,
wakafanya mauaji, kupora silaha na kisha kuondoka wakiwa salama.
Sisi bado tunaamini kuwa mara zote, polisi ndiyo mahala sahihi pa
kukimbilia pindi mtu yeyote akijihisi kuwa usalama wake uko shakani.
Kamwe haitarajiwi kuwa wao (Polisi) ndiyo wageuke kuwa waathirika wa
matendo ya uhalifu.
Tunadhani kwamba kwa mwenendo huu, sasa kuna kila sababu kwa Jeshi
la Polisi kujitathmini kwa kina ili kujihakikishia kuwa kila kitu ndani
yake kiko sawa.Msingi wa hoja hii unatokana na shaka nyingine kuwa
pengine, kikulacho kinguoni mwako.
Jeshi la Polisi linapaswa kufuatilia kwa kina juu ya namna
linavyowapata watu wenye sifa ya kuajiriwa kama askari ili kuwa walinzi
wazuri wa raia na mali zao.Wafuatilie upya mchakato wote wa kuwapata
vijana wanaowapeleka mafunzoni kabla ya kuwaajiri, lengo kubwa likiwa ni
kujua kiundani juu ya tabia zao na uadilifu wao.Hili ni muhimu kwani
inapotokea kuwa ndani yake kuna watu huajiriwa kwa sababu zisizozingatia
kanuni na taratibu zao, ni wazi kwamba matukio ya aina hii siyo ajabu
kutokea.
Kama hiyo haitoshi, Jeshi la Polisi linapaswa pia kufuatilia
mitaala inayotumika katika utoaji wa mafunzo kwenye vyuo vyake ili
kuzalisha askari imara wa kukabiliana na changamoto za uhalifu wa kisasa
unaohusisha baadhi ya wavamizi walio na umahiri mkubwa katika mapigano
na matumizi ya silaha za moto.
Wafuatilie pia kujua kama nyendo za askari wote ziko sawa kwani
isije miongoni mwao wakawa wavujishaji wakubwa wa siri zake na mwishowe
kuwapa urahisi wahalifu. Na je, hao wanaopewa nafasi ya kuajiriwa
wanaaminika? Je,utayari wao ukoje?.
Tunakumbushia yote haya kutokana na ukweli kuwa kati ya silaha
zilizowahi kuporwa na majambazi, zipo ambazo wavamizi walitumia silaha
za jadi kuwazidi nguvu askari wetu wenye mafunzo na mwishowe kuwapora
bunduki zao madhubuti kama za aina ya SMG.
Shime, wananchi watoe ushirikiano katika kuwatafuta wahusika wa
matukio kama ya Stakishari na tunasisitiza kuwa, Jeshi la Polisi
lijichunguze pia kwani isije ikawa chanzo cha yote haya ni ndani ya
jeshi lenyewe, kwa maana ya 'kikulacho kinguoni mwako'.
0 comments:
Post a Comment