MGOMBEA urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amepata
kashikashi baada ya polisi kumzuia kumzika mwasisi wa Chama cha TANU na
CCM, Peter Kisumo, kwa madai kuwa wamepata maagizo kutoka juu.
Msafara wa Lowassa ulioanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA), ulikutana na kizuizi cha polisi katika Kijiji cha
Maroro, kilomita moja kutoka Mwanga kuelekea Ugweno, ambako Kisumo
alizikwa jana.
Lowassa akiongozana na viongozi mbalimbali, akiwamo Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Chadema Kilimanjaro, Philemon
Ndesamburo na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema, walikuwa na msafara wa
magari na pikipiki zaidi ya 100.
Licha ya kwamba msafara wa kiongozi huyo ulitoka KIA ukiwa na magari
machache, idadi ya magari na pikipiki iliongezeka kadiri safari
ilipokuwa ikiendelea kutokana na baadhi kujiunga kila alipokuwa akipita.
KIZUIZI
Akizungumza na waandishi wa habari waliokuwapo kwenye msafara huo,
Mbatia alisema kuwa alizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest
Mangu na akawaruhusu kuendelea na safari, lakini Mkuu wa Polisi Mwanga
alikataa kutii agizo hilo.
“Nimeongea na IGP akiwa Kibondo, tukakubaliana na kutoa maelekezo kwa
RPC, lakini tuliporuhusiwa na kuanza kuondoka, ikaja amri kutoka kwa OC
CID akiwa huko juu msibani, ya kwamba hakuna kuruhusu msafara huo, kama
kupanda ni gari moja tu la Lowassa na langu,” Alisema Mbatia na
kuongeza.
“Lowassa ni Waziri Mkuu mstaafu, huwezi kusema eti iende gari moja tu, na pia siye viongozi wengine wanatunyima haki yetu.
“CCM sasa wameamua kuipasua nchi, Serikali ya CCM inatupeleka kwenye
hali ya kutozikana, wametuzuia kwenda kumzika mzee wetu Kisumo, kisa
woga tu.”
Wakati yote hayo yakiendelea, Lowassa na Ndesamburo, walikuwa kwenye magari.
Lakini hata hivyo, baada ya mazungumzo ya muda mfupi, hatimaye majira
ya saa 6:53 mchana, msafara huo uliofika eneo hilo saa 6:42,
uliruhusiwa kuendelea na safari wakitakiwa kuondoa bendera za Chadema
kwenye magari na pikipiki.
WANANCHI WAONDOKA MSIBANI
Mara baada ya kuzagaa kwa taarifa za kuwa Lowassa amezuiwa
kuhudhuria mazishi hayo, baadhi ya wananchi waliondoka eneo la msiba.
Wananchi hao walioonekana kuwa na shauku ya kumwona mgombea huyo
urais wa Ukawa, walisikika wakilalamika kuzuiwa kwake, huku wengine
wakilalamika kuibwa na kunyofolewa kwa bendera zao za Chadema katika
vyombo vya usafiri.
Mbali na hilo pia baadhi ya wanachama wa CCM, walionekana wakiwa
wamezaga sehemu mbalimbali msibani hapo, wakiwa na sare za chama hicho
na bendera zikipepea katika miti iliyokuwa eneo hilo.
UWANJA WA NDEGE
Wananchi wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, walianza kufika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro saa 1:00 asubuhi kumlaki kiongozi
huyo.
Lowassa aliwasili uwanjani hapo saa 2:00 ambapo aliwasalimia mamia ya wananchi waliokuwapo kisha msafara wake ukaondoka.
Baadae msafara huo uliondoka uwanjani hapo kuelekea Moshi ambapo
MTANZANIA ilishuhudia baadhi ya wananchi wakitoka eneo hilo kwa miguu
hadi mjini humo, ikiwa ni umbali wa takribani kilomita 46.
Baada ya kutua mkoani Kilimanjaro, msafara wa Lowassa ukiongozwa na
pikipiki nyingi zikiwa na bendera za Chadema, ulienda moja kwa moja
kwenye Hoteli ya Kiss, iliyoko Kiboriloni, mjini Moshi kwa mapumziko mafupi kabla ya kuelekea Usangi.
Akiwa hotelini hapo, maelfu ya wananchi walivamia wakitaka kumwona Lowassa.
Wananchi hao walizuiwa na walinzi kuingia hotelini humo, kitendo
kilicholazimisha Polisi wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU), kuingilia
kati kutuliza vurugu, lakini hata hivyo waligoma kuondoka.
Baada ya polisi kushindwa kuzuia hali hiyo, Lowassa alitoka na kuzungumza na wananchi hao huku akiwataka kutofanya fujo yoyote.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani
Golugwa, alisema wameandaa mapokezi makubwa ya kuwapokea na
kuwatambulisha Lowassa na mgombea mweza, Juma Hadi Duni, ambao watafika
Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro kesho saa 3:00 asubuhi.
Golugwa ambaye pia ni Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, alisema
baada ya viongozi hao kuwasili uwanjani hapo, msafara wao utaelekea
viwanja vya Tindigani vilivyopo eneo la Kimandolu ambako kutafanyika
mkutano mkubwa wa hadhara wa kuwatambulisha.
“Kesho Jumamosi tutakuwa na mapokezi makubwa ya kihistoria ya
kumtambulisha mgombea urais wa Ukawa kupitia chama chetu, ambapo
watawasili uwanja wa ndege wa KIA na baada ya hapo kutakuwa na msafara
kuanzia uwanjani hapo hadi katika viwanja ya Tindigani, eneo la
Kimandolu,” alisema Golugwa.
Alisema kuwa mbali na kumtambulisha mgombea huyo, pia atapata fursa ya
kutafuta wadhamini ambapo kwenye Kanda ya Kaskazini majimbo mawili
ambayo ni Arusha Mjini na Moshi Mjini yatatoa wadhamini 300 kila moja.
Alisema baada ya kumaliza kuzungumza na wananchi, Lowassa na msafara
wake wataelekea wilayani Monduli ambako pia atakuwa na mkutano wa
hadhara.
Alisema kuwa mgombea huyo ataongozana na viongozi wengine akiwemo
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, manaibu katibu wakuu John Mnyika
na Salum Mwalimu Zanzibar na wenyeviti wenza wa Ukawa kutoka NLD, NCCR
Mageuzi pamoja na viongozi wakuu wa CUF.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment