Zoezi la Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la wapiga kura kwa teknolojia ya Biometric Voters
Registration (BVR) lililoahirishwa katika jiji la Dar es salaam na mkoa wa
Pwani hivi karibuni sasa litafanyika kuanzia Julai 7-20 kwa mkoa wa
Pwani na Julai 16- 25 kwa jiji la Dar es salaam.
Uboreshaji wa Daftari
hilo kwa jiji la Dar es salaam na Mkoa wa Pwani uliahirishwa kutokana na
kuchelewa kwa vifaa vya uboreshaji kutoka mikoani ambavyo vilipelekwa ili
kuongeza ufanisi kutokana na maeneo hayo kuwa na idadi kubwa ya watu wenye sifa
ya kuandikishwa kuwa Wapiga Kura.
Mkurugenzi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, Julius Mallaba amewataka wananchi wote wa mikoa hiyo
kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya uandikishaji vitakavyokuwa kwenye Vijiji,
Vitongoji na Mitaa ili kujiandikisha waweze kupiga kura na kuchagua
viongozi wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu Mwezi Oktoba Mwaka huu.
Amewataja watakaohusika
na zoezi hili kuwa ni watu wote waliotimiza umri wa Miaka 18 na kuendelea na
wale watakaotimiza Miaka 18 ifikapo mwezi Oktoba Mwaka huu.
Wengine ni
waliojiandikisha awali kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la zamani ili
kuhuisha taarifa zao na kupata kadi mpya za kupigia kura. Aidha Mallaba
amewataja wengine wenye sifa ya kujiandikisha kuwa ni wale wote wenye sifa za
kujiandikisha lakini hawajawahi kujiandikisha kwenye Daftari hilo.
Amesema wale wote wenye
Kadi za kupigia Kura za zamani wanatakiwa kwenda na Kadi zao ili kurahisisha
uchukuaji wa taarifa zao na kadi hizo zitarudishwa NEC na watapata vitambulisho
vipya. Wananchi wanatakiwa kujiandikisha katika Vituo vilivyopo
ndani ya Kata zao ili kuweza kupata fursa ya kumchagua Diwani, Mbunge na Rais.
Mkurugenzi huyo ametoa
wito kwa wananchi wa mikoa hiyo kuhakikisha wanajiandikisha kwani bila kufanya
hivyo hawataweza kupiga Kura wakati wa Uchaguzi Mkuu. Vituo vya kujiandikisha
vitafunguliwa kila siku kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa ifikapo saa 12:00
jioni.


0 comments:
Post a Comment