Katika siku za karibuni, Dk. Slaa amekuwa gumzo kutokana na
kutoonekana katika shughuli mbalimbali za chama hicho pamoja na mikutano
muhimu inayoitishwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa).
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Dk. Slaa alisema kuna
mambo mengi yanayozungumzwa juu yake ambayo hayana ukweli wowote na
kwamba hivi karibuni atazungumza na kuweka hadharani kila kitu.
Hata hivyo, Dk. Slaa hakusema ni mambo gani yasiyo ya kweli
yanayozungumzwa juu yake na wala hakuwa tayari kuweka wazi siku
atakayoweka hadharani yale aliyoyahifadhi moyoni mwake.
Alipoulizwa kuhusu taarifa kuwa atashiriki uzinduzi wa kampeni za
uchaguzi mkuu ujao, Dk. Slaa alisema hakuna ukweli wowote kuhusiana na
jambo hilo na zaidi, akasisitiza kuwa pawe na subira kwani mambo yote
yatajulikana siku atakapozungumza.
“Hakuna ukweli baba... sijui kwa nini watu wanapenda kutoa kauli za
namna hiyo. Ukweli utajulikana tu ndani ya muda mfupi,” alisema Dk.
Slaa kupitia ujumbe mfupi alioutuma kwa namba ya simu yake ya kiganjani
jana.
Awali, Dk. Slaa alipigiwa simu na Nipashe simu yake ya mkononi
ikawa inaita muda mrefu bila kupokelewa, lakini baadaye alipotumiwa
maswali kupitia ujumbe mfupi wa maneno alijibu haraka na kukanusha
taarifa zilizodai kuwa atashiriki uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu
zitakazoanza Agosti 22.
Swali jingine aliloulizwa ni sababu za yeye kuwa kimya na haonekani
katika shughuli za kisiasa za chama chake na Ukawa unaoundwa pia na
washirika wa Chadema; Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.
Hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika,
alikaririwa akisema kuwa amewasiliana na Dk. Slaa na kwamba (Dk. Slaa)
amekubali kushiriki uzinduzi wa kampeni za Ukawa kwenye jimbo la
Kibamba.
Mnyika aliwaambia wanachama wa Chadema wa matawi ya kata ya Goba
muda mfupi kabla ya kufanyika kura za maoni kumchagua mgombea wao wa
udiwani katika eneo hilo.
"Dk. Slaa yupo mapumzikoni na nilizungumza naye kwa kirefu na
aliniambia bado anapumzika, lakini atakuja kushiriki kampeni za chama
Jimbo la Kibamba ambalo mimi nagombea ubunge," alisema Mnyika.
KIKAO KIZITO
Kauli ya Dk. Slaa inakuja huku kukiwa na juhudi kadhaa za
kumshawishi mwanasiasa huyo kujiunga na Ukawa kabla ya kuanza kwa
kampeni mwezi huu.
Mathalan, chanzo kimoja kimeiambia Nipashe kuwa Jumanne wiki hii,
Dk. Slaa alifanya mkutano wa faragha na Mbunge wa Kigoma Kusini, David
Kafulila, kwa takriban saa tano.
Inaelezwa kuwa Kafulila alikuwa akijaribu kumshawishi Dk. Slaa
kubadili msimamo wake ili Ukawa waweze kufanya kampeni wakiwa na umoja.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Dk. Slaa anadai Mwenyekiti wa Chadema
Taifa, Freeman Mbowe, aliwaburuza wenzake katika hatua za mwisho za
kumkubali Lowassa kuhamia chama hicho na hatimaye kuwa mgombea wa urais.
Dk. Slaa pia anahisi kupuuzwa na wenzake hasa kwa kuzingatia
mchango wake wa kukijenga chama hicho tangu mwaka 2010 alipogombea
urais.
Alipoulizwa na Nipashe kuhusiana na taarifa kuwa alikutana na Dk.
Slaa, Kafulila alikiri kufanya hivyo lakini akakataa kuzungumza kiundani
juu ya kile kilichojiri kwa maelezo kuwa ni masuala ya faragha.
"Tuliongea kweli, ni mambo mazito lakini siyo ya kuweka hadharani maana ulikuwa mkutano wa faragha," alisema Kafulila.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na hofu iliyotanda ndani ya Chadema na
wananchi kwa ujumla kutokana na kutoonekana kwa Dk. Slaa katika matukio
mawili makubwa ya kisiasa yanayohusu mustakabali wa chama hicho.
Dk. Slaa hakuonekana siku Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
alipotangaza kujivua uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga
Chadema.
Kadhalika, Dk. Slaa hakuonekana wakati Lowassa alipofika kuchukua
fomu ya kuwania urais kupitia chama hicho akitarajiwa kuwakilisha Umoja
wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Pia hakuonekana katika mkutano mkuu wa Chadema wa kumchagua mgombea
urais na mgombea mwenza na pia katika maandamano ya kumsindikiza
Lowassa yaliyovutia maelfu ya wananchi Jumatatu wakati akienda kuchukua
fomu za kuwania urais kwenye ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment