JANA Rais Jakaya Kikwete alikaririwa akisema kuna haja kubwa ya
kuwashughulikia madereva wanaovunja sheria za barabarani kwa kutofuata
taratibu zilizowekwa ili kuepusha ajali na kunusuru vifo nchini.
Alitoa agizo hilo mjini Tanga wakati akizindua Wiki ya Nenda kwa
Usalama Barabarani ikiwa na kaulimbiu ‘Endesha Salama, Okoa Maisha’. Kwa
mujibu wa Rais Kikwete asilimia 56 ya ajali za barabarani zinatokana na
uzembe na ukosefu wa umakini wa madereva.
Rais Kikwete alisema katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka
2010 hadi 2014, watu 19,264 walipoteza maisha kutokana na ajali za
barabarani na idadi ya waliokufa katika kipindi cha mwaka huu pekee ni
3,534 sawa na idadi ya wanaopoteza maisha kwa malaria.
Hii maana yake ni kwamba watu wanaopoteza maisha kwa ajali ni kubwa.
Kinachosikitisha zaidi ni kuwa ajali hizo zinaepukika endapo madereva au
wanaoendesha vyombo vya moto wangekuwa makini.
Kutokana na wimbi hilo la ajali ni wakati muafaka kwa madereva wetu
kubadilika. Kuhakikisha wanazingaria sheria na yale yote waliyofundishwa
vyuoni. Pia, kuna umuhimu wa vikosi vya usalama barabarani kuongeza
kasi ya kuzidhibiti ili kulinda usalama wa wananchi.
Tunaamini kwamba madereva wakizingatia sheria na kuwa makini barabarani kuna uwezekano mkubwa wa kuondokana na ajali.
Kwa mlolongo wa ajali zinazotokea nchini njia pekee ya kuokoa maisha
ya Watanzania ni kila abiria kuwa mkali anapoona dereva anaendesha gari
ovyo ovyo, lakini pia, askari wa usalama barabarani wanatakiwa kuwa
makini katika kudhibiti hali hiyo.
Kwa sababu hiyo madereva ambao hawazingatii sheria ni lazima
wawajibishwe kwani tumechoka kushuhudia ajali za mara kwa mara katika
nchi yetu. Madereva wasipokuwa makini maisha yetu yataendelea kuwa
hatarini.
Ni imani yetu kuwa madereva wataacha kuendesha magari yao kizembe ili
kuepusha ajali za aina hiyo kwani zinapunguza nguvu kazi ya taifa bila
sababu zozote za msingi. Kuna ulazima wa adhabu kali kutolewa kwa
wahusika ili wawe makini barabarani.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment