Waziri Mkuu wa zamani wa Lesotho Thomas Thabane, amekana ombi la kurudi nchini peke yake bila ya kufuatana pamoja na viongozi wenzake wa upinzani.
Thabane alisisitiza kwamba ataendelea kubakia Afrika Kusini endapo viongozi wenzake wa upinzani, wanajeshi, mawakili na wanahabari wote walioondoka naye hawatohusishwa.
Miezi kadhaa iliyopita, Thabane pamoja na viongozi wenzake walikwenda uhamishoni Afrika Kusini kwa kudai kwamba maisha yao yalikuwa hatarini nchini Lesotho.
Hivi karibuni, kulikuwa na taarifa zilizotolewa kuhusiana na kurudi kwa Thabane nchini kufuatia makubaliano yaliyotiwa saini kati yake na waziri mkuu wa Lesotho Pakalitha Mosisili.
Akitoa maelezo kuhusiana na taarifa hizo, Thabane alisisitiza kwamba hakukuwa na makubaliano yoyote ya kurudi nchini Lesotho peke yake bila ya kuongozana na wenzake.
Maelezo zaidi yanaarifu kwamba Thabane alitia saini makubaliano ya kurudi nchini pomoja na wenzake wote alioondoka nao.
Nchi ya Lesotho ililazimika kufanya uchaguzi wa mapema mwezi Februari kufuatia jaribio la mapinduzi lililotokea Agosti mwaka jana.
Mosisili alishinda uchaguzi huo na kumteua tena mkuu wa jeshi ambaye alikuwa tayari amefutwa kazi na Thabane kwa madai ya kuhusika na jaribio la mapinduzi.
Baada ya mkuu wa jeshi kuteuliwa, aliamrisha kukamatwa kwa wanajeshi wengi wakiwemo walinzi wa Thabane, jambo ambalo lilimtia hofu waziri mkuu wa zamani na kumlazimu kuenda uhamishoni.
0 comments:
Post a Comment