Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotolewa hivi karibuni, uhakiki
utafanyika nchini kote, ukianzia kwenye mikoa mingine na kuhitimishwa
katika jiji la Dar es Salaam.
Ili kufanikisha kazi hiyo, kila mwananchi aliyejiandikisha
ametakiwa na NEC kujitokeza ili kuhakikisha kuwa taarifa zake
zimechukuliwa kwa usahihi.
Sisi tunaungana na NEC katika kuwasihi wananchi wote wenye sifa
kujitokeza ili kuhakiki taarifa zao na za wengine katika maeneo yao.
Tunasisitiza jambo hili kutokana na ukweli kuwa hii ni hatua mojawapo
muhimu kabla ya upigaji kura. Kutotekeleza jukumu hili ni sawa na
kujiweka katika hatari ya kupoteza sifa za kushiriki upigaji kura ili
kuwapata viongozi wa taifa hili katika kipindi kingine cha miaka mitano.
Kila mwananchi mwenye sifa anatakiwa kujitokeza mapema katika siku
zilizoteuliwa kwa kazi ya uhakiki.
Kwa kukumbushia, ni kwamba kazi hii ndiyo itakayomhakikishia kila
mwananchi kuwa na fursa ya kushiriki uchaguzi. Ni kwa sababu kupitia
kipindi hiki, ambacho kwa jiji la Dar es Salaam kitachukua siku tano
kuanzia kesho (Jumamosi), kila aliyejiandikisha atakuwa na nafasi ya
kupitia taarifa zake na kujiridhisha kuwa zimerekodiwa kwa usahihi. Kwa
mfano, kama mtu anaitwa Mussa Ali, umri miaka 23, halafu ikaonekana kuwa
taarifa zake zimekosewa kwa kuandikwa kuwa ni Ally Musa mwenye miaka
32, ni wazi kwamba atalazimika kurekebishiwa taarifa zake katika kipindi
hiki. Kinyume chake, kuna hatari mtu wa aina hii akapoteza haki yake ya
kupiga kura kwani taarifa atakazotoa zitatofautiana na zile
zilizorekodiwa.
Kadhalika, mbali na kurekebisha taarifa binafsi za kila mmoja pindi
zinapokuwa na makosa, kazi hii ya uhakiki pia inatoa fursa kwa wananchi
kupinga kuandikishwa kwa watu wasiokuwa na sifa. Mathalani, ikitokea
kuwa kuna raia wa kigeni wanaoishi nchini isivyo halali wamejipenyeza na
kujiandikisha kama wapigakura, ni wazi kwamba wananchi watakuwa na
fursa ya kupinga kitendo hicho kwa kutoa taarifa kwa maafisa
uandikishaji wa NEC na mwishowe kwenye vyombo vya dola ili watu wa aina
hiyo wachukuliwe hatua za kisheria.
Mbali na kudhibiti wageni, kipindi hiki kinaweza pia kutoa fursa
kwa wananchi wa kila eneo kupata nafasi ya kuwabaini watu wengine wasio
na sifa, wakiwamo wenye umri chini ya miaka 18, watu wasioishi kwenye
maeneo yao na pia kubaini majina ya watu waliopoteza sifa baada ya
kufariki dunia. Nipashe tunaamini kuwa kwa kuzingatia yote haya, wapiga
kura katika kila eneo watabaki kuwa ni wale wenye sifa tu. Na hili ni
muhimu kwani mwisho wa siku, wapigakura wenye sifa ndiyo watakaokuwa na
nafasi ya kuchagua viongozi watakaokuwa madarakani kwa kipindi kingine
cha miaka mitano. Kinyume chake, kama watu wasio na sifa wakiwamo raia
wa kigeni watapata nafasi ya kupiga kura, ni wazi kwamba demokrasia
itapata pigo kwani wananchi wanaweza kupata viongozi wasiowataka.
Kwa kuzingatia yote hayo, ndipo sisi tunaposisitiza kuwa sasa ni
muhimu kwa kila aliyejiandikisha kushiriki kazi ya uhakiki. Hili
lizingatiwe.
0 comments:
Post a Comment