MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga watafungua dimba la michuano ya
Kombe la Kagame dhidi ya Gor Mahia ya Kenya Julai 18 mwaka huu.
Michuano hiyo inayoshirikisha mabingwa wa soka kwa nchi za ukanda wa
Afrika Mashariki na Kati, inatarajiwa kufanyika Dar es Salaam kuanzia
Julai 18 mpaka Agosti 2 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa Baraza la
Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicholas Musonye
alisema maandalizi yote ya michuano hiyo yamekamilika na kwamba
itashirikisha timu 13 zilizogawanywa kwenye makundi matatu. Wenyeji
Tanzania watashirikisha timu mbili, ambazo ni mabingwa wa msimu wa mwaka
2013/2014 Azam na Yanga.
Yanga iliyotwaa ubingwa wa bara msimu wa mwaka 2014/2015 imepangwa
kundi A pamoja na Gor Mahia ya Kenya, Telecom ya Djibouti, KMKM ya
Zanzibar na Khartoum ya Sudan. Azam FC ipo kundi C pamoja na Malaika ya
Sudan Kusini, Adama City ya Ethiopia na KCCA ya Uganda wakati kundi B
lina timu za APR ya Rwanda, Shandy ya Sudan, AAB AFC ya Burundi na
Hegaan FC ya Somalia.
“Tunashukuru sana kwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kuku bali
kuwa wenyeji wetu na safari hii mashindano yatafanyika Dar es Salaam
kila kitu kimekamilika, mechi zitaoneshwa moja kwa moja na kituo cha
SuperSport na mechi itakayofungua mashindano ni Yanga na Gor Mahia,”
alisema Musonye.
Kuhusu zawadi alisema zitakuwa dola za Marekani 60,000, ambapo
mshindi wa kwanza atapata dola 30,000 wa pili dola 20,000 na wa tatu
dola 10,000.
Rais wa Rwanda, Paul Kagame ndiye mdhamini mkuu wa michuano hiyo kwa
muda mrefu, amekuwa akitoa fedha kwa ajili ya zawadi kwa timu tatu za
juu.
Akifafanua kuhusu ushiriki wa timu kwenye michuano hiyo, Mwenyekiti
wa Cecafa Leodegar Tenga alisema Baraza lake hutoa mialiko kwa vyama vya
soka wanachama ambao ndio huchagua timu za kushiriki.
“Sisi kama Cecafa huwa tunatoa mialiko kwa wanachama wetu maana ndio
tunaofanya nao kazi, wao ndio wanaamua timu ipi ishiriki… kuhusu timu
kuleta timu B, hilo hatuwezi kulikubali kwani kuna mashindano ya watoto
ambayo mwaka huu yatafanyika Uganda Desemba, kwa hiyo kama ni timu za
watoto zishiriki huko, mashindano haya ni kwa ajili ya timu za wakubwa
pekee na tumesisitiza hilo,” alisema.
Tenga alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuibuka kwa minong’ono
kwamba Azam inataka kushirikisha timu B kwenye michuano hiyo.
Taji hilo linashikiliwa na El Merreikh ya Sudan iliyoifunga APR kwa
bao 1-0 katika fainali zilizofanyika kwenye uwanja wa Amahoro, Kigali
Rwanda mwaka jana.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment