Image
Image

Ubunge CCM leo ni presha tupu.

Wakati vikao vya  Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vikiwa vimeanza jana mjini Dodoma kwa ajili ya kuchuja majina ya wagombe Ubunge na Uwakilishi, baadhi ya wagombea wamekuwa na hofu kubwa kama majina yao yatateuliwa au ‘yatachinjwa’.

NEC ilianza kikao chake cha siku mbili jana saa 12:02 jioni huku Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, akisema wana kazi ngumu ya kuwapata wagombea ubunge na udiwani kupitia chama hicho, kazi itakayokamilika leo.

"Tuna kazi kubwa sana...ila kazi tuliyoifanya kwenye kamati ya usalama na maadili pamoja na kamati kuu, itatusaidia NEC kurahisha kazi," alisema.

Rais Kikwete aliuliza ni wagombea wangapi ndani ya NEC waliogombea ubunge asilimia kubwa ya wajumbe hao walinyoosha vidole.

"Aisee kumbe ni wengi sana mliogombea kasoro mimi (Rais Kikwete) na Mangula (Makamu mwenyekiti, Philipo Mangula) na Kinana (Katibu Mkuu) ndiyo hatukugombea," alisema.

Awali, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdurahman Kinana alisema jumla ya wajumbe 362 kati 374 sawa na asilimia 96 wamehidhuria kikao hicho.

Hata hivyo, Mgombea wa Urais kupitia chama hicho, John Magufuli naye ameudhuria kwenye vikao hivyo vya NEC

Akifungua kikao hicho, Rais Kikwete, alisema hata hivyo kazi hiyo ngumu imerahisishwa na vikao vya Kamati ya Maadili na Usalama pamoja na Kamati Kuu (CC), ambavyo vimepitia kwa kina majina ya wagombea wote.

Alisema kikao cha NEC kikimalizika majina ya wagombea watakaokuwa yameteuliwa yatatangazwa leo.

Kabla ya NEC kuanza vikao vyake, wajumbe wa kikao hicho na baadhi ya wagombea ambao wamepiga kambi mjini hapa walionekana wakihaha huku na kule na kubadilishana mawazo.

CCM ilianza vikao vyake Jumatatu wiki hii ambapo ilianza kukaa Sekretarieti na kufuatiwa na CC kwa ajili ya kuchambua rufaa na kupitia majina ya wagombea wa ubunge na uwakilishi.

HALI ILIVYOKUWA NJE YA VIKAO
Baadhi ya wagombea walioshinda, wapambe na wale walioshindwa katika kura za maoni walionekana wakirandaranda kila kona ya mji huu.
wagombea waliokata rufaa wakihangaika huku na kule kwenye ofisi za CCM makao makuu wakitaka kujua hatma yao.
Baadhi ya wagombea hao walisema hawajui hatma yao.

WALIOSHINDA ZUNGU
Mgombea wa Ilala, Mussa Hassan Zungu, ambaye alishinda kwa kura 10,457 dhidi ya mkuu wa wilaya wa zamani wa Korogwe, Mrisho Gambo ambaye alipata kura 2038 alisema: "Alichonipangia Mwenyezi Mungu ndiyo hicho hicho nitakachopata."

RWEIKIZA
Naye, mgombea katika Jimbo la Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza alisema NEC ndiyo yenye uamuzi wa mwisho kwani inazingatia maslahi ya wanachama wake pamoja na taifa kwa ujumla.

"NEC haina upendeleo wala haiwezi kumpendelea mtu wala kumdidimiza ila inatenda haki," alisema.
Rweikiza alishinda jimbo hilo kwa kura zaidi ya kura 23,000 dhidi ya Nazir Karamagi.

LUSINDE
Mgombea wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde maarufu Kibajaji alisema hana hofu yoyote kwa sababu aliyeshinda ameshinda.

"Kwenye vikao vya NEC hakuna shida yoyote kwa sababu kanuni zipo wazi, kwani aliyeshinda ameshinda...sina hofu yoyote," alisema Lusinde. 

WALIOSHINDWA
Wagombea walioshindwa katika kura za maoni, walisema bado hawajakata tamaa kwani wana amini NEC inaweza kufanya maajabu.

"Yaani tupo kwenye wakati mgumu...mimi kama mimi mpaka sasa sijui chochote kinachoendelea ila lolote linaweza kutokea," alisema mgombea mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Aliongeza kuwa sasa hivi kila mtu (mgombea) yupo roho juu kwa sababu hajajua hatima yake.

"Unajua unaweza kushika nafasi ya kwanza lakini ukashangaa jina lako limekatwa likachukuliwa jina la pili au la tatu...hivyo bora tusubiri tuone nini itatokea," alisema mgombea huyo.

KAMATI KUU 
Kikao hicho kimekutana wakati mgumu katika kuteua majina ya wagombea ubunge kutokana na kujitokeza kwa malalamiko mbalimbali, huku Kamati Kuu Maalum ya Zanzibar ikutana kwa ajili ya kupitia tena majina yaliyopitishwa na Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT).

WALIOKATIWA RUFAA
Hali imekuwa mbaya zaidi kwa  baadhi ya wagombea waliokatiwa rufaa kutokana na kutojua hatima yao.

Hali hiyo ilitokea juzi mjini hapa ambapo Kamati Kuu ya CCM ilishindwa kumaliza shughuli zake hadi  Zanzibar itakapopitia majina yaliyopigiwa kura na Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake (UWT).

Kamati Kuu iliahirisha kikao chake juzi saa 2:00 usiku ili kupisha masuala hayo yaweze kujadiliwa na Zanzibar.
Kamati hiyo ya Zanzibar ilikutana jana saa 3:00 asubuhi na kumaliza kikao chake saa 7:17 mchana katika Makao Makuu ya CCM 'White House," kwenye ukumbi wa NEC.

Mara baada ya Kamati Kuu Maalum ya Zanzibar kumaliza kikao chake, Kamati Kuu ilianza tena kikao mida ya saa 9:00 jioni.

KILICHOJILI KAMATI YA ZANZIBAR
Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Vuai Ally Vuai alisema kikao hicho kilikutana kwa ajili ya kupitisha majina ya wagombea kutoka Zanzibar waliopigiwa kura na wajumbe wa Baraza Kuu la UWT. 

Alisema kamati hiyo haikupitia majina hayo ya wawakilishi na wabunge kutoka katika makundi mengine ya vijana, wafanyakazi, wazazi, walemavu, NGO's na vyuo vikuu kutokana na vikao kuwa vingi.

"Kwa kweli hatukuwa na kitu kingine kipya zaidi ya kupitia majina hayo tuliyoambiwa na kamati kuu tuyapitie na kuyathibitisha," alisema.

Naye, Naibu Katibu Mkuu UWT Zanzibar, Salama Aboud Talib, alisema kamati hiyo ilipokea malalamiko mengi ya msingi na yasiyo ya msingi.

MAJIMBO KURUDIA UCHAGUZI LEO
Wakati hayo yakiendelea, majimbo matano yanarudia uchaguzi wa kura za maoni leo.
Majimbo hayo yanarudia uchaguzi huo kufuatia uamuzi uliotolewa na Kamati Kuu ya CCM ambayo aliketi na kubaini kasoro mbalimbali wakati wa chaguzi za awali.

Hata hivyo, akitangaza uamuzi huo wa Kamati Kuu juzi, Nape alikataa kutaja sababu zilizopelekea chaguzi hizo kurudiwa, akisema ni masuala ya ndani ya chama.

Majimbo yaliyoamuriwa kurudia uchaguzi huo ni Busega, Kilolo, Ukonga, Makete na Rufiji. Hata hivyo, Jimbo la Kilolo uchaguzi huo ulirudiwa jana.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment