KAMATI ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekipa
onyo kituo cha utangazaji cha Independent Television (ITV) kutokana na
kutangaza taarifa zisizo za kweli na za uchochezi.
Aidha, imevitaka vituo vya utangazaji nchini kufanya kazi kwa
kuzingatia maadili ili kuzuia uvujifu wa amani na kuwa hawatasita
kuchukua hatua kali kwa watakaokiuka taratibu hizo.
Akisoma hukumu dhidi ya ITV, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Margaret
Munyagi alisema kituo hicho katika kipindi cha ‘Habari zilizotufikia
hivi punde’, kati ya saa 2:00 na saa 5:00 asubuhi, Agosti 10 mwaka huu,
kilitangaza taarifa ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
kupiga marufuku maandamano ya mgombea urais kupitia Umoja wa Vyama vinne
vya upinzani (Ukawa) Edward Lowassa.
“Mtangazaji pia alisikika akisema habari zilizoifikia ITV na Radio
One, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku
maandamano ya Chadema kupitia Ukawa kwenda kuchukua fomu ofisi za Tume,”
alisema.
Munyagi alisema baada ya kuridhika na ushahidi wa video ya taarifa
hiyo na kupokea utetezi kutoka kwa uongozi wa ITV na Radio One, Kamati
imekipa onyo kali kituo hicho na kutakiwa kukanusha habari hizo katika
kipindi cha taarifa ya habari ya saa 2:00 asubuhi na usiku kwa siku
mbili mfululizo.
“Endapo ITV watakiuka kutekeleza adhabu hiyo, kamati yake haitasita
kuchukua hatua kali dhidi ya kituo hicho. Pia ITV inaweza kukata rufaa
ndani ya siku 30 tangu kutolewa kwa hukumu,” alisema.
Awali, katika utetezi wao, uongozi wa ITV na Radio One walisema
habari hiyo haikuwa na msingi wa uchochezi bali lilikuwa ni ombi la
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliyetaka
kukanusha taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa polisi
wamezuia maandamano hayo.
Mkurugenzi wa Radio One na ITV, Joyce Mhavile aliomba radhi kwa kosa hilo na kuahidi kuwa watakuwa makini katika taarifa zao.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment