Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imesema kuwa imeunda timu ya ushindi ya kuhakikisha matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu yanatangazwa kwa wakati, ya kweli na haki kwa pande zote.
Akizungumza na Nipashe jana lililotaka kujua mipango ya Tume ili
kuondoa malalamiko ya wananchi, vyama vya siasa, wagombea na wadau
kuhusu kucheleweshwa matokeo na kuzua hofu ya uchakachuaji, Mkurugenzi
wa Nec, Ramadhani Kailima, alisema timu hiyo itakuwa na wajibu mkubwa na
hakuna kulala hadi matokeo yote yawe wazi.
“Tutakuwa na timu ya ushindi kutangaza matokeo yote mapema, hakuna
kulala hadi tutoe matokeo kwa wakati, ya haki na kweli na yanayoaminika
kwa wapigakura,” alisema.
Alisema malalamiko ya kupendelewa kwa chama chochote hayana msingi
wowote kwa kuwa Tume haina chama na haitapendelea chama zaidi ya kuweka
wazi matokeo yote itakayoyapata kwa wakati kwa kuwa watakuwa wanafanya
kazi kisasa zaidi.
Alipoulizwa juu ya uzoefu wa Tume miaka ya nyuma kuhusiana na
kuchelewesha matokeo hata ya maeneo ya mijini kunakofikika kirahisi,
Kailima alisema kama kutakuwa na ucheleweshaji sababu zitawekwa wazi na
wapigakura watatangaziwa bila kificho.
“Ya 2010, yasizungumziwe sasa kwa kuwa tunafanya kazi kisasa
kuhakikisha matokeo yanakuwa wazi na kila hatua wananchi watatangaziwa,”
alisema na kuongeza:
“Tunawaomba wananchi mara baada ya kupiga kura wakae mbali na
ikiwezekana waende nyumbani kwa kuwa kila kituo cha kupigia kura
kutakuwa na mawakala kama kuna tatizo lolote la kufanya matokeo
yasitangazwe kwa wakati, watajulishwa mapema.”
Kailima alisema Nec iko huru na inatekeleza majukumu yake kwa
mujibu wa sheria na kanuni na haiingiliwi kokote kwani katika kugawa
majimbo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kinadaiwa kubebwa na Tume,
kimelalamika na kama wangekuwa wanapendelewa, ni wazi kuwa malalamiko
yao yangesikilizwa, lakini Tume imeamua kufanya kazi zake kwa uhuru.
“Uhuru wetu siyo jina, bali ni kutekeleza majukumu ya kikatiba na
sheria bila kuingiliwa, kiwe chama au mtu hawaruhusiwi kutangaza matokeo
ya uchaguzi, bali msimamizi wa uchaguzi wa kata atatangaza ya kata,
ubunge yatatangazwa na Mkurugenzi wa Manispaa, mji au halmashauri na
Tume itatangaza matokeo ya urais,” alisema.
Alisema watumishi wote wa Tume kabla ya kufanya kazi huapishwa
kujiondoa au kukana itikadi ya chama chake na kuanza kutekeleza majukumu
yake ili kusiwe na upendeleo kutokana na itikadi.
Alipoulizwa kuhusu matukio kadhaa yaliyotokea katika uchanguzi mkuu
wa mwaka 2010 ikiwamo wasimamizi wa baadhi ya majimbo mfano, Shinyanga
mjini kutoroka baada ya kutangaza matokeo yenye utata yaliyompa ushindi
mgombea wa CCM na kuzua vurugu, Kailima alisema:
“Tuko 2015, tumejipanga kikamilifu, ndiyo maana tuna timu ya
ushindi kuhakikisha hakuna ucheleweshwaji wa matokeo. Itakuwa Tume
tofauti na ya miaka mingine.”
0 comments:
Post a Comment