Katika tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia jana, inaelezwa kuwa
kundi la majambazi lilivamia kituo hicho cha Polisi na kufanya mauaji
kabla ya kukimbia na bunduki pamoja na risasi kadhaa.
Tukio hili la usiku wa kuamkia jana siyo la kwanza. Kumbukumbu
zinaonyesha kuwa kuvamiwa kwa polisi katika vituo vyao ni muendelezo wa
matukio ya aina hiyo ambayo yalianza kujitokeza Juni mwaka jana.
Sisi tunaungana na Watanzania wengine kuwapa pole wote walioguswa
na msiba huu utokanao na uvamizi wa ghafla na mauaji ya kinyama dhidi ya
askari wetu na raia wasio na hatia.
Hakika, matukio ya aina hii siyo ya kawaida. Kwa sababu hiyo,
yanapaswa kupewa umuhimu wa kipekee na mwishowe kupata majawabu sahihi
kuhusiana na namna ya kuhakikisha kuwa hayajirudii.
Tunasisitiza hili kwavile kuwapo kwa matukio ya aina hii
kunaashiria hali duni ya usalama katika baadhi ya maeneo yetu. Hofu
inatokana na ukweli mwingine kuwa matukio ya ujambazi kwenye vituo vya
polisi yamekuwa yakijitokeza kwa kujirudia. Yasipotafutiwa dawa ya
uhakika kungali mapema, ni wazi kuwa mwishowe yatachukuliwa kuwa ni
matukio ya kawaida na hapo hali itakuwa mbaya zaidi.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa kabla ya tukio la Stakishari juzi,
kulikuwapo pia na matukio kadhaa ya aina hiyo yaliyosababisha mauaji ya
polisi na pia kuporwa kwa silaha.
Kwa mfano, inakumbukwa kuwa Septemba 6 mwaka jana, askari polisi
wawili waliuawa na bunduki zaidi ya 10 aina ya SMG kuporwa katika Kituo
Kikuu cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe mkoani Geita. Katika wiki ya pili
ya Juni mwaka jana, kuna kundi la majambazi lilivamia Kituo cha Polisi
Kimanzichana na kuua askari wawili na pia kupora bunduki mbili aina ya
SMG zilizokuwa na risasi 30.
Matukio ya kuvamiwa polisi, kuporwa silaha, kujeruhiwa na baadhi
kuuawa yamewahi pia kutokea katika maeneo ya Newala, Ikwiriri,
Kimanzichana, Tanga, Pugu, Mgeta na juzi Stakishari.
Ni wazi kwamba kuwapo kwa matukio ya haya kunaweza kuibua hofu
miongoni mwa wananchi, hasa kuhusiana na ujasiri huu wa majambazi
wanaovamia polisi.
Kadri tunavyofahamu, majambazi huwaogopa sana polisi. Hukosa amani kila mara wanapokumbana na polisi.
Wanajua kuwa wakiingia kwenye mikono ya walinzi hawa wa raia na
mali zao, basi kasi yao hii haramu huwa shakani. Kama siyo kukamatwa na
kufikishwa mbele ya mkono wa sheria, ni lazima wataangamizwa. Kwa sababu
hiyo, majambazi huwa wa kwanza kukimbia kila mara wanapojua kwamba
polisi wapo jirani yao. Huogopa kukamatwa na kuchukuliwa hatua kali.
Hivyo, kitendo hiki cha kuvamiwa kwa vituo vya polisi kama
Stakishari kinabaki kuwa miongoni mwa matukio ya kushangaza na
kusikitisha. Ni ishara kwamba wahalifu hawa sasa wamekuwa sugu.
Wamekuwan na jeuri kubwa kiasi cha kuwa na ujasiri wa kuvamia siyo tu
wananchi wasio na hatia na kuwapora mali zao, bali sasa wanavamia vituo
vya polisi na kuwaua walinzi wetu wa amani.
Kwa kuzingatia yote hayo, ndipo sisi tunapoona kwamba sasa kuna
kila sababu ya kuongezwa kwa kasi ya kuwadhibiti wahalifu hawa. Kwamba,
operesheni maalum za kuwasaka wahalifu wa aina hii ziwe endelevu.
Kadhalika, jambo muhimu kwa kila raia ni kuhakikisha kwamba wote
wanaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa jeshi la polisi. Kila
mwenye taarifa za kuwapo kwa watu wanohisiwa kuwa nyendo zao zinatia
shaka, ni vyema wakazifikisha polisi mara moja ili hatua zaidi
zichukuliwe na mwishowe kudhibiti vitendo vya aina hiyo.
Ieleweke kuwa bila ushirikiano wa kutosha kwa polisi, wahalifu kama
hawa waliohusika katika tukio la Stakishari na kwingineko nchini
wataendelea kutamba na kutishia amani na usalama wa watu wasio na hatia.
Tambarare Halisi tunaamini kuwa kwa pamoja, majambazi hawatafua dafu.
Ushirikiano wa kutosha baina ya Jeshi la Polisi na raia utaendelea
kuwabaini mmoja baada ya mwingine na mwisho wa siku, vitendo vya uhalifu
kama huu vitakoma na wauaji kama hawa wa Stakishari watakamatwa mara
moja na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.
0 comments:
Post a Comment