WANACHAMA wapya wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa na Juma Duni Haji wamepitishwa
katika Mkutano Mkuu wa chama hicho kugombea ngazi ya urais na umakamu wa
rais kwa asilimia 99.3.
Jumla ya wajumbe 2,021 kati ya 2,035
waliotakiwa kuhudhuria kwenye mkutano huo, waliwapitisha wajumbe hao
wapya kwa kishindo katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa
Mlimani City, Dar es Salaam leo.
Lowassa aliyeteuliwa kugombea
urais, alijiunga na chama hicho Julai 28 mwaka huu. Duni maarufu kama
Babu Duni ambaye ndio mgombea mwenza wake akijiunga na chama hicho jana.
Duni
alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), pia Waziri wa
Miundombinu na Mawasiliano katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ),
ambapo nafasi hizo mbili alizivua jana na kisha kujiunga Chadema.
Babu
Duni alilazimika kuvua nyadhifa hizo ili kutii Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayelekeza chama kinachosimamisha rais ndio
kitachosimamisha mgombea mwenza.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya
kuwepo kwa makubaliano ya pamoja ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA) kukubaliana kuunda nguvu ya pamoja ili kukikabili
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.
Katika
mkutano huo, utaratibu uliotumika kupitisha wagombea hao ni kura ya
wazi ambapo kanda 10 za chama hicho kila moja iliposimamishwa ilipiga
kura ya ‘ndio’.
Mratibu wa shughuli ya upigaji kura ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chadema-Taifa, Freeman Mbowe alitaja kuwepo kwa kanda 10
zilizoundwa na chama hicho ambazo ni Kanda ya Ziwa, Kati, Magharibi,
Kusini, Pwani, Pemba, Unguja, Nyasa, Serengeti na Nyanda za Juu Kusini.
Hata
hivyo, wakati wa kumpitisha mgombea mwenza (Duni), ni mjumbe mmoja
kutoka Kanda ya Pemba aliyesimama na kupinga uteuzi wake.
Akizungumzia
utaratibu wa kuteua mgombea huyo Mbowe amesema kuwa, kwa mujibu wa
katiba hiyo kifungu namba 7.16, mgombea urais pamoja na makamu wake
wanateuliwa na sio kupigiwa kura.
Mbele ya wajumbe hao pamoja na
wageni waalikwa kutoka nchi na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi
Mbowe amesema, “Jana Baraza Kuu lilikubali kwa asilimia 100 mapendekezo
ya Kamati Kuu ya kumteua Duni na Lowassa kuwa wagombea wetu.”
Hata
hivyo, Mbowe amesisitiza kuwa, katika kumkaribisha Lowassa kwenye chama
hicho, Dk. Willibrod Slaa ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho
alihusika na aliridhia.
“Narudia Kamati Kuu yote iliridhika
kumkaribisha Lowassa akiwemo Dk. Slaa,” na kuongeza “lakini pengine
nguvu za pembeni zikashauri tofauti.”
Kauli kuwa ‘nguvu za
pembeni zilishauri vingine’ ililenga kuwepo kwa sintofahamu kati ya
chama hicho kuhusu ujio wa Lowassa na msimamo wa Dk. Slaa unaoonekana
kupinga hatua hiyo.
Mbowe amewaambia wajumbe hao kuwa, nchi hii
ina ndoto ya mabadiloko na kwamba, mpaka sasa kazi kubwa imefanywa na
Chadema pia vyama washirika wa UKAWA na hata leo kuwa wamoja.
“Vimefanyika
vikao vingi ikiwa ni sehemu ya kutimiza ndoto hii ya kitaifa, umoja
wetu hautenganishwi kwa misingi ya ukabila, rangi, dini. Tunamuhitaji
kila mtu mwenye malengo chanya kuungana nasi,” amesema Mbowe na
kuongeza;
“Hatuwezi kujenga uadui wa kudumu, tunahitaji karama ya
kila mtu kuunda jeshi la umoja ili kufikia ndoto yetu. Ndoto ya taifa
letu ni kubwa kuliko matumaini ya kila mmoja wetu.”
Amefafanua
kuwa, chama hicho kinatambua kwamba wapo kwenye umoja katika safari hiyo
na kwamba, kila chama kina uwezo wa kusimamisha mgombea wake ngazi zote
lakini kutokana na kuwa na doto ya aina moja, wamekubali kuungana ili
kuitimiza.
Amekumbusha kuwa, katika kuelekea kukamilisha ndoto
hiyo, vyama hivyo vimepigana kwa zaidi ya miaka 20 na kuwa, wapo
waliopoteza maisha, waliopata ulemavu na wengine kuachika katika
harakati hizo.
Hata hivyo, aliwakaribisha wanachama wengine
waliopo nje na kuongeza kuwa “Chadema nchi nzima hatuna haki ya
kuwahukumu wanaohamia.tuwatie moyo na kuwakaribisha vizuri ili ndoto
itimie.
“Sisi wote ni wanaadamu, tuna mapungufu. Wapo watu
watatoka nje na kuja kuishi na sisi kama wana Chadema. Sisi ni chama cha
siasa, chama cha siasa ni watu na sio mahakama. Namkaribisha Lowassa.”
Mbowe mesema “Mabaya ya chama cha zamani tumeyasamehe, tunayaomba mazuri yote mliyoyapata huko mtuletee.”
Pia
Mbowe alieleza wasifu wa wagombea wa chama chake na kuwataka wajumbe,
wanachama na wananchi kutokuwa na mashaka na wateule hao.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment