Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kuwa
litamualika Waziri wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli kuwa mgeni rasmi
kwenye ufunguzi wa michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki
inayoanza mwishoni mwa wiki.
Ikijua wazi kuwa inafanya makosa, TFF ilitoa
mifano mingi ya kuonyesha kuwa uamuzi wa kumuita mwanasiasa kuwa mgeni
rasmi kwenye ufunguzi wa mashindano hayo ni sahihi na kuwataka wananchi
wasilielewe vibaya shirikisho kwa kitendo hicho.
Ni vizuri kuwa TFF imebaini kuwa inafanya makosa
yaliyo dhahiri katika kipindi ambacho wanasiasa wanazidi kukomaa na
hivyo kujua jambo gani linafanywa kwa hila na jambo gani kwa moyo
mkunjufu.
Itakumbukwa kuwa kiongozi wa TFF aliwahi kwenda
ofisini kwa mmoja wa wanachama wa CCM waliokuwa wakitajwa kuwania urais,
kwa ajili ya kujitambulisha mara baada ya kuchaguliwa kiuongoza
shirikisho hilo.
Picha ambayo ilitumwa na TFF kwenye mitandao
mbalimbali, ilieleza kuwa kiongozi huyo alienda kumweleza mikakati ya
shirikisho. Wengi walijiuliza kama ataenda kuwaeleza wagombea wote wa
urais au huyo mmoja.
Kwa hiyo leo tunaposikia tena kuwa shirikisho hilo
limemualika Dk Magufuli kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mashindano
ya Kombe la Kagame, picha inakuja ile ile kuwa TFF inaingiza siasa
kwenye mpira au kuna kiongozi anataka aitumie TFF kwa malengo binafsi ya
kisiasa.
Tunapenda kupinga kitendo hicho cha TFF kuingiza
siasa kwenye michezo na hasa kwenye kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi
Mkuu ambacho vyama vya michezo na taasisi nyingine zisizofungamana na
upande wowote wa kisiasa zinatakiwa zijitenge kabisa na siasa na
wanasiasa.
Tunajua kuwa Dk Magufuli ni waziri, lakini ukweli
kwamba hadhi yake imebadilika baada ya kuteuliwa na CCM kuwa mgombea
urais, inampotezea sifa hiyo ya kushiriki kwenye shughuli za kijamii
zenye chembechembe za kampeni. Kwa sasa huwezi kumtofautisha Dk Magufuli
na mgombea urais wa CCM. Dk Magufuli ni mgombea urais wa CCM na mgombea
urais wa CCM ni Dk Magufuli.
Kwa hiyo hoja kwamba Dk Magufuli anaalikwa kwa
kofia ya uwaziri ni kujaribu kutetea uozo ambao unaonekana dhahiri.
Isitoshe, wakati huu hadhi yake ya kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM
ndiyo inakuja kwanza kuliko hata hicho cheo cha uwaziri na hivyo kumuita
Dk Magufuli kushiriki kwenye shughuli za michezo ni kumpa jukwaa la
kufanya kampeni hata kabla ya muda wake.
TFF ikumbuke kuwa wapenzi wa michezo ni watu wenye
itikadi tofauti, mitazamo tofauti na wengine ambao hata ushabiki wa
vyama haumo ndani yao. Wote hao wanatakiwa kuunganishwa na michezo na si
kutenganishwa. Hivyo, mashabiki hao watakapokwenda uwanjani siku ya
ufunguzi wanataka kuona burudani waliyoifuata ndiyo inatawala na si
siasa ambazo huwachefua baadhi ya wapenzi wa michezo.
Vyama vya michezo havitakiwi kuwa chanzo cha
kubagua au kutenganisha Watanzania, bali kuwaunganisha kwa kuwa moja ya
kazi kuu za michezo ni kuunganisha watu badala ya kuwatenganisha.
Hatuoni kwamba itakuwa busara kwa TFF kuwa chanzo
cha mapingamizi dhidi ya mgombea urais wa CCM itakapofikia muda huo. TFF
na Baraza la Vyama vya Soka vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati
(Cecafa), ambalo linaendesha mashindano hayo, hawana budi kutafakari
upya uamuzi huo na kuubatilisha ili usije kuwa chanzo cha misuguano
kwenye Uchaguzi Mkuu.
0 comments:
Post a Comment