Rais Jakaya Mrisho kikwete akimsikiliza Meneja wa Klabu bingwa wa Kombe la Kagame na mabingwa wa Tanzania Azam FC walipofika Ikulu jijini Dar es salaam kumkabidhi kombe hilo Ikulu jijini Dar es salaam leo Agosti 6, 2015.
Rais Jakaya Mrisho kikwete akikabidhiwa kombe la ubingwa michuano ya Kagame ya CECAFA na nahodha wa mabingwa wa Tanzania Azam FC walipofika Ikulu jijini Dar es salaam kumkabidhi kombe hilo Ikulu jijini Dar es salaam leo Agosti 6, 2015.
RAIS Jakaya Kikwete ameitaka timu ya Azam kufika kimataifa zaidi kwa kuchukua makombe kutoka katika michuano mikubwa barani Afrika.
Pia amewataka wachezaji wa timu hiyo kuheshimu maadili ya michezo kwa kutojihusisha na matendo ya utovu wa nidhamu badala yake kuwa na dira ya mafanikio.
Kikwete alitoa wito huo alipozungumza na wachezaji na viongozi wa timu hiyo walioenda kumtembelea Ikulu na kumkabidhi Kombe la Kagame walilolitwaa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kuifunga Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0.
Kikwete alisema kuwa Azam imekata kiu ya Watanzania kwa kuwaletea kombe kubwa kama hilo na kuwataka kutobweteka.
Alisema kuwa Azam Fc ni moja kati ya klabu ambazo zinaonekana kujipanga na kupambana na klabu kubwa hasa katika medani ya soka kwa kuwa imejipatia umaarufu na mafanikio makubwa katika soka kwa muda mfupi. Alisema kuwa Watanzania wanapenda soka ingawaje wanakwazwa na mambo mbalimbali ambayo yanarejesha nyuma tasnia hiyo.
“Azam ni klabu ambayo binafsi naona kuwa inaweza kufika mbali zaidi katika soka hasa kutokana na kuwa na umakini wakati imeanzishwa na hadi leo hii inachukua kombe kubwa kama hili la CECAFA, hii ni ishara ya kuwa kama Tanzania ikiwekeza zaidi basi siku moja tutakuwa mbali katika soka,” alisema Kikwete.
Aliwataka kuhakikisha kuwa wanashinda Kombe la Shirikisho Afrika michuano ambayo timu hiyo itashiriki mwakani na kuendelea kuwapatia furaha Watanzania na kusema kuwa klabu hiyo inaweza kufanikisha hilo. Pia alipata wasaa wa kubadilishana mawazo na wachezaji hao akiwa eneo la nje ambapo alisikika akiwataka kuzingatia zaidi mazoezi na kuepuka vishawishi.
“Mimi nawaambieni nyie vijana kuna mengi huko mtaani utakuta unapitapita mitaani na kisha unaitwa na watu wanakukaribisha kinywaji, sasa ukijisahau unaweza kujikuta unaanza kupotea njia na kuwa mlevi na kushindwa kuendelea na soka,” alisema Kikwete.
Aliongeza kuwa: “Kamwe msikwepe kufanya mazoezi bila ya sababu za msingi manake sio wakati wa mazoezi wewe unaitiwa mambo binafsi yasiyokuwa na faida kwa soka na unapotelea huko hiyo sio nzuri”.
Aliwata wachezaji hao kutumia muda wao mwingi kusoma vitabu kutoka kwa wachezaji wengine waliofanikiwa na kuiga mazuri kutoka kwao.
Rais Kikwete pia alikabidhiwa jezi namba tisa kutoka kwa Mwenyekiti wa timu ya Azam, Said Mohamed ambapo alisema kuwa klabu hiyo imeamua kumkabidhi jezi yenye namba hiyo kwa kuwa ni namba ya mashambulizi.
Awali akimwelezea madhumuni ya ujio wao Ikulu, Mohamed alisema kuwa timu hiyo imeamua kwenda Ikulu kumuonesha kombe hilo Rais kutokana na hamasa ambayo Kikwete aliwapa wakati akifungua Uwanja wao wa Azam Complex uliopo Chamanzi, Dar es Salaam.
Alisema kuwa katika kuhakikisha timu hiyo inafika mbali ilijipanga na kuchukua taji la Ligi Kuu msimu wa 2013/ 2014 na msimu wa mwaka 2014/20 15 ikawa ya pili. Aliongeza kuwa baada ya hapo ikahakikisha kuwa inachukua kombe jingine kubwa zaidi ambalo ni CECAFA na ndio imelipeleka kwa Rais kama zawadi yao kwake.
“Mheshimiwa leo tumeleta zawadi hii kwako na ni matunda ya hamasa yako haya, sasa basi tunakuhakikishia kuwa kazi ndio inaanza kwa kuwa tunataka kuleta kombe kubwa la Shirikisho Afrika, CAF,” alisema Mohamed.
0 comments:
Post a Comment