KUANZIA leo zitakuwa zimebaki siku 11 kabla ya kuanza kwa kampeni za
Uchaguzi Mkuu wa tano wa Tanzania tangu baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa
vyama vingi vya siasa nchini mwaka 1992.
Katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu,
wananchi wa Tanzania bara wanapiga kura kumchagua Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, wabunge na madiwani. Wakati huo huo wananchi wa
Zanzibar wakichagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Wabunge wa Bunge la Muungano,
Wawakilishi wa Baraza la Mapinduzi na Masheha ambao ni sawa na madiwani.
Baadhi ya vyama vya siasa vimeshafanya uteuzi wa wagombea wao kwa
ngazi mbalimbali kuanzia ubunge, udiwani na urais, wakati vingine vikiwa
katika siku za mwisho za kukamilisha uteuzi huo ili kuwahi siku ya
mwisho iliyowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya kupitisha uteuzi
huo.
Kwa mujibu wa NEC, muda wa kuchukua fomu kwa wagombea wa urais
itakamilika Agosti 20, mwaka huu na siku mbili baadaye kampeni za kusaka
kura za Watanzania zaidi ya milioni 23 waliojiandikisha kwa ajili ya
kupiga kura siku hiyo ya Oktoba ili kuchagua viongozi wanaowataka.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni miongoni mwa vyama ambavyo vimefanya
uteuzi wa mgombea urais ambao ulifanyika Julai 12, mwaka huu, kilimteua
Waziri wa Ujenzi Dk John Pombe Magufuli kuongoza upeperushaji wa bendera
ya kijani. Wiki iliyopita Dk Magufuli alikwenda Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kuchukua fomu za kugombea ili kutimiza sheria za Uchaguzi
ambapo aliandamana na Mgombea Mwenza Samia Suluhu Hassan ambaye ni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano.
Baada ya kuchukua fomu Dk Magufuli na Samia walirejea katika Ofisi
Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Mtaa wa Lumumba ambako walipokewa na umati
mkubwa wa wanaCCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya
Kikwete.
Wagomba hao walitumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa maelfu wanachama
waliowasindikiza ambapo Magufuli alionesha wazi kuwa amejiandaa vizuri
pale aliposema haoni wa kumshinda na kwamba yupo tayari kuanza jukumu
kubwa kuwatumikia Watanzania endapo watampatia ushindi katika uchaguzi
wa Oktoba 25 mwaka huu. “Kujitokeza kwenu kwa wingi leo ni ushahidi
mwingine kuwa CCM itaendelea kutawala.
Niwathibitishie kuwa shida za Watanzania nazijua, mategemeo ya
Watanzania ninayo, na ipo misingi mizuri imewekwa chini ya Rais
Kikwete,” anasema Magufuli. Anaendelea kusema,” nawaahidi nitakuwa
mtumishi wenu sababu ninazijua shida za Watanzania. Watanzania wana
tatizo la ajira, hawataki kero za ovyo kama kukimbizana na mama ntilie
na bodaboda. Wanataka uchumi wao uwe mzuri, wanataka maisha mazuri
zaidi.
Nitayasimamia, nawahakikishia sababu kero hizo nazijua. “Nimekuwa
mbunge kwa miaka 20 na kushika nafasi za uwaziri katika wizara
mbalimbali hivyo nimepata uzoefu kutoka kwa Rais Kikwete, Mzee Mwinyi,
Mzee Mkapa, Mzee Nyerere, na viongozi wengine. Niko tayari kukipokea
kijiti kwa mikono miwili,” Magufuli anasema. “Nataka Mwenyekiti
kukuhakikishia kuwa tutashinda, sioni wa kutushinda,” alisema Dk
Magufuli mbele ya viongozi, wanachama, mashabiki na wapenzi wa CCM huku
akirudia maneno ya “sioni wa kutushinda,” alisema mara tatu.
Alisema atakuwa mtumishi wa Watanzania wote bila kujali dini, kabila,
itikadi kwa sababu maendeleo ni ya wote, lakini akawataka wadumishe
umoja na amani, na kuwaahidi kuwa hatawaangusha. “Nitapeperusha bendera
ya CCM kwa manufaa ya Watanzania wote ili kuwaletea maendeleo kwani
maendeleo hayana chama, lakini nitafanya hivyo kupitia CCM kwa sababu
naamini rais bora atatoka CCM....Nawaahidi kuwa nguvu zenu, jasho lenu,
kuacha kazi zenu leo, na muda wenu mliotumia leo hapa, havitapotea bure.
Nasema hazitapotea bure. Nawaahidi Tanzania yenye neema. Ombi langu
kwenu ni kuendelea kudumisha amani na umoja wetu bila ya kujali itikadi
zetu, dini zetu wala kabila zetu,” alisema Dk Magufuli na kusisitiza
kuwa atakuwa mtumishi wa Watanzania wote. Aliongeza: “Sitawaangusha.
Wakati wa kampeni nitasema mengi zaidi, wakati huo nikiwa na Ilani ya
Uchaguzi na yale ya pembeni. Lakini lengo langu kubwa ni Watanzania
kuimarika kiuchumi zaidi na kuondoa kero zaidi. Wajumbe hawakukosea
kuniteua sababu ninazijua shida za Watanzania.
CCM mbele kwa mbele, umoja ni ushindi.” Awali, Mwenyekiti wa Taifa wa
CCM, Rais Kikwete alisema chama hicho sio chama cha mchezo na kuvionya
vyama vya upinzani kuwa watakiona cha mtema kuni katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba. Alisema CCM itapata ushindi katika uchaguzi huo kwa kuwa
imejipanga kwa hoja na imeleta maendeleo nchini, huku akieleza kuwa wapo
watu wenye tamaa ya uongozi ambayo imekithiri.
“Sasa kazi ndio imeanza rasmi. Dodoma zile zilikuwa rasharasha. CCM
sio chama cha mchezo. Watakiona cha mtema kuni. Kama ni mpira wa miguu,
basi tumefunga mabao wakiwa wamesimama. Tumejiandaa vya kutosha na
kushinda tutashinda. Uzoefu, maarifa na uwezo wa kushinda tunao,”
alisema Rais Kikwete na kuongeza: “Nawataka wanaCCM kujipanga,
msimdharau adui yeyote hata akiwa mdogo maadhali yuko upande wa pili
shughulikeni naye.
Tumejipanga kwa hoja, tunazo hoja za kuzungumza. Nchi tulivu na
maendeleo yanaonekana na duniani kote wanajua kuwa Tanzania inafanya
vizuri. Tunao utawala bora, demokrasia na uhuru wa habari. “Hata duniani
wanajua hilo na wanaona fahari kushirikiana na Tanzania. Lakini wapo
watakaokuwa na tamaa tu, duniani wapo watu wameumbwa hivyo, wengine
wanayo tamaa hadi imekithiri, imevuka mipaka,” alieleza Kikwete mbele ya
maelfu ya viongozi, wanachama na mashabiki wa chama hicho tawala.
Lakini wakati kampeni zikitarajiwa kuanza siku 11 zijazo, Dk Magufuli
licha ya kukiri kufahamu shida na matarajio ya Watanzania, lakini kwa
Watanzania, Waziri huyo wa Ujenzi sio mtu wanayemtilia shaka kuhusu
uwezo wake. Amejipambanua kama mtendaji mahiri, mchapakazi na kiongozi
asiyetaka ubabaishaji ambaye kwa muda wote aliofahamika ndani ya
Serikali amekuwa mtu mwadilifu na wa kupigiwa mfano.
Tangu alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi mwaka 2005 na
aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, tangu wakati huo msomi
huyu wa udaktari wa sayansi ya kemia, amekuwa mmoja wa mawaziri wachache
katika Serikali ya Awamu ya Tatu na baadaye Awamu ya Nne, anayefahamika
kwa Watanzania kwa uchapakazi.
Hakuna Mtanzania wa kawaida kuanzia Tunduru hadi Horohoro, Tarakea
hadi Mugumu, Bukoba hadi Singida, Kigoma hadi Dar es Salaam, asiyefahamu
Magufuli si tu kwa jina au kwa sura, bali hata kwa utendaji wake kazi
ambayo ameifanya katika nyadhifa mbalimbali alizokabidhiwa.
Uteuzi wake Dodoma mwezi mmoja uliopita uliwakuna wengi hasa
ikizingatiwa pia kwamba hakuwa mmoja wa wagombea wa CCM aliyetumia muda
mwingi kujipigia chapuo kwamba ndiye anayefaa kuteuliwa kwa nafasi hiyo.
Aliendesha kampeni za kimyakimya, za kistaarabu na zilizozingatia
kanuni, sheria na maadili ya chama chake.
Ana sababu ya kuwavutia wengi kuchaguliwa kuwa mrithi wa Rais Kikwete
kwa sababu ya uwezo alionao, uadilifu, uchapakazi na utendaji
usiotiliwa shaka katika kuongoza. Watanzania hawatafanya kosa
wakimchagua.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment