UMEME ni nishati muhimu kwa maisha ya binadamu na kukosekana kwake
huleta athari kubwa kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa, uzalishaji
viwandani na hata kwa taasisi nyeti, kama hospitali, vyuo na shule.
Katika miaka ya karibuni, serikali imejitahidi mno kuchukua hatua
mbalimbali kuboresha uzalishaji na usambazaji wa nishati hiyo ; na miaka
ya karibuni serikali iliwahi kutangaza kuwa mgao wa umeme, ungekuwa
jambo la kihistoria nchini. Aidha, kuna wakati serikali iliwahi kutenga
kiasi cha Sh bilioni 503 ili kuondoa adha ya mgawo wa umeme.
Hatua nyingine iliyowahi kuchukuliwa na Serikali ni kupunguza gharama
za kuunganisha umeme. Katika mikoa mingi gharama hizo, zilipungua hadi
Sh 450,000 na katika mikoa ya Mtwara na Lindi, wananchi wanaunganishwa
umeme kwa gharama nafuu ya Sh 27,000 tu.
Kwa sasa, idadi ya Watanzania waliounganishiwa huduma hiyo mijini na vijijini, imeongezeka maradufu.
Hata hivyo, kwa karibu wiki mbili sasa, limezuka tatizo la umeme
kukatika mara kwa mara katika jiji la Dar es Salaam, hasa maeneo yote ya
katikati ya jiji, kwa maana ya kata ya Kisutu, ambako kuna maduka
makubwa na madogo, ofisi za serikali, mashirika ya kimataifa, kampuni
binafsi na mashirika ya umma.
Umeme unakatwa ovyo na mara kwa mara pia katika eneo lenye heka heka
nyingi za kibiashara la Kariakoo. Huduma ya umeme pia imekuwa ikikatwa
mara kwa mara katika maeneo ya Temeke, Chang’ombe Magomeni, Kinondoni,
Kigogo, Manzese na Ilala.
Katika jiji la Dar es Salaam, umeme umekuwa ukikatikakatika saa za
kazi hadi jioni na hali ni mbaya zaidi siku za mwishoni mwa wiki,
Jumamosi na Jumapili. Kutokana na kero hiyo, tunakumbusha wafanyakazi wa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kutekeleza ahadi ya serikali
kwamba mgao wa umeme hautakuwepo.
Jambo lingine linalowatatiza watu hivi sasa ni kwamba kwa nini mgao
huo wa mara kwa mara, hautolewi taarifa katika magazeti, redio na
televisheni? Pia, kwa nini haielezwi utakwisha lini? Watendaji wa
Tanesco watambue kuwa katika kipindi hiki tulichonacho sasa, kukosekana
kwa huduma ya umeme, kunachochea maneno maneno yasiyokuwa na tija ya
wananchi kwa serikali yao.
Kwa mfano, mgombea mmoja wa urais akihutubia jijini Mwanza mwishoni
mwa wiki iliyopita, alipojaribu kueleza vipaumbele vyake vya urais
atakavyovitekeleza, wananchi walipaza sauti wakimtaka aelezee
atakavyomaliza kero ya umeme.
Ni dhahiri kelele hizo za wananchi wa Mwanza, zinaonesha kuwa kero ya
umeme kwa sasa haipo Dar es Salaam tu, bali imesambaa hadi mikoani,
kama vile Mwanza, ambalo ni jiji la kibiashara katika Kanda ya Ziwa.
Tunahimiza uongozi wa Tanesco kuondoa haraka kero hii kwa ajili ya
maslahi mapana ya Taifa na Watanzania kwa ujumla. Tuna imani kama
Tanesco itadhamiria, tatizo hili litapungua na baadaye kuwa historia.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment