Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Agosti 18,
2015), wakati akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza mkutano
wa 35 wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)
uliofanyika jijini Gaborone, Botswana.
“Jumuiya ya SADC kupitia sekretarieti yake itabidi
iweke mkakati maamlu wa kufuatilia kama nchi wananchama imeandaa mapango wa
kuendeleza viwanda kulingana na makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao cha leo,”
alisema Waziri Mkuu ambaye ameshiriki kikao hicho kwa niaba ya Rais Jakaya
Kikwete.
Alisema yeye binafsi amefurahishwa na kupitishwa kwa
azimio la uendelezaji wa viwanda katika nchi za SADC kwani unaendana na juhudi
za Serikali ya Tanzania za kukuza uchumi kupitia uendelezaji wa viwanda vya
usindikaji.
“Nimefurahi kwa sababu azimio hili linaendana na
mpango wetu wa kuendeleza viwanda wa mwaka 2015/2016 hadi 2020/2021. Sisi
tumelenga viwanda vya kusindika mazao ya wakulima, wavuvi na wafugaji… kwa hiyo
naamnini tutaenda vizuri na mpango mzima wa Jumuiya hii,” alisema.
Kuhusu madeni ya michango kutoka kwa nchi wanachama
wa Jumuiya hiyo, Waziri Mkuu alisema Tanzania iko kwenye hatua nzuri ya ulipaji
michango hiyo. “Jana nilipofika niliulizia suala hilo, nikaambiwa kwamba
Tanzania imekwishalipa kwa kiwango cha kuridhisha. Nilitoa wito wakamilishe
kulipa hiyo michango iliyobakia kwenye maeneo husika,” aliongeza.
Mapema, Waziri Mkuu Pinda alisoma salamu maalumu
mbele ya wakuu wa nchi na washiriki wa mkutano huo zaidi ya 500, zikiwa ni
salamu maalum za kuwaaga zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete. Rais Kikwete
anamaliza muda wake mwishoni mwa mwaka huu na hatapata nafasi nyingine ya
kushiriki kikao cha wakuu wa nchi.
Kikao kijacho kimepangwa kufanyika Agosti, 2016
nchini Lesotho ambapo Mfalme Letsie Mswati wa III alitumia fursa hiyo
kuwakaribisha wakuu wa nchi wanachama kwenye mkutano huo.
Katika hatua nyingine, wakuu wa nchi za
Jumuiya ya SADC wamechangua Rais Ian Khama Seretse Khama kuwa mwenyekiti mpya
wa Jumuiya hiyo.
Katika kikao hicho waliazimia kuendeleza mapambano
dhidi ya magonjwa ya Kifua Kikuu, Malaria na kuazimia kupunguza maambukizi ya
virusi vya UKIMWI kwenye nchi wanachama.
Mbali na kusisitiza utunzaji na uhifadhi wa
mazingira, waliazimia pia kila nchi itekeleze mpango wake wa kilimo ili kuwa na
akiba ya kutosha hasa ikizingatiwa hali ya ukame ambayo imezikumba nchi za
kusini mwa jangwa la Sahara na kuashiria uhaba mkubwa wa chakula.
Waziri Mkuu anatarajiwa kurejea nchini leo jioni.
0 comments:
Post a Comment