HIVI karibuni Rais Jakaya Kikwete amekaririwa akisema sekta ya kilimo
inakabiliwa na changamoto sita ambazo zinasababisha sekta hiyo
kushindwa kupiga hatua nchini.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete changamoto hizo ni matumizi ya jembe la
mkono ambalo husababisha uzalishaji mdogo, kilimo kutegemea mvua kila
mwaka, mabadiliko tabianchini, matumizi ya mbegu za asili na matumizi
madogo ya mbolea.
Rais Kikwete alizitaja changamoto nyingine ni kukosa ujuzi na maarifa
kwa wakulima walio wengi hivyo, kujikuta wakilima kilimo kisicho na
tija kwao na Taifa.
Alisema mengi katika kukabiliana na changamoto hizo, ikiwa ni pamoja
na Serikali kuongeza bajeti kila mwaka, ambapo bajeti ya mwaka 2005
walitenga sh. milioni 200, na mwaka jana ilikuwa zaidi ya sh. bilioni
moja.
Pamoja na kuongeza bajeti ni lazima kwenda mbali zaidi kubaini sababu
sa sekta ya kilimo kupewa kisogo au kutothaminiwa. Ni kweli matumizi ya
jembe la mkono yamepitwa na wakati ni muda wa kuwekeza kwenye matrekta.
Ni muda wa kuhakikisha tunawekeza katika kilimo cha umwagiliaji
badala ya kuangalia angani tukisubiri mvua ya Mwenyezi Mungu. Wakati
umefika kutumia mbegu bora. Siku hizi kuna malalamiko ya wananchi
kuuziwa mbegu feki.
Hali hii inawaathiri wakulima kifedha na kupoteza nguvu zao bure.
Katika eneo hili Serikali inatakiwa kuwasaka na kuwakamata wanaowauzia
wakulima mbegu ambazo hazifai. Mbegu ambazo hawezi kustawi.
Si hivyo tu, kuna kila sababu ya Serikali kuhakikisha mazao ya
wakulima yanakuwa na thamani. Ilivyo sasa ni kama vile wakulima
wamekataa tamaa ya kuendeleza kilimo kutokana na kupewa bei ndogo ya
mazao yao.
Kuna kila sababu ya Serikali kuvunja ukimya na kupitia upya bei ya
mazao ya wakulima. Haiwezekani wakulima wapinde migongo, watumie fedha
zao kugharamikia mazao yao, lakini wanapouza wanakopwa au kulipwa bei
ndogo.
Kwa maoni yetu changamoto kubwa ya kuimaliza ni kuhakikisha mazao ya
wakulima yananunuliwa kwa bei nzuri. Kwa kufanya hivyo mazao yaliyotupwa
kisogo, yatafufuliwa na kusaidia kuharakisha kukuza uchumi wa nchi.
Jambo nyingine ni wataalamu wa sekta hiyo kutimiza wajibu wao.
Wakutane na wakulima na kuwashauri namna ya kulima kwa ufanisi.
Wasiishie kukaa ofisini kwa sababu huko hakuna kilimo. Waendee vijijini.
Ni matarajio yetu kwamba umefika wakati muafaka kuzipatia ufumbuzi wa
kweli changamoto zilizopo badala ya kuishia kuzijadili kwa kupapasa. Ni
lazima kila mmoja kwa wakati wake atimize lengo ili kunyanyua sekta
hiyo kwani kwa sasa imedumaa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment