Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR na Shirika la Afya Duniani,
WHO, yametoa wito wa utulivu kufuatia ripoti za kifo cha mkimbizi wa
Burundi kinachoshukiwa kutokana na kirusi cha Ebola, mnamo Agosti 10
2015. Taarifa ya Priscilla
Mkimbizi huyo ambaye alikuwa ameishi katika kambi ya wakimbizi ya
Nyarugusu kwa muda wa miaka mitatu akisubiri kuhamishiwa Marekani,
alifariki dunia katika hospitali ya Maweni katika mkoa wa Kigoma,
Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Mnamo Agosti 9, mkimbizi huyo alipelekwa kwa hospitali ya Maweni,
akiwa anatokwa damu katika ufizi, macho na masikio. Alikuwa pia
amechoka, huku mwili ukiwasha, ingawa hakuwa na homa.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Alvaro Rodriguez
ameiambia idhaa hii kwamba uwezekano kuwa ni Ebola ni mdogo, hata hivyo
Tanzania imejitayarisha kukabiliano na mlipuko wa aina hiyo.
“Kuna mpango wa kitaifa wa kudhibiti Ebola, pamoja na mpango wa
dharura wa Umoja wa Mataifa, kwa hiyo kuna kiwango fulani cha kujiandaa.
Hatuamini kwamba ni kisa cha Ebola, lakini iwapo kisa cha Ebola
kitaibuka, tunaamini kwamba misingi ya kazi imewekwa. Hata hivyo, kama
Afrika Magharibi, itakuwa changamoto kubwa kwa nchi yenye idadi kubwa ya
watu kukabiliana na ugonjwa huo. »
Taarifa ya pamoja ya WHO na UNHCR imesema hakuna ushahidi wowote kuwa
mtu huyo alikuwa amesafiri nje ya mkoa wa Kigoma au kupokea wageni
kutoka nchi zilizoathiriwa na Ebola Afrika Magharibi. Mashirika hayo
yamesema vipimo vya awali pia havijaonyesha dalili za Ebola, na hivyo
shughuli za kila siku zisivurugwe. Vipimo vingine vinafanywa kubaini
ugonjwa uliomuua mkimbizi huyo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment