Image
Image

Mahakama yampongeza Kikwete.

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohammed Othman Chande amesema kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa mara kwa mara wa majaji nchini, kimeongezea kwa kiasi kikubwa utendaji wa Idara ya Mahakama na hadi sasa kuna Majaji takribani 100, jambo ambalo halijawahi kutokea miaka ya nyuma.
Aidha, ameahidi kutokana na wingi wao, sasa wana uhakika wa kuongeza uchapaji kazi na kwa kuanzia, wameweka lengo kwamba, kesi zote katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Biashara zisiendeshwe zaidi ya miezi 10.
Jaji Chande alikuwa akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam jana mara baada ya Rais Kikwete kuapisha Majaji wa Mahakama Kuu 13 na Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani. “Tunamshukuru Rais kwa ongezeko hili la majaji ambalo sasa linaifanya Tanzania kuwa na majaji 100, hawa ni wengi haijawahi kutokea,” alisisitiza.
Alisema ongezeko hilo, litasaidia sekta hiyo kushughulikia tatizo la mlundikano wa kesi hasa katika kanda za Mahakama Kuu, ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikielemewa na kesi nyingi.
Alitaja kanda ambazo zina mzigo wa kesi nyingi, ambazo sasa zitapunguziwa mzigo huo kutokana na ongezeko hilo la majaji kuwa ni Kanda ya Mahakama Kuu ya Bukoba, ambayo Jaji mmoja alikuwa akishughulikia kesi 3,000 na Mwanza jaji mmoja kesi 600.
Aidha, alisema ongezeko hilo litasaidia maeneo mengine yenye kesi nyingi pia, ambayo ni Tabora na vitengo vya Mahakama Kuu kama vile Idara ya kazi, Ardhi na Biashara. Alisema tayari sekta ya Mahakama ilishajiwekea mikakati ya kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na kubadilisha ratiba, ambapo kwa upande wa Majaji walipangiwa Jaji mmoja sasa kusikiliza kesi 220, Hakimu Mkazi wa wilaya na Mkoa kesi 250 na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo kesi 260.
“Kila Mahakama pia imewekewa malengo yake na lengo kubwa ni kuhakikisha kesi hazichukui muda mrefu kusikilizwa, kwa mfano kwa mujibu wa mabadiliko haya kitengo cha Biashara cha Mahakama Kuu kesi zake hazitosikilizwa kwa muda wa zaidi ya miezi 10 hadi mwaka mmoja,” alisisitiza.
Aliwataka majaji walioteuliwa na kuapishwa jana kutambua kuwa waliteuliwa katika nyadhifa hizo, kutokana na utendaji, uzoefu na uadilifu wao, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanadumisha sifa hizo katika utendaji wao.
Alisema kabla ya majaji hao hawajaanza rasmi kazi, wataandaliwa mafunzo maalum ili waweze kuendana na utaratibu wa kimahakama kwa kuwa kati ya majaji hao, watano walikuwa mawakili wa kujitegemea, watano mawakili wa Serikali na watano walikuwa mahakamani.
Akizungumzia suala la uchaguzi, Chande, alisema tayari wamejipanga kuhakikisha kuwa kesi za uchaguzi zinasikilizwa kwa haki na muda ambapo hazitosikilizwa kwa zaidi ya miezi sita.
Kuhusu Majaji waliotuhumiwa kupatiwa mgawo wa fedha za akaunti ya Escrow, alisema tume iliyoundwa kufanya uchunguzi na upelelezi, tayari imekamisha upelelezi wake wa awali na itakapokamilisha kuuandaa, itaukabidhi rasmi kwa mamlaka ya uteuzi (Rais) kwa hatua zaidi.
Majaji hao ni Profesa Eudes Ruhangisa anayedaiwa kupata Sh milioni 400.25 na Aloysius Mujulizi Sh milioni 40.4. Awali, akizungumza na gazeti hili kuhusu uteuzi wake, Jaji wa Mahakama Kuu Ignas Kitusi, alisema kuna mipango mingi ya kuboresha huduma za Mahakama, ambapo aliahidi pamoja na wenzake kutekeleza mipango hiyo ikiwemo kurejesha imani ya wananchi dhidi ya Mahakama ambayo kwa sasa imepotea.
Jaji wa Mahakama Kuu, Rehema Kirefu, alisema uteuzi wa Rais wa majaji utasaidia haki kutendeka kwa haraka, kwani uchache wa majaji ulisababisha kesi nyingi kuchelewa kutokana na majaji waliopo kuzidiwa.
Jaji Salima Chikoyo alisema ana uzoefu wa muda mrefu na amefanikiwa kutumikia vitengo mbalimbali hivyo aliwataka wananchi wategemee kupata haki. Majaji wengine waliapishwa jana ni jaji wa Mahakama ya Rufani Richard Mziray na Majaji wa Mahakama Kuu ambao ni Lameck Mlacha, Wilfred Dysobera, Isaya Harufani, Julisu Malaba, Victoria Makani, Lucia Kairo, Benhaj Masoud, Issa Maige, Adam Mambi na Sirilius Matupa.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment