“KUNA umuhimu mkubwa kwa wanawake kushiriki kwenye mikutano ya
kampeni za kisiasa ili waweze kufahamu sera za wagombea na kuchagua
viongozi watakaosimamia ajenda ya haki na maendeleo ya wanawake,”
anasema Fortunata Makafu.
Makafu ambaye ni Mwezeshaji kutoka shirika la Woman Wake Up (WOWAP)
lenye makao makuu Mjini Dodoma ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati
akizungumza na wanawake wa kata ya Lupeta wilaya ya Mpwapwa kwenye
mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake juu ya kushiriki katika uchaguzi.
Makafu anasema ajenda za wanawake zinatekelezwa kwa kutegemea mfumo
wa maisha katika eneo husika na unaweza kupikwa kwa kuangalia mgawanyo
wa rasilimali kwa kuzingatia kijinsia, vipaumbele vya huduma za jamii,
na ushiriki wa mwanamke katika shughuli mbalimbali za maendeleo na
kwenye vyombo vya kutoa maamuzi. Makafu anasema wakati huu wa kuelekea
uchaguzi mkuu wanawake wanatakiwa kushiriki kikamilifu kwenye mikutano
ya kampeni ili kusikiliza sera za wagombea na hatimaye kumpigia kura
kiongozi ambaye anafaa.
“Wanawake lazima mshiriki kwenye kampeni ili mfanye chaguo sahihi,
usikubali kupokea rushwa, kiongozi anayetoa rushwa hataweza kukuletea
maendeleo ni muhimu kuwaepuka viongozi wa nipe nikupe,” anasema Makafu.
Anawataka wanawake kutambua kushiriki kwenye uchaguzi ni haki yao ya
msingi hivyo wanapaswa kuitambua, kuithamini na kuitumia ipasavyo kwa
kuzingatia na kusisitiza kwa kusema , “haki huwa haiombwi inuka
uitafute.”
Makafu anasena wanawake wengine bado wana mawazo kuwa hawafai
kuongoza lakini inabidi ifike mahali waijue thamani yao katika kuleta
mabadiliko na kushiriki kikamilifu katika shughuli za siasa kwa kupiga
na kupigiwa kura. “Msikubali kununuliwa kwani kura yako ina thamani
kubwa sana kama utaitumia vizuri kwa manufaa ya jamii,” Makafu
anasisitiza.
Mwezeshaji Nuhu Suleiman anasema anawataka wanawake kujitokeza kwa
wingi kushiriki kwenye uchaguzi na watumie vizuri kura zao kwa kuchagua
viongozi ambao wataleta mabadiliko. Anasema ushiriki wa wanawake kwenye
mikutano ya kampeni bado hafifu kutokana na changamoto kubwa ambazo
wanawake wamekuwa wakikabiliana nazo kama vile kunyimwa ruhusu na waume
zao, kuzidiwa na kazi nyingi za nyumbani na uelewa mdogo wa umuhimu wa
kushiriki katika kampeni za kisiasa.
Anasema wanawake wanatakiwa kuachana na dhana potofu kuwa siasa ni
shughuli ya wanaume na kusisitiza kuwa wanawake wanapaswa kushiriki
kikamilifu kuchagua viongozi bora kwa kuwa wana mahitaji mengi zaidi ya
wanaume hasa huduma mbalimbali hasa za afya.
Suleiman anasema vipaumbele vinatofautiana; wakati wanaume wanapoona
kipaumbele chao ni barabara kwa vile wanaendesha pikipiki, gari au
baiskeli, wanawake wanaona kipaumbele chao ni zahanati, maji na shule
kwa kuwa wanapenda kuona watoto wao wakipata huduma nzuri ya afya, maji
safi na salama na elimu bora kwa watoto.
Hata hivyo anawataka wanawake wa Mpwapwa kutambua haki zao na wajibu
wao wa kidemokrasia katika kushiriki uchaguzi mkuu ujao ili wachague
viongozi watakaoweza kusimamia ajenda zao na kuwaunga mkono wagombea
wanawake ambao wana sifa za kuongoza.
Anasema tangu nchi ipate uhuru Tanzania imekuwa ikikabiliwa na maadui
watatu umasikini, ujinga na maradhi na maadui hao wataweza kuondolewa
iwapo watapatikana viongozi wenye uwezo wa kuongoza na kuendeleza mazuri
yaliyofanywa na viongozi wengine.
Pamoja na hayo anasema uoga ni adui mkubwa wa maendeleo ya mwanamke.
Pia anasema asilimia 51 ya Watanzania ni wanawake lakini ushiriki wao
katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi bado ni mdogo. Anasema
wanawake wanatakiwa kushiriki kwenye uchaguzi na kuchagua wale walio
tayari kutekeleza ajenda za wanawake. Anawataka kuona umuhimu wa
kushiriki kwenye mikutano ya kampeni ili kusikiliza sera za wagombea na
kuwauliza maswali pamoja na kuona umuhimu wa kujitokeza kupiga kura.
‘Wanawake ni sehemu kubwa ya jamii na wanahitaji kufanya mabadiliko
ya kimfumo, pia wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kiuchumi wengi
hawana fursa za kiuchumi ni vizuri ukachagua mgombea ambaye yuko tayari
kuleta mabadiliko,” anasema. Anawahimiza wanawake wasikubali kununuliwa
na viongozi wanaotafuta madaraka kwa kutumia fedha kwa kuwa mgombea
anayetoa rushwa hata kuwa na deni endapo atachaguliwa hivyo atatumia
madaraka kutafuta fedha badala ya kuwahudumia wananchi.
“Msikubali kununuliwa kwa kopo la pombe, khanga, kitenge au fulana,
mtalipa yoye hayo kwa kipindi cha miaka mitano kwa kukosa maendeleo....
kwa kuwa kiongozi atakayeinga madarakani kwa kutumia fedha ataendelea na
mambo binafsi na hamtakuwa na uwezo wa kumhoji maana uongozi wake ni wa
kununua,” anasema.... Anasema ni wajibu wa kila mpiga kura kwenda
kwenye mkutano ili kuwasikiliza wagombea na kuwapima.
“Ni lazima mshiriki kwenye mikutano yote ya vyama vya siasa bila
kubagua kwani huwezi kufahamu kiongozi mzuri ni yupi kama utakuwa
hujamsikiliza,” anasema. Anasema kampeni ni harakati za wagombea
kuwashawishi wapiga kura kuwaletea maendeleo ‘nitoe rai mshiriki kampeni
kwa kila mgombea aliyeteuliwa ili kuangalia ni nani analeta maendeleo
bila kujali mwanachama wa chama chako au sio, lakini kama mwananchi ili
kutimiza haki ya msingi ya kila mgombea ili mwisho wa siku ufanye
maamuzi sahihi’’ anasema.
“Ni muhimu sana kujitokeza pale tume itatangaza tarehe ya kampeni ili
kusikiliza sera za wagombea wote, ”anasisitiza. Mratibu wa mradi huo,
Nasra Suleiman anasema mafunzo hayo yanatolewa kupitia mradi wa Fahamu
Ongea Sikilizwa, awamu ya pili, yanalenga wanawake walio kwenye makundi
mbalimbali wakiwemo walemavu na vijana kwa lengo la kuwajengea uwezo juu
ya kushiriki katika uchaguzi.
Anasema mradi huo una lengo kuu la kuhakikisha kunakuwa na usawa na
uwazi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili wananchi waliopo pembezoni
hasa wanawake na vijana waweze kushiriki kikamilifu kama wapiga kura,
wagombea wa nafasi mbalimbali .
Pia kuwahamasisha na kukuongeza uelewa wa wananchi kushiriki
kikamilifu katika uchaguzi kama wapiga kura, watazamaji, waangalizi na
wagombea.” Tunataka kuimarisha uwezo wa wanawake ili washiriki
kikamilifu kwenye mchakato mzima wa uchaguzi.
Anasema wamechagua wanawake kupata mafunzo hayo kwani ni kundi lililo
pembeni na mfumo uliokuwepo umewanyima nafasi za ushiriki kwenye
uongozi na hata wanawake viongozi ni wachache. JU
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment